UCHAMBUZI WA MALOTO: ‘Utajiri’ wa watoto wa viongozi hausimuliwi kwa bahati mbaya

Moja ya matukio ya Oktoba 29, 2025, ni video iliyorekodiwa Arusha. Vijana walivamia jengo ambalo inaonekana ujenzi wake upo hatua za mwishoni. Baada ya uvamizi huo, vijana walichoma moto na kuteketeza gari aina ya Toyota Alphard.

Katika video hiyo vijana wanaonekana wakifurahia na kutamba kwamba jengo hilo walilovamia mmiliki ni Abdul. Kishujaa kabisa wale vijana wanasema ni gari mpya, “namba E”, ndilo walilolichoma. Abdul aliyemaanishwa hapo ni Abdul-Halim Hafidh Ameir, mtoto wa Rais Samia Suluhu Hassan.

 Nikajiuliza kama video hiyo itamfikia Abdul. Nikawaza endapo hata hilo jingo kama analijua. Inatikisa mengi. Inawakilisha jinsi chuki ilivyotengenezwa mitaani. Inatafsiri macho na nyoyo za umma. Inatahadharisha kuhusu mwendo wa nchi na masahihisho yanayopaswa kufanyika.

Madhara ya Oktoba 29 ni makubwa. Hata hivyo, pengine ni madogo dhidi ya makubwa ambayo yanaweza kujitokeza baadaye. Inawezekana yaliyotokea ni wito wa uamsho kutoka kwa Mungu. Wito wa masahihisho kuhusu jinsi tunavyotazamana, tunavyotendeana na tunavyotumia ndimi zetu dhidi ya wenzetu.

Turejee kisa cha vijana wa Arusha na Abdul. Kinanikumbusha tukio ambalo nilisimuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete. Ni tukio ambalo lilitokea wakati Ridhiwani akiwa siyo waziri wala naibu waziri. Alikuwa mbunge wa benchi la nyuma.

Kwa mujibu wa Ridhiwani, tukio hilo lilimtokea akiwa safarini Mkoa wa Kilimanjaro. Alisafiri kutokea Dar es Salaam kwa ndege, kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia). Alipofika Kia, alikodi taksi iliyompeleka Moshi. Dereva taksi hakuwa akimfahamu Ridhiwani kwa sura na umbo, ila jina alishalisikia sana.

Katikati ya Kia na Moshi, Ridhiwani aliona mahali ujenzi unaendelea. Ridhiwani akamdadisi dereva kuhusu ujenzi uliokuwa ukiendelea. Ni hoteli, kituo cha manunuzi au uwekezaji gani mwingine? Yule dereva taksi badala ya kujibu swali aliloulizwa, alikwenda kugusa mshipa.

“Najua basi kinachoendelea? Anayejua ni Ridhiwani Kikwete, ambaye ndiye mmiliki. Sisi yetu macho, tunasubiri ujenzi ukamilike ndiyo hasa tujue. Kwa sasa tunashangaa tu,” alisema yule dereva taksi. Ridhiwani alishangaa kuona anaambiwa yeye ndiye mmiliki wa huo uwekezaji.

Pamoja na mshangao wake. Ridhiwani alimudu kutulia, akaendelea kumchokonoa yule dereva.“Kumbe huo ujenzi ni wa Ridhiwani? Inaonekana ana pesa sana,” Ridhiwani aliuliza.

“Aah, hapo basi kuna kitu? Dar es Salaam ndiyo kuna balaa. Kule amenunua hadi mitaa unaambiwa. Ana vituo vya mafuta, malori, mahoteli, ni tajiri sana,” alijibu yule dereva taksi. Ridhiwani akauliza: “Huyo Ridhiwani ni nani hasa?”

Bila kuchelewa, dereva taksi alijibu: “Ni mtoto wa mkubwa nchi huyo. Ni mtoto wa Rais Jakaya Kikwete.”

Ridhiwani akamuuliza: “Huyo Ridhiwani ukikutana naye unaweza kumtambua?” Dereva taksi akasema kuwa hamjui kwa macho ila akadai kwamba kwa jina, kila Mtanzania alikuwa akimfahamu Ridhiwani Kikwete.

Kumbe yule dereva taksi kichwani alikuwa na umbile la Ridhiwani alilolichora kwenye fikra. Alidhani Ridhiwani ana umbo kubwa. Miraba minne hivi. Ridhiwani alipojitambulisha kama tajiri anayemsema anamiliki hadi mitaa Dar es Salaam ndiyo yeye, dereva taksi akakataa.

Ulifuata wasaa wa Ridhiwani kumwelewesha dereva taksi kwamba yeye ndiye Ridhiwani na mali anazotajwa kuzimiliki anasingiziwa, ikiwemo ujenzi uliochokoza mada. Akamwambia: “Ona sasa, nakuuliza kinachojengwa pale, unasema anajua Ridhiwani kwa sababu ndiye mmiliki. Wakati Ridhiwani ni mimi na sijui chochote kuhusu ujenzi huo wala mmiliki wake.”

Usambazaji wa taarifa za umiliki wa mali, hufanywa kwa njia inayojenga chuki ya kijamii. Haisemwi kishujaa, bali kwa namna ambayo huchokonoa hasira za watu, ionekane kuna viongozi, watoto wao, au familia zao, hutajirika kupitia nafasi zao.

Vituo vya mafuta na gesi vya Lake Oil, ambavyo vinamilikiwa na kampuni ya Lake Oil Limited, navyo vikakumbana na shambulio Oktoba 29. Vijana walivichoma moto, wakapora mitungi ya gesi na mali nyingine. Walisema wanafanya hivyo ili kumkomoa Ridhiwani Kikwete. Walisema mmiliki wa Lake Oil ni Ridhiwani.

Mmiliki wa kampuni ya Lake Oil Limited, kwa mujibu wa nyaraka za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), ni mfanyabiashara Ally Edha Awadh. Zaidi, ukipitia wasifu wa Lake Oil Limited, kama ulivyochapishwa kwenye tovuti yao rasmi, inaonesha kuwa Awadh alianzisha kampuni hiyo mwaka 2006, akiwa na umri wa miaka 27.

Oktoba 29, watu waliyafuaya mabasi ya Esther Luxury Coach kwenye yadi na kuyachoma moto. Wachomaji walisema mabasi ya Esther yanamilikiwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.

Kampuni ya mabasi ya Esther, inamilikiwa na wazawa Joseph Didas Ngeleuya na Neema Peter Thomas, kama inavyoainishwa kwenye nyaraka za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra).

Inakumbusha, mwaka 2007, nilitumiwa orodha ya majina ya watoto wa viongozi waliodaiwa kufanya kazi Benki Kuu Tanzania (BOT). Orodha nilitumiwa mbunge wa chama cha upinzani wakati huo. Orodha hiyo iliandikwa kwa namna ambayo mtu ungesoma, ungepata tafsiri ya haraka kuwa “vigogo wanaajiri watoto wao BOT”.

Nilimuuliza yule mbunge uthibitisho wake kama kweli orodha ile, wote walikuwa wakifanya kazi BOT, na ukweli kwamba walikuwa watoto wa viongozi waliotajwa. Yule mbunge aliniambia: “Nimekuletea wewe mwandishi wa habari, fanyia kazi.”

Ni kweli niliifanyia kazi, lakini sikuweza kuiandikia habari, maana haikuwa na ukweli. Mmoja wa waliotajwa kufanya kazi BOT ni rafiki yangu. Ni kweli yeye ni mtoto wa veterani wa kisiasa Tanzania. Baada ya kumaliza masomo yake Marekani, alirejea Tanzania na kuajiriwa kwenye benki za kimataifa, kabla ya kuingia kwenye siasa. Hakuwahi kuajiriwa BOT.

Tunapoelekea kuufunga mwaka 2025 na kuuanza 2026, hatutasahau maumivu na aibu ya Oktoba 29, 2025. Wito ni kutibu majeraha, ukweli taifa linahitaji uponyaji wa ubongo. Chuki ikiondoka, majeraha yatafutika yenyewe, na tabasamu la kitaifa litachomoza.

Muhimu ni kwamba utajiri wa Abdul, Ridhiwani, Mwigulu na wengine wenye nasaba za kisiasa, hausimuliwi kwa bahati mbaya. Ni makusudi ili Watanzania waamini, wajenge chuki. Tuchukiane. Mwisho wa chuki ni taifa kusambaratika.