BAADA ya jana Jumanne kuwa ni mapumziko, leo Jumatano michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inaendelea kwa kuchezwa mechi mbili za kundi A.
Uhondo wa mechi za leo unatokana na wapinzani wanaokwenda kukutana, huku kila mmoja akihitaji kushinda na kusaka rekodi.
Lakini katika mechi hizo, matokeo mabaya kwa upande wowote, lazima mtu alaumiwe na si vinginevyo kwani zinasakwa timu mbili za kufuzu nusu fainali. Kundi hili pekee linatoa timu mbili kutokana na kuwepo nne, lakini lile la B na C, zinapenya moja moja kwani yanaundwa na timu tatu kila moja.
Mabingwa watetezi, Mlandege, watacheza mechi ya pili dhidi ya URA kutoka Uganda ambayo kwao itakuwa mechi ya kwanza baada ya ratiba ya awali iliyoonyesha ilitakiwa kucheza Desemba 28, 2025 dhidi ya Azam, kusogezwa mbele hadi Januari 5, 2025.
Mechi hii itakayoanza saa 10:15 jioni, URA ambayo imewahi kubeba ubingwa wa michuano hiyo mwaka 2016, imepania kuanza vizuri, huku Mlandege ikipanga kurekebisha makosa yake.
Akizungumzia namna walivyojiandaa na mechi hiyo, Kocha wa URA, Ssemuyaba Bashir, amesema: “Hapa sio wageni, lakini safari hii tumekuja tumekuta mazingira tofauti.
“Malengo yetu ni kuona tunafanya vizuri katika mashindano haya na mechi hii ya kwanza tunaichukulia kwa uzito mkubwa.”
Naye Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri Ramadhan China, amesema: “Ni kweli mechi ya kwanza tumepoteza, ilikuwa sehem ya mchezo, tumejianda vizuri kupata pointi zetu tatu za kwanza kabla ya kufunga hesabu mwisho dhidi ya Azam.”
SINGIDA BLACK STARS VS AZAM FC
Saa 2:15 usiku, vita ya Ligi Kuu Bara inahamia Zanzibar, Singida Black Stars iliyoanza na ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya ufunguzi wa Kombe la Mapinduzi 2026, itacheza dhidi ya Azam ambayo inashuka dimbani kwa mara ya kwanza.
Timu hizi zinafahamiana vizuri sana, msimu huu zilikutana Desemba 3, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, mechi ikaisha 0-0. Kabla ya hapo, msimu wa 2024-2025 katika ligi, kila moja ilishinda kwake. Singida iliichapa Azam 1-0, nayo ikakandwa 2-1 pale Chamazi.
Kocha Msaidizi wa Singida Black Stars, David Ouma, amesema: “Jambo zuri wachezaji wetu wote wapo katika afya nzuri baada ya mechi ya kwanza.
“Kama mnavyofahamu mechi ya Singida na Azam huwa na ushindani mkubwa kimbinu, hivyo kesho (leo) tutarajie mchezo mzuri.”
Florent Ibenge, kocha mkuu wa Azam amesema: “Singida ni timu nzuri nimewaona wakicheza mechi ya kwanza, tumeiandaa timu kuona tunaanza vizuri kwani tunahitaji kuwa mabingwa.”
Wakati Ibenge akisema hayo, kiungo wa Azam, Himid Mao amesema: “Kila timu inapokwenda kwenye mashindano inataka kuwa bingwa, Azam tumechukua ubingwa huu mara nyingi kwa sababu tuliweka malengo na kuyapambania, hali hiyo pia tunayo msimu huu.”
