Tunapofikia ukingoni mwa mwaka 2025, leo Jumatano ikiwa ni siku yake ya mwisho, Watanzania tunaingia katika mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya wa 2026.
Ni wakati wa kufanya tathmini ya safari tuliyotoka, kujifunza kutokana na tuliyokutana nayo na kujipanga kwa mustakabali ulio mbele yetu.
Uchambuzi wangu unaangazia kutafakari yaliyopita kwa jicho la busara na kuyaangalia yajayo kwa matumaini mapya.
Mwaka 2025 ulikuwa na sura mbili: mafanikio na changamoto. Hakika kulikuwa na mambo makubwa na mazuri, lakini tukio kubwa zaidi lililoutia alama mwaka huu ni Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Uchaguzi huu Mkuu uliofanyika Jumatano ya Oktoba 29 ambao ulipaswa kuwa kilele cha demokrasia yetu, uliacha maswali na majeraha kwa wengi, kutokana na matukio yasiyopendeza yaliyotokea siku hiyo ya uchaguzi.
Matukio hayo yameliacha doa katika taswira ya Tanzania kama taifa linalojivunia amani, utulivu na mshikamano.
Katika muktadha huo, busara ya Kiswahili hutufundisha kuwa; “yaliyopita si ndwele, tugange yaliyopo na yajayo.”
Methali zetu zinatukumbusha pia kuwa haraka haina baraka, mwenye pupa hadiriki kula tamu, na mkamia maji hayanywi.
Kwa mtazamo huo, yaliyotokea Oktoba 29 yanaweza kuelezwa kama matokeo ya uamuzi wa pupa na kukosa subira ya kujenga maridhiano ya kitaifa kabla ya uchaguzi.
Badala ya kuwa ‘mwenda pole’, tulikimbia tukajikwaa na kuanguka. Cha msingi sasa si kulaumu bali kujifunza, kurekebisha tulipokosea na kuhakikisha hatujirudii.
Katika kipindi chote cha mwaka 2025, mjadala mkubwa ulikuwa juu ya uchaguzi huru na wa haki. Wadau mbalimbali walitoa mapendekezo ya nini kifanyike ili kuimarisha uaminifu wa mchakato wa uchaguzi.
Pendekezo lililopewa uzito zaidi na wengi lilikuwa kufanyika kwa mabadiliko madogo ya Katiba pamoja na marekebisho ya sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi, ili kusawazisha uwanja wa kisiasa.
Hata hivyo, mapendekezo hayo hayakuzingatiwa ipasavyo na taifa likaingia tena kwenye uchaguzi bila kuyafanya marekebisho ya kikatiba yaliyopendekezwa, jambo lililozaa matokeo tata.
lawama nyingi zimeelekezwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan. Lakini kwa uhalisia, Rais alichukua hatua kadhaa ikiwamo kuunda kikosi kazi, kukusanya maoni ya wadau na kujadili mapendekezo, mojawapo likiwa ni mabadiliko madogo ya Katiba.
Pendekezo hilo halikupata ridhaa. Badala yake, Serikali ilifanya marekebisho ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa, ikaivunja Tume ya zamani ya Uchaguzi (NEC) na kuunda Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
Hata hivyo, hapa ndipo changamoto ya kisheria ilipojitokeza. NEC ni chombo kilichoanzishwa na Katiba na kikatiba, chombo kama hicho hakiwezi kuondolewa kwa sheria ya kawaida bila kwanza kufanya mabadiliko ya Katiba.
Kwa hali ilivyokuwa, INEC iliundwa kwa msingi wa sheria bila kuingizwa kwanza ndani ya Katiba, hali iliyozua mkanganyiko wa kisheria na kikatiba.
Zaidi ya hayo, viongozi walioteuliwa kuongoza INEC walikuwa ni wale wale wa NEC ya awali, jambo lililoacha maswali kuhusu uhalisia wa mabadiliko yaliyokusudiwa.
Kwa mtazamo mpana, muda ulikuwepo wa kutosha kufanya mabadiliko madogo ya Katiba.
Sababu kuu ya kutofanyika kwake haikujulikana wazi, isipokuwa hisia za kiburi cha madaraka na hofu ya kuonekana kukubali shinikizo la kisiasa. Lakini ukweli ni kwamba, kiburi si maungwana. Kutofanya marekebisho ya Katiba ndiko kulikokuwa chanzo cha matatizo ya Oktoba 29; yaliyotokea ni matokeo, si mzizi wa tatizo.
Funzo kubwa kwa Serikali yetu ni kujenga utamaduni wa kusikiliza wananchi. Tanzania ni mali ya Watanzania; mamlaka kuu yanatokana na wananchi.
Rais, Serikali, Bunge na Mahakama wote ni watumishi wa wananchi. Pale wananchi wanapodai mabadiliko, wanastahili kusikilizwa au kupewa maelezo ya wazi endapo madai hayo hayawezi kutekelezwa.
Sasa maji ya Oktoba 29 yameshamwagika; hayazoleki. Tukiwa mwishoni mwa mwaka, ni vyema kuyaacha yaliyopita, tugange yaliyopo na yajayo.
Kwa kuwa ipo tume ya uchunguzi wa yaliyotokea, ni jukumu la wananchi na wadau kuwasilisha maoni yao ili ukweli uweze kujulikana na suala hilo kufungwa kwa haki.
Mbele yetu ajenda kubwa ni katiba mpya. Baada ya CCM kushinda uchaguzi kwa kishindo na kuweka hoja hiyo ya katiba mpya katika Ilani yake ya 2025/2030, pamoja na ahadi ya Rais Samia ya kuanza mchakato huo ndani ya siku 100 za kwanza za Bunge jipya, matumaini mapya yamechomoza.
Katiba mpya inaweza kuwa suluhisho la kudumu, ikikata mzizi wa migogoro na fitna za kisiasa.
Tunapoingia mwaka 2026, tunapaswa kuingia kama taifa jipya lenye dhamira mpya ya kuwa Tanzania mpya, mambo mapya.
Heri ya Mwaka Mpya. Mungu Ibariki Tanzania.
