Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Januari 15, 2026 kutoa hukumu katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi inayomkabili, Kulwa Mathias (32) na mwenzake Edina Paul.
Mathias ambaye ni mkazi wa Shinyanga na Edina mkazi wa Urambo, mkoani Tabora, wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 512.50.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 11, 2024 eneo la ukaguzi wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam, ambapo walikutwa wakisafirisha kiasi hicho, kinyume cha sheria.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumatano Desemba 31, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Hassan Makube , baada ya washtakiwa hao kumaliza kujitetea.
“Baada ya washtakiwa kumaliza kutoa utetezi wao, mahakama hii inapanga Januari 15, kutoa hukumu dhidi yenu” amesema Makube na kisha kuahirisha kesi hiyo.
Hata hivyo Kulwa yupo ndani huku Edina akiwa nje kwa dhamana.
Awali, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Adolf Verandumi alidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya upande wa utetezi kujitetea na wapo tayari kusikiliza utetezi huo.
Katika ushahidi wake Mathias alidai kuwa hahusiki na shtaka hilo na hajawahi kukamatwa na jeshi la polisi
Pia alidai kuwa hamfahamu Edina, bali amekuja kumuona walipofikishwa mahakamani, hivyo anaomba mahakama imuachie huru.
Kwa upande wake Edina alidai kuwa Mathias alimchukua kutoka Tabora kwa madai kuwa anataka kumuoa na pia alimueleza kuwa anafanya kazi Zanzibar, hivyo wataenda kuishi wote.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, upande wa utetezi ulifunga ushahidi wao na kisha mahakama kupanga tarehe kwa ajili ya kutoa hukumu ambayo ni Januari 15, 2026.
Desemba 24, 2025 washtakiwa hao walikutwa na kesi ya kujibu na kutakiwa kuanza kujitetea Desemba 30, 2025.
Hatua hiyo ilitokana na Mahakama kupitia ushahidi wa mashahidi 12 na vielelezo 11 vilivyotolewa na upande wa mashtaka na hivyo kuwakuta na kesi ya kujibu.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 5, 2025 na kusomewa kesi ya jinai namba 5543 ya mwaka 2025 yenye shtaka moja la kusafirisha bangi.
