Mauya, Mbeya City kuna jambo

WAKATI dirisha dogo la usajili likitarajiwa kufunguliwa kuanzia Januari Mosi, 2026, uongozi wa Mbeya City uko katika mazungumzo ya kuipata saini ya aliyekuwa kiungo wa Yanga, Zawadi Mauya, ikiwa ni pendekezo la Kocha Mkuu, Mecky Maxime.

Mauya ambaye kwa sasa yupo huru tangu alipoachana na KenGold Juni 30, 2025, baada ya timu hiyo kushuka daraja ikitokea Ligi Kuu Bara hadi Championship ni pendekezo la Maxime aliyefanya naye kazi wakiwa Singida Black Stars zamani Ihefu.

“Mazungumzo yanaendelea kati ya mchezaji na uongozi kwa sababu moja ya jambo kubwa linaloweza kurahisisha dili hilo ni ushawishi wa Maxime kwake, pia haitokuwa kazi ngumu kukubaliana suala nzima la maslahi binafsi,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema mchezaji huyo ameonyesha utayari wa kurudi tena katika soka la ushindani baada ya kukaa nje kwa muda wa miezi sita, hivyo jitihada za mazungumzo zinaendelea kati ya pande hizo mbili ili kupata saini yake kwa haraka.

Nyota huyo aliyezichezea Lipuli, Kagera Sugar, Yanga, Singida Black Stars na KenGold, inaelezwa tayari amekubaliana na kikosi hicho ili kwenda kukitumikia, ambapo uongozi wa Mbeya City umemwekea mkataba wa miezi sita hadi mwisho wa msimu.

Maxime aliyechukua mikoba ya Malale Hamsini aliyejiunga na KVZ ya visiwani Zanzibar, tayari ameanza mipango ya kukisuka upya kikosi hicho dirisha dogo, ambapo tayari ameinasa saini ya aliyekuwa kiungo wa Fountain Gate, Abdallah Kulandana.