Chalamila aeleza mafanikio, changamoto mwaka 2025 Dar

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameainisha mafanikio na changamoto zilizojitokeza mwaka huu na hatua zilizochukuliwa katika kuzitatua.

Miongoni mwa mafanikio hayo kuanza kwa ujenzi wa madaraja la Jangwani, Kigogo na Kikwajuni, wakati changamoto zikiwa ni mafuriko, ukame (uhaba wa maji) na foleni alizodai zilikuwa zinasimamisha uchumi wa mkoa huo kwa wakati fulani.

Chalamila ameeleza hayo leo Desemba 31, 2025 alipokuwa akitoa tathimini ya utekelezaji wa majukumu ya serikali ndani ya mkoa huo na mipango waliyojiwekea kwa mwaka mpya 2026.

Akianza kuzungumzia kero, Chalamila amesema kero kubwa kwa mwaka uliopita ilikuwa mafuriko, ambayo mara kwa mara yalisababisha kufungwa kwa barabara muhimu za kiuchumi zinazounganisha wilaya mbalimbali.

Amesema maeneo yaliyoathirika zaidi ni barabara ya Morogoro Road eneo la Jangwani, daraja la Kigogo na Kikwajuni, ambapo kila mvua kubwa iliponyesha maji yalijaa na kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara hizo.

“Mathalani eneo la Jangwani, daraja la Kigogo na Kikwajuni yalikuwa hayapitiki wakati wa mvua kutokana na maji kujaa, hali iliyolazimisha shughuli za kiuchumi kusimama,” amesema Chalamila.

Ili kutatua changamoto hiyo, Chalamila amesema serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa madaraja hayo ambapo daraja la Jangwani linajengwa kwa gharama ya Sh97 bilioni na linatarajiwa kukamilika mwaka 2026/27.

Wakati daraja la Kigogo linajengwa kwa Sh17.7 bilioni huku daraja la Kikwajuni likijengwa kwa Sh11 bilioni.

“Fedha hizi zimetolewa ili kuhakikisha madaraja yanakamilika kwa wakati na barabara zinazoingia mjini na kutoka zinapitika wakati wote, kwani zilikuwa kero kwa muda mrefu,” amesema Chalamila.

Kwa upande wa Barabara ya Kilwa, kipande cha Mbagala Rangi Tatu hadi kuvuka Mto Mzinga kuelekea Kongowe, Chalamila amesema kumekuwapo malalamiko mengi kutokana na ajali za mara kwa mara zilizosababisha vifo na ulemavu wa kudumu.

“Barabara ilikuwa nyembamba na ajali zilikuwa nyingi, baadhi ya wananchi walipoteza maisha na wengine kupata ulemavu wa kudumu,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, Chalamila amesema serikali imetoa Sh54 bilioni kwa ajili ya upanuzi wa barabara hiyo, ambapo ujenzi umefikia asilimia 25.

Ameongeza kuwa kwa barabara zote zinazomilikiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), mkoani Dar es Salaam, serikali imetenga jumla ya Sh900 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu.

Kwa barabara hizo zinazosimamiwa na Tarura, Chalamila amesema ujenzi unaendelea kupitia Mradi wa DMDP Awamu ya Pili, unaohusisha kilomita 250.

“Tayari mikataba 21 yenye jumla ya kilomita 158 imesainiwa, ikigharimu Sh438 bilioni. Ujenzi umefikia kati ya asilimia 28 hadi 40,” amesema, huku akiwasihi wananchi kutoa ushirikiano.

Amesema bado mikataba michache haijasainiwa kutokana na hatua za ulipaji fidia, lakini na itakapokamilika wakandarasi wataanza kazi.

Katika tathmini yake, Chalamila amesema mkoa wa Dar es Salaam ulikumbwa na ukame uliosababisha upungufu wa maji baada ya kushuka kwa kina cha maji katika Mto Ruvu kinachotegemewa.

Hata hivyo, amesema mvua zilipoanza kunyesha, uzalishaji wa maji umeanza kurejea katika hali ya kawaida.

Ameeleza kuwa serikali inaendelea na mpango wa kudumu wa kukabiliana na tatizo la maji, ikiwemo ujenzi wa Bwawa la Kidunda mkoani Morogoro, lenye uwezo wa kuhifadhi lita bilioni 100 za maji.

“Bwawa hili litahudumia mikoa ya Dar es Salaam na Pwani hasa kipindi cha ukame. Ujenzi umefikia asilimia 40 na unatarajiwa kukamilika mwaka ujao,” amesema Chalamila.

Ameongeza kuwa serikali pia ina mpango wa kuchukua maji kutoka Mto Rufiji kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam, Pwani na maeneo mengine jirani.

Chalamila amesema Shirika la umeme Tanzania (Tanesco), limefanya kazi nzuri katika kusambaza umeme mkoani humo, huku akisisitiza kuwa kinachobaki ni kuimarisha miundombinu ya usafirishaji wa umeme na ujenzi wa vituo vya kuongeza nguvu ya umeme.

Akizungumzia maandalizi ya mwaka 2026, Chalamila amesema mkoa umejipanga vyema katika sekta ya elimu kupokea wanafunzi wote wapya.

Amesema jumla ya wanafunzi 95,323 wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza, huku miundombinu ikiwa tayari ikiwemo ujenzi wa majengo ya maghorofa katika baadhi ya shule.

Kwa elimu ya awali, amesema watoto zaidi ya 135,279 wanatarajiwa kuanza masomo na hakuna atakayekosa nafasi darasani.

Amehimiza wazazi kuhakikisha wanawapatia watoto mahitaji muhimu ya shule, ikiwemo madawati yatakayokidhi idadi ya wanafunzi.

Chalamila amesema Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa itakayofanya majaribio ya mfumo wa bima ya afya kwa wote katika siku 100 za mwanzo wa utekelezaji za serikali.

“Tumejipanga kuweka mifumo mizuri ili wananchi wetu wanufaike moja kwa moja na mpango huu,” amesema.

Kuhusu utoaji wa miili ya marehemu, Chalamila amesema mkoa umeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha hakuna urasimu ili kuunga mkono mipango ya serikali na maelekezo ya Wizara ya afya.

“Kama kutakuwa na changamoto yoyote, wananchi wawasiliane na ofisi za wakuu wa wilaya ili kuepuka usumbufu,” amesema.