Kusimama kwa Mv Malagarasi kwachochea ujenzi wa daraja

Dar es Salaam. Serikali ipo katika mpango wa kujenga daraja litakalounganisha vijiji vya Ilagala na Kajeje mkoani Kigoma, kufuatia kusambaa kwa picha mjongeo kwenye mitandao ya kijamii zikionesha Kivuko cha Mv Malagarasi kimesitisha kutoa huduma kutokana na hitilafu ya kiufundi.

Kauli hiyo imetolewa baada ya Mwananchi kumtafuta Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya aelezee hatua zinazochukuliwa na Serikali kukabiliana na changamoto ya usafiri katika eneo hilo.

Akizungumza jana Jumanne, Desemba 30, 2025 Kasekenya  amesema maandalizi ya ujenzi wa daraja hilo yapo na usanifu tayari umekamilika.

“Hatua za kujenga daraja zimeshaanza kuchukuliwa, tayari usanifu wake umeshakamilika,” amesema Kasekenya.

Desemba 29, 2025 kwenye mitandao ya kijamii zilisambaa picha za mjongeo zikionesha kivuko hicho kikiwa kimesitisha huduma kutokana na hitilafu, huku kinamama wakionekana ndani ya mtumbwi wakimsaidia mjamzito kujifungua.

Katika picha hiyo, kijana aliyerekodi video ambaye hakutaja jina lake, alisikika akieleza kuwa kinamama hao walikuwa wakimsaidia mjamzito kujifungua ndani ya mtumbwi mdogo baada ya kivuko kushindwa kutoa huduma.

“Tumerudi tena, adhabu ya leo ni kuvuka kwa mtumbwi. Tumepata neema, mama amejifungulia kwenye mtumbwi. Hadi dakika hii tumepata katoto na kina mama wanaendelea kumsaidia,” alisikika akisema.

Kijana huyo ameomba Serikali kuchukua hatua za haraka, akieleza kuwa wakazi wa Kigoma Kusini wanakumbwa na mateso kutokana na changamoto ya kivuko.

“Tusaidieni tupate kivuko. Angalieni kina mama wajane na wajasiriamali wanavyomzalisha mwenzao ndani ya mtumbwi mdogo. Boti letu kubwa lina maboya zaidi ya 40 lakini si salama. Tunaomba juhudi za haraka zifanyike tupate daraja,” amesema.

Kufuatia hali hiyo, Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) kupitia Meneja wa Vivuko Kanda ya Ziwa na Magharibi, ulitoa taarifa kwa umma Desemba 29, 2025, ukikiri kusimama kufanya kazi kwa kivuko hicho.

“Ni kweli kivuko cha Mv Malagarasi kilisimama kutoa huduma kwa muda mfupi kutokana na hitilafu ya kiufundi. Hata hivyo, hitilafu hiyo ilirekebishwa kwa wakati na baada ya hapo kivuko kiliendelea kutoa huduma kama kawaida,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa sasa, Temesa imesema Kivuko cha Mv Malagarasi kinaendelea kutoa huduma bila matatizo yoyote katika eneo husika, huku uongozi wa wakala huo ukiomba radhi kwa abiria waliopata usumbufu na kuwakumbusha kufuata maelekezo ya mabaharia wakati wote wanapotumia kivuko.

Akizungumza na Mwananchi Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma amesema tayari usanifu wa kina na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa daraja litakalounganisha vijiji vya Ilagala na Kajeje umeshafanyika.

Amesema mradi huo umeingizwa kwenye mpango wa ufadhili wa Benki ya Dunia, lakini benki hiyo ilikataa kufadhili, hivyo Serikali inalazimika kutafuta chanzo kingine cha fedha.

“Tayari usanifu wa kina na upembuzi yakinifu umefanyika, lakini baada ya Benki ya Dunia kukataa kufadhili, sasa tunahitajika kutafuta fedha mbadala,” amesema Choma.

Amesema makadirio ya awali ya gharama za ujenzi wa daraja hilo ni Sh24 bilioni.

Hata hivyo, ahadi ya ujenzi wa daraja hilo si ya kwanza kutolewa, mwaka 2021, Serikali ilitangaza mpango wa kujenga daraja la kudumu litakalounganisha Ilagala na Kajeje kama mbadala wa Kivuko cha Mv Malagarasi, ili kuondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika maeneo hayo.

Akizungumza na wananchi wa maeneo hayo wilayani Uvinza, mkoani Kigoma wakati huo, Kasekenya alisema Serikali ilitambua adha wanayopata wananchi na kutenga Sh400 milioni katika mwaka wa fedha 2021/22 kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja hilo.

“Serikali imeona changamoto zenu, hivyo tayari imetenga Sh400 milioni kwa ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Baada ya kazi hii kukamilika, ujenzi utaanza mara moja,” alisema Kasekenya.