Matumizi nishati safi ya kupikia yafungua fursa mpya za ajira

Mkuranga. Imebainika kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia yanaendelea kufungua fursa mbalimbali za ajira kwa Watanzania, hususan katika uzalishaji wa mkaa mbadala na utengenezaji wa mashine zinazotumika kuzalisha mkaa huo.

Mkurugenzi wa Nishati Safi ya Kupikia kutoka Wizara ya Nishati, Nolasco Mlay ametoa kauli hiyo leo Jumatano Desemba 31 wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi ya Wazalendo Movement wilayani Mkuranga, mkoani Pwani. Taasisi hiyo inajishughulisha na utengenezaji wa mashine za kuzalisha mkaa mbadala sambamba na mkaa wenyewe.

Mlay amesema taasisi nyingi zinazohudumia watu kuanzia 100 na kuendelea, zimeanza kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua ambayo imeongeza kwa kiasi kikubwa mahitaji ya mkaa mbadala na hivyo kuhitaji uzalishaji wa kasi zaidi ili kukidhi mahitaji.

“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuzalisha mkaa mbadala pamoja na mitambo ya kutengenezea mkaa huu. Hii ni fursa kubwa kwa Watanzania kwa kuwa mahitaji ni makubwa. Hata hivyo, ni muhimu kuhakikisha mkaa unaozalishwa ni wa ubora wa hali ya juu na unaodumu hata unaposafirishwa kwa umbali mrefu,” amesisitiza Mlay.

Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Deusdedit Malulu amesisitiza umuhimu wa kushirikisha Shirika la Viwango Tanzania (TBS) katika mchakato wa utengenezaji wa mkaa mbadala ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Aidha, amewahimiza wazalishaji kujisajili kwenye mfumo wa NEST utakaowasaidia kupata fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali na wadau wengine.

Ameongeza kuwa Rea ina mpango wa kutoa fursa kwa wananchi kushiriki katika utengenezaji wa mashine, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kuzalisha mkaa mbadala nchini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wazalendo Movement, Saidi Malema amesema taasisi hiyo katika kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, imeanzisha kikundi cha nishati safi kinachojihusisha na uzalishaji wa mkaa mbadala unaotengenezwa kutokana na magunzi ya mahindi na nyasi kavu.

Amesema taasisi hiyo hutengeneza mashine za kuzalisha mkaa mbadala zinazotumia umeme na zisizotumia ikilenga kukidhi mahitaji ya wananchi katika maeneo yenye umeme na yasiyo nao.

Mbali na hilo, amesema wameanzisha kikundi cha Nishati Safi Sanaa Group kinacholenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia sanaa ya maigizo na nyimbo.

“Taasisi ya Wazalendo Movement imefanikiwa kuuza mashine zake kwa wadau katika mikoa ya Tabora, Singida na Pwani,” amesema Malema.

Mlay ametembelea pia kampuni ya Matima Investment inayojihusisha na utengenezaji wa majiko ya kuchomea nyama yanayotumia gesi, ili kujionea namna yanavyosaidia kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.