Fundi aliyebomoa ukuta ni miongoni mwa mashahidi 55, kesi kuporomoka jengo Kariakoo

Dar es Salaam. Mashahidi 55 na vielelezo 54 vinatarajiwa kutolewa mahakamani katika kesi ya kuua bila kukusudia  inayotokana na kuporomoka kwa jengo  Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, inayowakabili wafanyabiashara wanne wa jiji la Dar es Salaam.

Washtakiwa katika kesi hiyo  ni  Leondela Mdete (49) mkazi wa Mbezi Beach, pamoja na wenzake watatu ambao ni Soster Nziku (55) mkazi wa Mbezi Beach, Aloyce Sangawe(59) mkazi wa Sinza na Stephen Nziku (28) mkazi wa Mbezi Beach.

Mdete na wenzake ambao wote ni wafanyabiashara wanakabiliwa na shtaka la kuua 31 bila kukusudia, tukio wanalodaiwa kulitenda  Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022

Wanadaiwa siku hiyo ya tukio, isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha vifo vya watu 31.

Mashahidi hao wanatarajia kutoa ushahidi wao, Mahakama Kuu, na hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mshtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Wakili wa Serikali, Christopher Olembelle akishirikiana na Neema Kibodya, ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu  jana Desemba 30, 2025, mbele ye Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya Jamhuri kuwasomea maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Wakili Olembelle alitoa maelezo hayo, wakati akimsomea maelezo ya mashahidi na vielelezo mshtakiwa huyo.

Katika mashahidi hao 55, yupo Lusekelo Mwakyami ambaye Mhandisi wa ujenzi wa majengo ya Serikali pamoja na fundi ujenzi aliyehusika kuvunja ukuta wa jengo hilo kwa kutumia nyundo aitwaye James Markos.

Vilevile yupo,  Zenabu (61) na Ashour Awadh Ashour(38), ambao hapo awali walikuwa ni washtakiwa katika kesi hiyo, lakini jana DPP aliwafutia mashtaka yao na kuwaachia huru, hivyo kwa sasa ni  mashahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi hiyo.

Mashahidi wengine ni Said Omay ambaye ni Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Kariakoo Magharibi.

Mashahidi wengine ni askari Polisi, wafanyabiashara wa nguo waliopanga katika jengo hilo, wamachinga, walinzi wa jengo hilo, wamiliki wa jengo hilo na fundi ujenzi aliyehusika kuvunja ukuta wa jengo hilo kwa kutumia nyundo  pamoja na daktari.

Alivitaja vielelezo kuwa ni maelezo ya onyo ya washtakiwa, maelezo ya mashahidi, ripoti ya hospitali.

Kabla ya kusomewa kwa maelezo hayo, wakili  Olembelle  alieleza Mahakama hiyo kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa wawili kati ya washtakiwa wanne wanaokabiliwa na kesi hiyo

‎”Mheshimiwa hakimu, DPP amewasilisha hati ya kutokuendelea na kesi hii kwa washtakiwa wawili, ambao ni Zenabu na Ashour  chini ya kifungu cha 92 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya mwaka 2023″ alidai wakili Olembelle na kuongeza

“Kutokana na hati hii, tunaomba Mahakama itumie kifungu hicho kuwafutia mashtaka na kuwaachia huru washtakiwa hawa wawili,”alisema.

‎Uamuzi huo wa kuwafutia kesi washtakiwa hao wawili, umetolewa na hakimu Mhini, baada Jamhuri kuwasilisha maombi hayo.

Baada ya kuwaondoa washtakiwa hao wawili, Jamhuri ilibadilisha hati ya mashtaka kwa kuondoa washtakiwa wawili na kubaki washtakiwa wanne na kisha kuwasomea upya mashtaka yao

Akisoma baadhi ya maelezo ya mashahidi, wakili Olembelle alisema shahidi wa tatu katika kesi hiyo, James Markos ambaye alikuwa fundi ujenzi katika jengo hilo, alidai kuwa yeye na wenzake walilipwa Sh1 milioni kwa ajili ya kuvunja kuta kwa kutumia nyundo kubwa yenye uzito wa kilo tisa na shughuli ya kuvunja ilianza Novemba 14, 2024 na Novemba 16, 2024 wakati wakiendelea na kazi katika jengo hilo, waliona linashuka na ndipo walipotoka lakini kabla hawajafika nje walidondokewa na ukuta na hivyo kuokolewa, kisha kupelekwa hospitali kwa kutumia usafiri wa bajaji.

Katika maelezo hayo, James alidai kuwa wakiwa wanabomoa ukuta wa jengo hilo, walibaini zege iliyokuwa imemiminwa kwenye nguzo ilikiwa hafifu na hata matofali yaliyotumika kujengea jengo hilo hayakuwa na saruji ya kutosha.

Hivyo  wakati wote wa ubomoaji wa ukuta wa jengo hilo, hafahamu kama kulikuwa na mkandarasa wala mhandisi aliyekuwa anatembelea jengo hilo.

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza maelezo hayo, alisema kesi hiyo anaihamishia Mahakama Kuu, ambapo itapangiwa tarehe kwa ajilia ya kuanza  kusikilizwa ushahidi.

“Washtakiwa mtaendelea kuwa nje kwa dhamana, mkisubiri kupangiwa tarehe kwa ajili ya kuanza usikilizwaji wa shauri lenu Mahakama Kuu” alisema Hakimu Mhini.

‎Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kinyume na kifungu 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

‎Kwa pamoja wanadaiwa Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo, washtakiwa hao isivyo halali walishindwa kutimiza majukumu yao na kusababisha kifo cha Said Juma.

Katika shtaka la pili hadi la 31, washtakiwa hao siku na eneo hilo wanadaiwa kusabisha kifo cha Hussein Njou, Prosper Mwasanjobe, Shadrack Mshingo, Godfrey Sanga, Neema Sanga, Elizabeth Mbaruku, Hilary Minja, Abdul Sululu na Catherine Mbilinyi.

‎Vile vile, wanadaiwa kusababisha kifo cha  Elton Ndyamukama, Mariam Kapekekepe, Elizabeth Kapekele, Hadija Simba, Frank Maziku, Rashid Yusuph, Ally Ally, Ajuae Lyambiro, Mary Lema na Khatolo Juma.

Walisababisha pia, kifo cha Sabas Swai, Pascal Ndunguru, Brighette Mbembela, Ashery Sanga, Venance Aman, Linus Hasara, Pascalia Kadiri, Issa Issa, Lulu Sanga, Happyness Malya na Brown Kadovera.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo Novemba 29, 2024 na kusomewa mashtaka ya 31 ya kuua bila kukusudia katika kesi ya mauaji namba 33633/2024.