Dar es Salaam. Foleni ya magari iliibuka Barabara ya Mandela, jijini Dar es Salaam, kuanzia saa 12:00 asubuhi ya Desemba 31, 2025 na kusababisha usumbufu kwa wasafiri na watumiaji wengine wa barabara hiyo.
Kutokana na foleni hiyo, magari yalisogea kwa mwendo wa kusuasua, baadhi yakisimama kwa muda mrefu bila kusogea.
Chanzo cha foleni hiyo kimeelezwa kuwa ni wingi wa malori yaliyokuwa yakiingia bandari kavu zilizo kando mwa barabara hiyo.
Malori hayo yalikuwa yakijipanga upande mmoja wa barabara, jambo lililosababisha njia kuwa finyu hivyo kuathiri mtiririko wa magari mengine, hususani daladala na magari binafsi.
Malori yakiwa yamejipanga mstari katika barabara ya Mandela, Dar es Salaam kwa ajili ya kuingia katika moja ya bandari kavu iliyopo katika barabara hiyo.
Akizungumza na Mwananchi Desemba 31, 2025 dereva wa lori, Zabron Mwambe, amesema licha ya lawama kuelekezwa kwa madereva wa malori, wao pia ni waathirika wa mazingira magumu ya kazi.
“Tunafika hapa mapema, lakini hakuna utaratibu mzuri wa kuingia bandari kavu. Maegesho ni machache na wakati mwingine tunalazimika kusimama barabarani kusubiri ruhusa ya kuingia,” amesema.
Amesema iwapo kutakuwa na ratiba maalumu na maeneo rasmi ya malori kusubiria huduma tatizo la foleni litapungua kwa kiasi kikubwa.
Dereva wa daladala, Jamal Hussein, amesema foleni huathiri shughuli zao za kujipatia kipato.
“Safari ambayo kawaida inachukua dakika 30 leo imechukua zaidi ya saa mbili. Abiria wanachoka, wengine wanashuka njiani na wengine wanatukana wakidhani sisi ndio chanzo cha tatizo,” amesema.
Amesema foleni husababisha daladala kushindwa kufanya safari nyingi kama ilivyo kawaida, hali inayowaumiza wao na abiria kwa ujumla.
Askari wa Usalama Barabarani wakiongoza magari yaliyosongamana barabara ya Mandela katika makutano ya Reli na barabara hiyo eneo la Mwananchi
Kwa upande wa abiria, Aurelia Anthony, mkazi wa Tataba Chang’ombe, anasema foleni imemsababishia hasara kwa kuunga usafiri kutoka kwenye daladala na kupanda bodaboda kuelekea kazini.
“Nilitoka nyumbani mapema nikitegemea nitawahi, lakini nilipofika Tabata Relini imebidi nishuke na kupanda bodaboda baada ya kuona nachelewa kazini,” amesema.
Mkazi wa Chanika, Peter Ambrose, amesema alikuta foleni Buguruni ambayo haikuwa ikisogea kwa takribani saa moja, hivyo alilazimika kupanda bodaboda.
“Sikujua tatizo, nimefika Buguruni saa 1:30 asubuhi lakini nimefika ofisini Mwenge saa 3:30 baada ya kubadilisha usafiri wa awali ili kuwahi ofisini,” amesema.
Askari wa usalama barabarani walilazimika kuongoza magari ambayo yalisongamana pasipo kufuata utaratibu wa safari ili kuwezesha njia iliyojifunga kufunguka.
