CRDB BANKI YAWAKABIDHI MAGARI, SIMU NA UFADHILI WASHINDI WA SIMBANKING

:::::::::


Benki ya CRDB kupitia huduma yake ya SimBanking imewakabidhi zawadi mbalimbali washindi wa kampeni yake ya SimBanking kwa mwaka huu, zikiwemo magari, simu za mkononi pamoja na ufadhili wa masomo.

Miongoni mwa washindi waliokabidhiwa zawadi hizo ni Deo Mlawa, mteja wa Benki ya CRDB kutoka Tawi la Mikocheni, ambaye amejishindia gari aina ya Toyota Harrier.

Washindi wengine wamekabidhiwa zawadi zikiwemo gari aina ya Toyota IST, simu za mkononi aina ya iPhone 17, pamoja na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).

Hafla ya ugawaji wa zawadi hizo imefanyika katika Tawi la Dar Village lililopo Mikocheni, ikihudhuriwa na viongozi wa benki pamoja na wateja mbalimbali.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya CRDB, Bonaventura Paul, amesema zaidi ya asilimia 95 ya miamala ya kibenki kwa sasa inafanyika kupitia huduma ya SimBanking.

Amesema kampeni hiyo iliyokuwa na kaulimbiu ya *“SimBanking ni Humu Tu”* ilihusisha utoaji wa zawadi kila baada ya miezi miwili, ambapo benki ilikuwa ikitoa gari aina ya Toyota IST kwa washindi waliobahatika.

Kwa mujibu wa Paul, hadi kufikia mwisho wa kampeni hiyo, jumla ya magari manne aina ya Toyota IST yalitolewa kwa washindi mbalimbali nchi nzima.

Benki ya CRDB ilizindua huduma ya SimBanking mwaka 2009 ikiwa na lengo la kuwaunganisha Watanzania na huduma za kifedha, pamoja na kuwawezesha kutekeleza shughuli zao za kila siku kwa urahisi, haraka na usalama.