Usugu wa vimelea bado tishio nchini

Kuanzia Desemba 2 hadi 5, 2025, Tanzania iliungana na mataifa mengine ya Afrika kwenye mkutano mkubwa wa saba wa African Continental World Antimicrobial Resistance Awareness, ambao mwaka huu umebeba kaulimbiu isemayo “Act now, protect our present, secure our future.”

Kauli hiyo imekuja wakati ambao dunia inakabiliwa na janga jipya linalokua taratibu lakini lenye madhara makubwa kuliko tunavyodhani: usugu wa vimelea dhidi ya dawa unaojulikana kwa kifupi  (UVIDA).

UVIDA ni hali inayojitokeza wakati bakteria, virusi, vimelea na vijidudu vingine vinapoacha kuitikia dawa zilizotengewa kuviua.

Dawa za kufubaza ama kuangamiza vimelea zinaposhindwa kufanya kazi, mgonjwa anahitaji dawa kali zaidi, za gharama kubwa, au hata anakabiliwa na hatari ya kifo.

Wataalam wa afya wanakiri kuwa hii ni miongoni mwa changamoto kubwa zaidi inayotishia mafanikio yote yaliyopatikana katika tiba ya magonjwa ya kuambukiza tangu ugunduzi wa penicillin karibu karne moja iliyopita.

Katika miaka ya karibuni, vimelea vimeendelea kuwa na uwezo wa kujibadilisha kwa kasi kutokana na matumizi makubwa na yasiyo sahihi ya dawa kwenye jamii. Hospitali zimekuwa eneo kuu la kuzalisha vimelea sugu kutokana na matumizi holela ya viuavijasumu kwa wagonjwa wasiohitaji dawa hizo.

Lakini tatizo hili pia linaanzia majumbani, ambapo wananchi wengi bado wana tabia ya kununua dawa bila ushauri wa daktari, kutomaliza dozi walizopewa, au kutumia dawa zilizobaki walizowahi kutumia wakati uliopita.

Kwa mujibu wa wataalam walioshiriki mkutano huo, sababu nyingine kubwa ya kuongezeka kwa usugu wa vimelea ni matumizi ya viuavijasumu kwenye mifugo na kilimo.

Wafugaji wengi hutumia dawa hizo kuzuia magonjwa na kuongeza uzalishaji, lakini madhara yake humfikia mlaji wa mwisho.

Mabaki ya dawa kwenye nyama, mayai, maziwa na mboga yanachangia kuunda mazingira ambayo vimelea vinapata nafasi ya kujifunza na hatimaye kuzoea dawa hizo.

Hili limeongeza kasi ya kutokea kwa vimelea sugu vinavyoathiri binadamu na kusababisha milipuko ya maradhi yanayoshindikana kutibiwa kwa urahisi.

Athari za UVIDA kwa jamii ni pana na zinaongezeka kwa kasi. Kila siku wagonjwa wanafikishwa katika hospitali mbalimbali nchini wakiwa na maambukizi ambayo hayaitiki dawa za kawaida.

Madaktari hulazimika kutumia dawa mbadala zenye nguvu, ambazo mara nyingi ni ghali na zinapatikana kwa ufinyu. Familia ambazo zinategemea kipato cha kawaida hupata mzigo mkubwa wa kifedha, na hivyo kuongeza umasikini.

UVIDA pia inaongeza muda wa kulazwa hospitalini, kupunguza uzalishaji wa kiuchumi na kuongeza gharama kwa serikali kupitia huduma za afya.

Taifa pia linakabiliwa na hatari ya kurudi nyuma katika vita dhidi ya magonjwa ambayo tulidhani tumeyashinda. Magonjwa kama nimonia, kifua kikuu, homa ya matumbo, maambukizi ya mfumo wa mkojo na yale ya upasuaji, yanarudisha sura ya zamani, huku vimelea vinavyozifanya kuwa sugu vikipanuka kimya kimya.

Katika kutafuta suluhisho, mjadala mkubwa umeibuka kuhusu majukumu ya serikali, sekta binafsi na wananchi. Miongozo ya utoaji dawa inahitajika kuimarishwa zaidi, huku maduka ya dawa yanayosambaza viuavijasumu bila cheti kibali cha daktari yakipaswa kuwajibishwa.

Aidha hospitali zinahitaji kuwekeza katika maabara bora ili madaktari waweze kufanya vipimo vya uhakika kabla ya kuandika dawa. Bila mfumo madhubuti wa uchunguzi, madaktari wengi hulazimika kutumia dawa za “kubahatisha,” jambo linalochochea usugu.

Kwa upande wa wananchi, elimu bado ni changamoto kubwa. Watu wengi hawaelewi kuwa viuavijasumu si dawa ya mafua, si dawa ya homa ya kawaida, na si kila maumivu yanahitaji dawa hizo.

Elimu ya mara kwa mara katika vituo vya afya, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii inaweza kusaidia kubadilisha tabia zinazochochea kuibuka kwa vimelea sugu.

Wataalam pia wanashauri kuwepo kwa usimamizi madhubuti wa matumizi ya viuavijasumu kwenye mifugo na kilimo, ikiwa ni pamoja na kuweka kanuni za kitaifa zinazoongoza matumizi ya dawa hizo kwenye sekta hizo.

Mkutano wa mwaka huu umesisitiza kuwa vita dhidi ya UVIDA haiwezi kupiganwa na sekta moja pekee. Hii ni vita ya pamoja inayohitaji ushirikiano kutoka kwenye afya, kilimo, mifugo, mazingira na elimu..

Tanzania tayari imeanza kusimika mikakati ya kitaifa ya kudhibiti usugu wa vimelea, lakini wataalam wanasema kasi inahitajika katika utekelezaji. Bila hatua thabiti, UVIDA inaweza kuwa janga litakalotikisa mfumo wa afya, uchumi na usalama wa Taifa.

Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari