Upigaji kura waendelea Siha, matokeo kutangazwa kesho

Siha. Shughuli ya upigaji kura kumchagua Mbunge wa Jimbo la Siha, mkoani Kilimanjaro inaendelea katika maeneo mbalimbali jimboni humo, huku wananchi 88,000 wanatarajiwa kupiga kura katika vituo 230 vya kupigia kura.

Uchaguzi huo ulisogezwa mbele baada ya aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Daudi Ntuyehabi kufariki dunia Oktoba 7, 2025, baada ya kudaiwa kushambuliwa na kundi la watu waliokuwa wakimtuhumu kuhusika na tukio la kumjeruhi kijana mmoja.

Akizungumza na waandishi wa habari jimboni humo leo Jumanne Desemba 30, 2025, Msimamizi wa uchaguzi, Marko Masue amesema vituo vya kupigia kura vilifungiliwa saa 1:00 na mpaka saa 8:00 mchana, wananchi walikuwa wanaendelea kupiga kura      kwa amani na utulivu.

“Uchaguzi unaendelea vizuri toka asubuhi vituo vilipofunguliwa na kwa Siha tuna vituo 230 na wapiga kura 88,000 wanatarajiwa kupiga kura.”

Ameongeza kuwa, “toka asubuhi nimepita katika vituo vyote hali sio mbaya na mwitikio sio mbaya, hakuna taharuki yoyote watu wana amani wanakuja kupiga kura hakuna changamoto yoyote.”

“Matokeo tutatangaza kesho saa 2:00 asubuhi kutokana na mchakato wa uhesabuji kura unaweza kuwa  mrefu,”amesema.

Vyama vitano vinashiriki uchaguzi huo ikiwamo Chama cha Mapinduzi (CCM), NRA, Makini, ACT – Wazalendo Sauti ya umma (Sau).