Unguja. Licha ya hali ya amani na utulivu kutawala, idadi ndogo ya wananchi imejitokeza kupiga kura katika uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Fuoni, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Zanzibar.
Hadi saa 7:10 mchana, Mwananchi limeshuhudia mwitikio mdogo wa wapiga kura katika vituo mbalimbali vya kupigia kura tangu vilipofunguliwa saa 1:00 asubuhi.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa mgombea wa Jimbo la Fuoni kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abbas Ali Mwinyi. Kifo cha Abbas kilitokea Septemba 25, 2025, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Mjini Magharibi Lumumba, Zanzibar.
Kutokana na tukio hilo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iliahirisha uchaguzi huo na baadaye kutangaza ratiba mpya ya uteuzi wa wagombea pamoja na muda wa kampeni, hadi Desemba 30, 2025, ambayo ndiyo siku rasmi ya upigaji kura.
Mbali na Jimbo la Fuoni Zanzibar, jimbo jingine linalofanya uchaguzi mdogo leo ni Siha, Mkoa wa Kilimanjaro, pamoja na kata tano kwa upande wa Tanzania Bara.
Asia Haji Mussa akikaguliwa kitambulisho chake na mmoja wa wasimamizi wa wapiga kura (hakutaka kutaja jina lake) katika kituo cha wapiga kura Gamba Mkoa wa Mjini Magharibi. Picha na Jesse Mikofu
Akizungumza baada ya kutembelea vituo vya kupigia kura, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele amesema hali ya uchaguzi ni shwari na wananchi wanaendelea kujitokeza kutimiza haki yao ya kikatiba.
Kwa mujibu wa Mwambegele, mvua iliyonyesha asubuhi imechangia mwitikio mdogo wa wapiga kura, lakini amesema Tume ina imani idadi itaongezeka kadri ya saa zinavyoenda.
“INEC imepita kuangalia mwenendo wa uchaguzi, tayari tumetembelea shehia mbalimbali na tumekuta wapiga kura wamejitokeza kupiga kura licha ya changamoto ya mvua iliyonyesha asubuhi,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa amepokea taarifa kutoka Jimbo la Siha zikionyesha uchaguzi unaendelea vizuri na wapiga kura wanajitokeza.
Aidha, katika kata tano za Tanzania Bara, uchaguzi umeendelea kwa amani na wapiga kura wamejitokeza kupiga kura kama ilivyopangwa.
“Kwa hiyo, kiujumla uchaguzi unaofanyika leo Desemba 30, 2025 katika majimbo mawili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na katika kata tano za Tanzania Bara unaendelea vizuri,” amesema.
Mwenyekiti huyo amewahimiza wananchi katika majimbo hayo mawili kuendelea kujitokeza kwa wingi kuwachagua wabunge wao, huku akieleza kuwa mawakala wa vyama vya siasa husika wamejitokeza katika vituo vya kupigia kura ili kuhakikisha masilahi ya vyama na wagombea wao yanalindwa.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Magharibi B, Miraji Mwadin Haji, amesema Jimbo la Fuoni lina wapiga kura 14,130 na vituo 36 vya kupigia kura vilivyopo katika shehia sita.
Amesema hali ya amani na utulivu katika jimbo hilo inaridhisha, huku akibainisha kuwa hakuna changamoto wala viashiria vyovyote vilivyojitokeza vinavyoweza kuvuruga mchakato wa uchaguzi.
“Asubuhi kulikuwa na changamoto ndogo ya mvua, hali iliyosababisha wananchi kuchelewa kufika vituoni, lakini kwa sasa wanaendelea kujitokeza,” amesema.
Ameongeza kuwa matarajio yao ni kutangaza matokeo leo iwapo hakutakuwa na changamoto yoyote, baada ya vituo kufungwa saa 10:00 jioni na kuanza kwa mchakato wa kuhesabu kura.
Baadhi ya mawakala wa vyama vya siasa wamesema hali katika vituo ni shwari na hakuna changamoto walizokutana nazo. Wamesema wapiga kura wanapotokea, majina yao yanatajwa, yanahakikiwa na kisha kuruhusiwa kupiga kura.
“Kwa kweli hali ni shwari, wapiga kura wanakuja, majina yanakaguliwa na kisha wanaruhusiwa kupiga kura,” amesema Hamrat Haji, wakala wa CCM.
Nao baadhi ya wapiga kura waliozungumza na Mwananchi, wamesema mchakato wa upigaji kura unaenda vizuri bila changamoto yoyote. Shaaban Khamis Haji, mpiga kura katika kituo cha Gamba, amesema amani na utaratibu mzuri vimetawala.
“Kwa kweli hali ni shwari, tumejitokeza kutimiza haki yetu ya kikatiba ya kupiga kura. Tunapongeza utaratibu uliopo, ni mzuri,” amesema.
Kwa mujibu wa INEC, jumla ya vyama 11 vimesimamisha wagombea katika uchaguzi huo mdogo, vikiwemo CCM, ADA-TADEA, Chaumma, Chama cha Wananchi (CUF), DP, NCCR Mageuzi, NLD, SAU, TLP, UMD na ACT Wazalendo.
Hata hivyo, licha ya INEC kueleza kuwa ACT Wazalendo kimeshiriki na kusimamisha mgombea katika uchaguzi huo, uongozi wa chama hicho umesema haujashiriki na ulijiondoa katika uchaguzi huo mdogo baada ya kudai kuwa uliofanyika Oktoba 29, 2025 haukuwa wa haki.
Kwa mujibu wa karatasi za kupigia kura, mgombea wa ACT – Wazalendo, Khamis Shaib Mussa, anaonekana katika orodha ya wagombea.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Katibu wa ACT – Wazalendo, Mkoa wa Magharibi B, Kichama, Salim Ali Khamis amesema chama hicho kilijiondoa rasmi na hakijashiriki katika uchaguzi huo.
“Chama kiliamua kutoshiriki uchaguzi huu baada ya yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu. Kwa hiyo sisi hatupo na hatuna mgombea,” amesema.
Akifafanua sababu ya mgombea wao kuonekana kwenye karatasi za kupigia kura, Salim amesema inawezekana hilo limetokana na matumizi ya karatasi zilizokuwa tayari zimechapishwa awali.
“Huenda ni kweli jina lake lipo kwa sababu katika uchaguzi mkuu tulishiriki, na pengine Tume imeona gharama kubwa kuchapisha karatasi mpya, hivyo ikaamua kutumia zilezile. Lakini sisi hatujashiriki,” amesema, akiongeza kuwa iwapo wananchi wataamua kumpigia kura mgombea huyo, itakuwa ni hiari yao.
Akizungumzia suala hilo, Miraji Mwadin Haji, amesema chama hicho na mgombea wake hawakuondolewa kwenye orodha kwa kuwa INEC haikupokea barua rasmi ya kujiondoa kwao.
“Kama walijiondoa lakini hatukupokea barua rasmi ya kuthibitisha kujiondoa kwao, hivyo mgombea yupo na atapigiwa kura,” amesema.
Hata hivyo, amekiri kuwa ACT Wazalendo hakikuweka mawakala katika uchaguzi huo mdogo.
