URA yapigwa mkwara mzito Mapinduzi Cup 2026

MABINGWA wa Kombe la Mapinduzi mwaka 2016, URA kutoka Uganda, wameambiwa wajiandae kupokea kipigo kutoka kwa watetezi wa michuano hiyo, Mlandege ya Unguja.

Mkwara huo umepigwa na kocha msaidizi wa Mlandege, Sabri Ramadhan ‘China’ muda baada ya kikosi hicho kuanza kwa kichapo cha mabao 3-1 ilichopata kutoka kwa Singida Black Stars.

Desemba 31, 2025, Mlandege inatarajia kucheza dhidi ya URA kwenye Uwanja wa New Amaan Complex ikiwa ni mechi ya kundi A katika mwendelezo wa michuano hiyo. Kundi hilo pia kuna Azam itakayocheza na Singida Black Stars siku hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, China amesema kuanza vibaya katika michuano hiyo imewafanya kurudi uwanja wa mazoezi kujiandaa kivingine kuhakikisha mechi ijayo dhidi ya URA wanapata ushindi kwa namna yoyote ile.

“Mechi ijayo tunahitaji ushindi wa lazima, lakini mpira una mambo mengi, dakika tisini zitaamua nani ataibuka mshindi.

“Tunawaheshimu, lakini tutapambana nao kuhakikisha tunaondoka na ushindi kwani tunataka kukaa sehemu nzuri na si vinginevyo.”

Kwa URA, hiyo itakuwa mechi ya kwanza baada ya ile ya Desemba 28, 2025 dhidi ya Azam kusogezwa mbele hadi Januari 5, 2026.

Mechi hiyo imeahirishwa kutokana na wababe hao wa Uganda kuchelewa kufika Unguja.