TIB YAAGIZWA KUHAKIKISHA INACHAGIZA UKUAJI WA MAENDELEO YA UCHUMI WA TAIFA

 

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza jambo wakati wa kikao chake na Uongozi wa Benki ya Maendeleo TIB, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bw. Sosthenes Kewe (wa pili kushoto), baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, jijini Dar es Salaam, ambapo walijadiliana masuala mbalimbali katika kukuza maendeleo ya benki hiyo na uchumi wa Taifa.

……….

Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameiagiza Benki ya Maendeleo ya TIB kuimarisha zaidi mifumo yake ya uendeshaji ili iweze kufikia malengo yake ya kuisaidia Serikali kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika maeneo ya kukuza uchumi wa Taifa na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.

Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ametoa maelekezo hayo Jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB) ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo, Bw. Sosthenes Kewe, kwa lengo la kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu kuimarisha utendaji wa benki hiyo na mchango wake katika kukuza uchumi wa Taifa.

Alisema kuwa ni lazima TIB ijikite katika kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwake kwa kushirikiana na taasisi nyingine za fedha ili iweze kuwa na mchango mkubwa zaidi katika kuwezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuja na mikakati kabambe ya kuwezesha masuala hayo ikiwemo kufuatilia urejeshaj madeni kutoka kwa wateja wake.

“Katika miezi 12 ijayo mnatakiwa kuja na mkakati wa kurekebisha masuala ya fedha na kiwe kipaumbele chenu cha kwanza na Bodi muweke mikakati ya kufanya marejeo kila robo mwaka wa fedha kwa kutumia vigezo vyenu mbalimbali” alisema Mhe. Balozi Khamis.

Wakitoa Taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Benki hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Bw. Sosthenes Kewe na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bw. Deogratius Kwiyukwa, walisema kuwa benki imejipanga kutoa mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 kwa kuchangia upatikanaji wa fedha za kuendeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii.

Walisema kuwa maeneo yatakayopewa kipaumbele katika miaka 25 ijayo ni yale ya kuongeza ajira kupitia miradi ya kilimo kwa kuongeza thamani ya mazao, miradi ya maji, na kufanya mageuzi ya sekta ya fedha ambapo kiasi cha zaidi ya shilingi trilioni 5 kinatarajiwa kuwekezwa katika sekta hizo.

Kwa upande mwingine, mkutano huo ulijadili pia umuhimu wa kufanya mageuzi ya mifumo ya ndani ya kiuongozi, namna ya kupunguza mikopo chechefu (Non-Performing Loans – NPL), kuimarishwa kwa mifumo ya tathmini ya mikopo, ufuatiliaji wa miradi inayofadhiliwa na benki hiyo.