Jenerali Doumbouya ashinda Urais Guinea, hujuma ya kuzimwa mitandao yatajwa

Guinea. Jenerali Mamady Doumbouya amechaguliwa kuwa Rais wa Guinea baada ya kupata kura nyingi, kulingana na matokeo ya awali ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, huku hoja ya kuzimwa mitandao ya kijamii ikitolewa.

Kiongozi huyo sasa amechaguliwa katika uchaguzi uliowahusisha wananchi wa Taifa hilo, awali alichukua madaraka kupitia mapinduzi ya kijeshi miaka minne iliyopita.

Hata hivyo, kundi la kiraia linalopigania kurejeshwa kwa utawala wa kiraia lilikemea uchaguzi huo na kuutaja kuwa ni maigizo baada ya wagombea wake wakuu kuzuiwa kushiriki uchaguzi. Aidha, wagombea wa upinzani walisema uchaguzi huo uligubikwa na dosari mbalimbali.

Siku ya Jumatatu, Shirika la Kufuatilia Matumizi ya Mtandao, NetBlocks, liliripoti kuwa upatikanaji wa mitandao ya kijamii ya TikTok, YouTube na Facebook yote ilikuwa imefungwa wakati raia wa Guinea wakisubiri matokeo.

Hakuna taarifa iliyotolewa kuhusiana na kufungwa mitandao kuzuia ukosoaji wa matokeo ya uchaguzi.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa jana  Jumanne Desemba 30, 2025  yalionyesha Jenerali Doumbouya amepata asilimia 86.72 ya kura zote katika uliofanyika 28 Desemba, idadi inayompa ushindi na kuzidi kiwango kinachohitaji kufanyika kwa duru ya pili ya kura.

Ushindi huo unampa kiongozi huyo mamlaka ya kuongoza kwa kipindi cha miaka saba. Hata hivyo iwapo matokeo hayo yatapingwa, Mahakama Kuu ya nchi hiyo itatoa siku nane ili kuyathibitisha madai yatakayowasilishwa.