Winga Mghana anukia Dodoma Jiji

DODOMA Jiji iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Coastal Union, Mghana Dennis Modzaka baada ya kikosi hicho na nyota husika kufikia makubaliano.

Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zilizonaswa na Mwanaspoti zinadai Modzaka kwa sasa anakaribia kujiunga na kikosi hicho katika dirisha dogo la Januari 2026, ambapo mchakato wa kumrudisha tena kwenye Ligi Kuu Bara unaendelea na uko hatua nzuri.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Dodoma Jiji, Moses Mpunga amesema mchakato utakapokamilika wataweka wazi kwa mashabiki wa timu hiyo, ingawa kwa sasa bado ni mapema kuzungumzia suala hilo kwa sababu hakuna chochote kilichofanyika.

Licha ya kauli ya Mpunga, ila kocha wa timu hiyo, Amani Josiah aliliambia Mwanaspoti kikosi hicho kinahitaji maboresho katika dirisha hili dogo, japo baada ya kurejea kambini kuanzia Januari 4, ndipo atakaa na kuzungumza na viongozi wake.

Mchezaji huyo baada ya kuachana na Coastal Union Januari 24, 2025, alijiunga na kikosi cha AS Vita Club ya DR Congo kwa mkataba wa miezi sita, ingawa kwa sasa anafanya mazungumzo ya kurejea tena katika Ligi Kuu Bara akiwa na Dodoma Jiji.

Nyota huyo alitua nchini mara ya kwanza na kujiunga na Coastal Union, Agosti 6, 2023 akitokea Bechem United ya kwao Ghana, ambapo kwa msimu wa 2023-2024 alifunga bao moja Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho hadi alipoachana nacho.

Bao pekee alilofunga lilikuwa la dakika ya 69 katika ushindi wa Coastal Union wa mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar ugenini kwenye Ligi Kuu, Mei 21, 2024, katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.