Dk Godwin Mollel ashinda ubunge Jimbo la Siha

Siha. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imemtangaza aliyekuwa mgombea ubunge wa Chama chama Mapinduzi (CCM),  Dk Godwin Mollel kuwa ndiye Mbunge wa Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro.

Uchuguzi huo ulisogezwa mbele baada ya aliyekuwa mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF) Daudi Ntuyehabi kufariki dunia Oktoba 7, 2025, baada ya kudaiwa kushambuliwa na kundi la watu, wakimtuhumu kuhusika na tukio la kumjeruhi kijana mmoja.

Akitangaza matokeo hayo usiku wa Desemba  30, 2025  Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo hilo, Marko Masue amesema Dk Mollel amepata kura 51,769 sawa na asilimia 78.4 huku mpinzani wake wa chama cha NRA, Ntaana Thobias akipata kura 4,992 sawa na asilimia 7.56.

Msimamizi huyo wa uchaguzi, amesema mgombea ubunge wa Chama cha ACT Wazalendo, Ashukuriwe Matemu amepata kura 3,678 sawa na asilimia 5.57, Mgombea wa chama cha Sauti ya Umma (SAU), Mdoe Ambazi amepata kura 3,128 sawa na asilimia 4.74 akifuatiwa na mgombea wa Chama cha Makini, Daniel Nsila aliyapata kura 2,007  sawa na asilimia 3.04.

“Kwa matokea haya namtangaza Dk Godwin Mollel wa chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba ndiye mshindi wa ubunge wa Jimbo la Siha,”amesema Msimamizi huyo wa uchaguzi