MZAWA wa kwanza kutoka Ligi Kuu Bara kufunga bao katika michuano ya AFCON 2025, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameeleza furaha aliyonayo ya kuivusha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ hatua ya 16 Bora, huku akiwataja makocha wawili ambao wamempa nguvu ya kufanya hivyo.
Katika fainali mbili zilizopita za AFCON 2019 na 2023 wafungaji wa mabao Stars wote walikuwa wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi, lakini Fei amefunga akiwa mmoka kati ya wachezaji wawili wa Ligi Kuu waliotupia mwaka huu akiwamo Prince Dube wa Zimbabwe.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fei alisema, kwake anaona ni mwanzo wa rekodi kubwa kwenye safari yake ya soka, jambo ambalo alikuwa akiliota muda mrefu na sasa limetumia.
Alisema, ushindi huo hatauchukua binafsi ila anawapa makocha wake wakubwa wawili ambao wakati wote wamekuwa na imani nay na kumpa morali ya kwamba anaweza kubadilisha mhezo wakati wowote.
“Nimeamini kwenye maisha kila kitu kinawezekana kikubwa ni imani na utii haya mengine yote yanapatikana kirahisi tu ukiwa na nidhamu ya kufanya kile ulichoagiza. Bao langu nawapa makocha wawili, awali ni Miguel Gamondi ambaye amekuwa akinipa imani kwamba timu inahitaji ubunifu wangu hasa kwenye eneo la kati.
“Wapili kuna kocha mwingine wa nje siwezi kumtaja alinitaka kujituma kagtika mechi ya mwisho huku akiniambia kama nitafanya hivyo naweza kufunga na imekuwa kweli.”
Stars itakwenda kucheza dhidi ya Morocco hatua ya mtoano ya 16 Bora katika michuano hiyo ya Afcon, mchezo utakaopigwa nchini Morocco Jumapili, Januari 4.
Fei amewatoa hofu mashabiki wa Stars akisema, licha ya kwamba mechi hiyo itakuwa na ugumu kutokana na ubora wa wapinzani wao lakini bado watapambana kufanya vyema.
“Morocco sio timu rahisi ukizingatia tuko kwao ila ninaimani sana na timu yetu kwamba itakwenda kufanya makubwa, Ijapokuwa haitakuwa mechi rahisi lakini tutajipanga kwa kuwa na tuna makocha wazuri kama Gamondi.”
Ikumbukwe kuwa hii sio mara ya kwanza kwa Fei kuifunga Tunisia, kwani ameshawahi kuwatandika Mwaka 2021, Yeye mwenyewe alisema: “Imekuwa rekodi iliyojirudia tu sio kwamba nawajua sana kwa sababu hata wao kikosi chao kimebadilika kidogo ila mbinu za makocha na wachezaji wenzangu zimenisaidia pia.”
