BoT yaeleza ugumu wa kudhibiti biashara holela ya fedha mpakani Tunduma

Dar es Salaam. Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema kudhibiti biashara holela ya kubadilisha fedha mitaani katika mpaka wa Tunduma ni changamoto kutokana na tabia ya watu wa eneo hilo kutokukaa mahali pamoja.

Tutuba ametoa kauli hiyo alipozungumza na Mwananchi leo, Desemba 30, 2025 kuhusu kushamiri kwa biashara hiyo katika mpaka huo.

Amesema kimsingi watu hao wanavunja sheria, ingawa kudhibiti shughuli zao ni changamoto, hususan mipakani. Ugumu huo unatokana na tabia ya watu hao kutokukaa eneo moja, wanavuka huku na kule, hivyo udhibiti unapofanyika sehemu moja, wanahamia kwingine.

“Ni vigumu kudhibiti watu wanaohamahama. Waliwahi kuzuiwa wakahamia darajani ambako ni nchi nyingine. Kuna kipindi tuliwapa hadi nafuu waje wafungue maduka, lakini bado wale wanaotembea barabarani wamekuwepo,” amesema.

Pia ameeleza ni vigumu kudhibiti hali hiyo kwa kuwa watu hao hawana uwezo wa kurasimisha biashara zao, kwani hawana mitaji inayohitajika kisheria ya Sh200 milioni ili kupata kibali cha kufanya biashara ya fedha za kigeni.

“Wale ni kama day workers, anaweza akawa na Sh5 milioni akaendelea na biashara kwa njia hizo. Mazingira ya mipakani ni tofauti na maeneo mengine,” amesisitiza.

Amesema ili kuwa na uhalali wa kufanya biashara ya fedha za kigeni kwa mujibu wa sheria, mfanyabiashara anapaswa kuwa na mtaji wa kuanzia Sh200 milioni na pia awe na ofisi, vigezo ambavyo wengi wa mipakani hawana.

Hata hivyo, ameeleza kadiri siku zinavyoenda, BoT itaandaa mkakati wa kuhakikisha biashara hiyo inadhibitiwa na kila anayefanya biashara ya fedha za kigeni anarasimisha shughuli zake.

Hakuna takwimu rasmi za kiasi cha fedha kinachobadilishwa kiholela mpakani Tunduma, lakini kwa kuzingatia idadi ya watu na magari yanayopita eneo hilo kila siku, ni fedha nyingi zinabadilishwa, kama anavyoeleza Watenas Maneno (si jina lake halisi), mmoja wa vijana wanaofanya biashara hiyo.

Amesema ni vigumu kutabiri kiwango cha faida kwa siku, lakini anakadiria kupata wateja kati ya 20 hadi 30 nyakati ambazo biashara imechangamka.

Ingawa yeye ndiye anayeonekana barabarani akifanya biashara, anasema kiuhalisia si yeye anayemiliki fedha hizo, yupo bosi wake mwenye vijana takribani wanane mpakani hapo, wote wakizungusha fedha.

“Unadhani ni za kwangu? Natoa wapi hela zote hizi? Zote ni za bosi, sisi tunalipwa kutokana na mauzo ya siku, ukiuza sana unapata hata Sh15,000 kwa siku, ukiuza kidogo unapata Sh10,000 na wakati mwingine Sh5,000,” anasimulia huku akisisitiza kulindwa kwa taarifa zake.

Ameeleza kuwa, ukiacha wao wanaoshika fedha na kubeba mabegi, kuna vijana wengine waliowekwa kando ya barabara kuwalinda wasitoroke na fedha, ambao ni vigumu kuwajua, lakini ukijaribu kuharibu au kutoroka ndipo wanapotokea.

Amesema hajui kuhusu vibali, risiti wala taarifa za miamala, anachokijua ni kuuza fedha na kupokea fedha. Hata bosi wao hana duka, badala yake kila mmoja hupelekwa kwenye eneo lake kupokea mzigo na kuanza kufanya biashara.

Kila muamala unaofanyika mitaani ni mapato yanayopotea kwa njia mbili. Kwanza, Serikali hukosa kodi na ada zinazopaswa kulipwa na biashara halali, pili, hukosa taarifa muhimu za mzunguko wa fedha zinazosaidia kupanga sera za kifedha na kudhibiti mfumuko wa bei, kwa mujibu wa Profesa Benedict Mongula, mtaalamu wa uchumi.

“Kwa maneno mengine, Serikali inapoteza si tu fedha, bali pia udhibiti wa mfumo wake wa fedha mpakani,” amesema mwanauchumi huyo.

Hatari ya kusambaa fedha bandia, utakatishaji

Zaidi ya hasara ya mapato, Profesa Mongula amesema biashara hiyo inaibua hatari za kiusalama na kifedha. Kutokuwepo kwa ufuatiliaji kunatoa mwanya wa kuingiza fedha bandia, fedha zinazotokana na uhalifu au hata fedha zinazotumika kufadhili shughuli haramu.

Katika mazingira ya mpakani, ambako biashara ya madini, mafuta na bidhaa nyingine zenye thamani kubwa hupita, anasema uholela wa kubadilisha fedha unaweza kuwa lango la utakatishaji wa fedha bila mamlaka kugundua.

“Unapokuwa na soko la fedha lisilo rasmi mpakani, unafungua mlango wa hatari ambazo athari zake zinaweza kufika mbali zaidi ya Tunduma,” amesisitiza.

Kuhusu kusambaa kwa fedha bandia, dereva wa lori, Gugu Abdulsalim, amesema mara nyingi vijana hao husambaza Kwacha bandia kwa wateja wasiokuwa na uelewa mzuri wa fedha ya Zambia.

Amesema hata yeye amewahi kuuziwa fedha bandia za Zambia kutoka kwa vijana hao na hakuwa na cha kufanya zaidi ya kumtafuta aliyemuuzia, ambaye hakumuona tena.

“Hapa upigaji upo wa kutosha. Unapigwa fedha bandia na huna wa kumtafuta. Kwa hiyo, ndivyo maisha ya hapa Tunduma,” amesema dereva huyo.

Kwa nini wananchi wanakimbilia mitaani?

Kwa nini biashara hii inaendelea kushamiri? Abdulsalim amesema hakuna maduka halali ya kubadilisha fedha katika eneo hilo, benki nazo ziko mbali na hufunga mapema. Wateja wengi wanahitaji fedha haraka, hasa madereva waliokaa kwenye foleni kwa siku kadhaa.

Hata hivyo, amesema kwa vijana wanaofanya biashara hiyo, ni suala la kuishi. Ukosefu wa ajira umewasukuma kuingia kwenye biashara isiyo rasmi lakini yenye mzunguko mkubwa wa fedha.

Ni saa tatu asubuhi mpakani Tunduma mkoani Songwe. Foleni ya malori haijasogea hata mita 100, lakini biashara nyingine inaenda kwa kasi ya ajabu.

Eneo linaitwa Kilimanjaro. Sio ile ya Kaskazini mwa Tanzania, hii ni Tunduma mkoani Songwe, ulipo mpaka wa Tanzania na Zambia na ni kiungo cha kuingia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Katika eneo hilo, ninakaribishwa na kijana aliyevalia mavazi chakavu, lakini mkononi anashika maburungutu ya fedha. Kwacha za Zambia katika mkono mmoja na Shilingi za Tanzania mkono mwingine.

Ukiacha alizoshika mikononi, pembeni kulikuwa na begi dogo lisilofungwa vizuri. Nalo lilijaa maburungutu ya fedha ambayo, kwa kuangalia tu, ingetosha kusema ni mamilioni.

Kadiri nilivyosogea katika mzunguko wa barabara (roundabout) wa eneo hilo, ndivyo kijana alivyonisogelea kunionesha fedha bila kusema chochote. Nami nilionesha ishara ya kukataa bila kutoa sauti.

Sikumaliza hata hatua 10, nikakutana na mwingine mwenye mavazi yenye hali sawia na yule wa awali, mikononi akishika vibunda vya fedha, naye akinionesha fedha, nikampita kama sikuoni.

“Hapa kubadilisha pesa, boss… rate nzuri,” kijana mwingine ananong’ona huku akikunja fedha mkononi kama ishara ya uhalisia wa biashara yake.

Kiuhalisia, huyu ndiye aliyefanya nibaini kuwa ile fedha nilichoonyeshwa ilikuwa ni biashara. Hakukuwa na bango. Sikuona kibali. Wala risiti, lakini wateja hawakupungua.

Hii si biashara ndogo ya pembeni. Ni mfumo usio rasmi wa kifedha unaofanya kazi hadharani kila siku, mbele ya macho ya mamlaka, na unaoiacha Serikali ikipoteza mapato bila takwimu wala kumbukumbu.

Huo ni muhtasari wa machache kati ya mengi yanayoendelea katika biashara ya ubadilishaji fedha mpakani Tunduma. Unaweza kusema ni Bureau de Change zinazotembea.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini biashara hii ya kubadilisha fedha mitaani imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku mpakani Tunduma.

Vijana hawa, wengi wao wakiwa hawajulikani rasmi, hufanya miamala ya mamilioni ya shilingi kwa siku, wakihudumia madereva wa malori, wafanyabiashara wadogo, wasafiri na hata baadhi ya mawakala wa mizigo.

Miamala hufanyika kwa kasi. Mteja akitaja kiasi, “rate” huamuliwa papo hapo. Hakuna rejea ya viwango rasmi vya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Hakuna uthibitisho wa chanzo cha fedha. Hakuna ufuatiliaji wa muamala.

Kwa mujibu wa sheria za fedha nchini, biashara ya kubadilisha fedha inapaswa kufanywa na taasisi zilizosajiliwa, zenye leseni ya BoT.

“Hairuhusiwi kwa mtu yeyote au taasisi yoyote kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila kuwa na leseni halali iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania,” kinaeleza Kifungu cha 3 cha Kanuni za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni za mwaka 2023.

Hata hivyo, kanuni hizo zinazitaka taasisi zilizopewa vibali vya kufanya biashara hiyo kutoa taarifa za miamala, kulipa kodi na kufuata taratibu za kupambana na utakatishaji wa fedha. Lakini Tunduma, kanuni hizo zinaonekana kubaki kwenye vitabu.