Tra Bi ajiandaa kusepa Singida Black Stars

BEKI wa kati wa raia wa Ivory Coast anayekipiga Singida Black Stars, Anthony Tra Bi Tra yupo katika hatua za mwisho za kuachana na kikosi hicho dirisha hili dogo la usajili, huku mkataba wake ukibaki miezi sita.

Nyota huyo aliyejiunga na Singida Agosti 7, 2024, akitokea Asec Mimosas ya Ivory Coast, alisaini mkataba wa miaka miwili unaofikia tamati Juni 30, 2026, japo mambo yamebadilika na sasa anakaribia kusepa.

Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo zinadai nyota huyo ameamua kusitisha mkataba wa miezi sita uliobaki ambapo kwa sasa kilichobakia ni makubaliano ya pande mbili kisha atafute changamoto mpya.

“Ni beki mzuri sana lakini tunahitaji kufanya maboresho katika eneo hilo kwa kuongeza nyota mwingine bora zaidi yake kwenye dirisha hili dogo. Tunakamilisha tu baadhi ya taratibu muhimu ili kuachana naye kwa wema,” kilisema chanzo.

Mwanaspoti linatambua Tra Bi Tra aliyeichezea pia FC Foix ya Ufaransa amekosa imani na benchi la ufundi chini ya Kocha Miguel Gamondi, jambo linalorahishisha pande hizo mbili kuachana.

Licha ya Singida kupiga hesabu za kusajili nyota mpya eneo analocheza, lakini tayari imenasa saini ya mabeki wawili wa kati ambao ni Abdallah Kheri ‘Sebo’ aliyetokea Pamba Jiji aliyoichezea kwa mkopo akitokea Azam FC na Abdulmalik Zakaria aliyekuwa Mashujaa. 

Timu hiyo ilikuwa inahitaji mabeki wengine wa kati baada ya mechi za hivi karibuni kuanzia Kombe la Kagame, Ligi Kuu Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kumtumia Mnigeria Morice Chukwu ambaye kiasili ni kiungo mkabaji.