Wakitakacho vijana kisiasa, kiuchumi ni hiki

Dar es Salaam. Katika kipindi ambacho Serikali imeweka juhudi za makusudi kushughulikia kero na changamoto zinazowakabili vijana nchini, makundi mbalimbali ya vijana, wakiwamo wanaojihusisha na siasa na shughuli za kiuchumi, yameeleza changamoto na matarajio yao kuelekea mwaka mpya wa 2026.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, vijana hao wameibua hoja mbalimbali wanazodai zimekuwa zikiwarudisha nyuma kimaendeleo, huku wakipongeza hatua ya Serikali kuanzisha wizara mahsusi ya vijana, wakionesha imani kuwa itakuwa chombo muhimu cha kusimamia na kutetea maslahi yao.

Akizungumza kuhusu nafasi ya vijana katika siasa na uchumi, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT-Wazalendo), Abdul Nondo amesema vijana ndio waathirika wakubwa wa changamoto za ajira, usalama na ukosefu wa uwakilishi wa kutosha katika vyombo vya uamuzi.

Amesema changamoto hizo zinaonekana pia katika mfumo wa elimu usioendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira, ukosefu wa mitaji kwa vijana wanaotaka kujiajiri, pamoja na ugumu wa mazingira ya kiuchumi hali ambayo amesema imewaathiri zaidi vijana.

“Kwa yaliyotokea mwaka 2025 wakati wa Uchaguzi Mkuu, mimi binafsi na vijana wengi hatutamani kuyaona yakijirudia. Rais ameunda tume ya uchunguzi na pia kuanzisha Wizara ya Vijana. Hii ni fursa kwa Watanzania wote kuwa na dhamira ya dhati ya kushughulikia sababu zilizosababisha hali hiyo, ili kujenga mshikamano wa kitaifa,” amesema Nondo.

Hata hivyo, Nondo ameonesha hofu kuwa dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan inaweza isilete matokeo chanya endapo wasaidizi wake hawatakuwa na dhamira ya kweli ya kuleta mabadiliko.

“Kama ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) hakutakuwa na watu wasiounga mkono mabadiliko yanayopendekezwa, juhudi za Rais Samia zinaweza kugonga mwamba,” amesema Nondo.

Amesema upande wa siasa, changamoto kubwa kwa vijana bado ni Katiba ya mwaka 1977, ambayo anadai imeweka misingi ya chaguzi zisizo huru na za haki, hali inayosababisha vijana wengi kukosa imani na mchakato wa uchaguzi.

“Vijana wengi hawaaminiwi licha ya wachache kupata nafasi, ndiyo maana wamepoteza imani ya kugombea nafasi za uongozi na wakashinda bila upendeleo.”

“Leo kijana akigombea anakumbana na ubabe wa askari, vurugu na kura feki kukamatwa, mizengwe ya kukatwa na mengine mengi, hali hii inayovunja ari ya vijana kushiriki siasa, Jeshi la polisi nalo linapaswa lijitenge na siasa, mifumo ya uchaguzi iwe huru ili ijenge imani kwa vijana,” amesema Nondo.

Amesema anapongeza tamko la Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene la Serikali kutaka kufanya mabadiliko ndani ya Jeshi la Polisi alilolitoa hivi karibuni.

Nondo anasema Jeshi la Polisi linatakiwa liwe katika muundo aliousema Simbachawene wa kutoa huduma kwa watu badala ya kuwa adui wa watu.

“Vijana tunataka mabadiliko hayo yawe ya kweli, hilo ni jambo zuri linaloweza kuleta matokeo mazuri,” amesisitiza kiongozi huyo wa vijana.

Amesema mabadiliko yote hayo yanatakiwa yasindikizwe na mabadiliko ya katiba, akikumbushia ahadi ya Rais Samia aliyosema ndani ya siku 100 za uongozi wake, ataanza mchakato wa katiba.

Kuhusu uchumi kwa vijana, amesema kupata Wizara ya Vijana ni jambo jema lililofanywa na Serikali, kwa sababu walikuwa hawana nafasi ya kusikilizwa, akiweka mkazo kuwa wizara hiyo itengeneze utaratibu bora wa kuwafikia vijana mpaka ngazi ya vijiji na vitongoji.

“Wizara iweke mkakati wa kujua vijana wa Kigoma shughuli yao ni nini, vijana Masasi, Bukoba na kila mahali ijue wanafanya nini na wanahitaji wasaidiwe kitu gani, bila upembuzi huo, wizara inaweza isiwasaidie vyema vijana.

“Zaidi, nitoe wito kwa vijana tuwe tunajitokeza kushiriki kwenye mijadala ya kisiasa, kijamii ili tutoe maoni watu na viongozi hususan wa Serikali watusikie kusudi wajue tunataka nini na sisi tujue mwelekeo wa sera za mambo mbalimbali yanayohusu maisha yetu, hii itatusaidia sana kutambua tunapaswa kufanya nini ili kufikia malengo yetu,” amesisitiza Nondo.

Hata hivyo, mtazamo huo unaungwa mkono na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama cha Wananchi (JUVICUF), Abeid Rutozi, ambaye amesema licha ya vyama vingi vya siasa kuwa na idara na jumuiya za vijana, bado vipo vikwazo vya kimfumo vinavyowanyima vijana fursa za kujiendeleza na kutimiza ndoto zao kwa urahisi.

Rutozi amesema tatizo la vijana kutokusikika kisiasa lina pande mbili; vijana wenyewe pamoja na mifumo ya kisiasa iliyopo nchini.

Ameeleza kuwa kwa nje Tanzania inaonekana kuwa na vyama vingi vya siasa, lakini hali halisi uwanjani inaonesha kuwa ni chama kimoja pekee ndicho chenye fursa pana za kufanya siasa.

“Vyama vya siasa, ikiwemo chama chetu cha CUF, vina jumuiya za vijana, lakini changamoto ya vijana kutokusikika ina pande mbili; vijana wenyewe na mifumo ya siasa iliyopo. Ukiangalia kwa nje utaona vyama vingi, lakini ukiingia kwenye uwanja wa siasa unakuta ni chama kimoja ndicho kina fursa kubwa za kisiasa,” amesema Rutozi.

Akizungumzia hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuwajumuisha vijana katika fursa za kisiasa na kiuchumi, Rutozi amesema Wizara ya Maendeleo ya Vijana inapaswa kushughulikia ukiritimba uliozoeleka katika fursa zinazowahusu vijana.

Amesema vijana wengi wana hofu ya kutumia fursa zilizopo wakihofia kusumbuliwa na taasisi za serikali, ikiwemo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

“Ili kuwafungulia vijana fursa za kisiasa na kiuchumi, wizara inapaswa kuondoa hofu iliyopo kuhusu uhuru wao wa kisiasa na kiuchumi. Leo ukitoa maoni, utasikia vijana wakisema ‘wewe huogopi?’, jambo linaloonesha kiwango cha hofu kilichopo. Vijana wanaamini kuwa kama huonyeshi ushirikiano na Chama cha Mapinduzi au huipongezi Serikali, basi upo hatarini. Hata ukitaka kujiajiri, unaweza kubanwa,” amesema.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana wa Chama cha NCCR Mageuzi (Vijana wa Mageuzi), Nicholaus Jovin amesema ongezeko la watu na idadi kubwa ya vijana ni tishio kwa mustakabali wa vijana kiuchumi na kisiasa, akisisitiza haja ya Serikali kuongeza uwekezaji katika elimu ya ujuzi ili kuwapatia vijana maarifa ya kujiajiri.

Amesema takwimu zinaonesha kuwa ifikapo mwaka 2050 Tanzania itakuwa na zaidi ya watu milioni 120 na wengi wao watakuwa vijana. Kwa kuzingatia ukweli kuwa Serikali haiwezi kuwaajiri vijana wote, amesema ni muhimu kuwekeza zaidi katika elimu ya ujuzi.

“Sisi vijana wa leo tunaondoka kwenye hatua ya ujana, wanakuja wadogo zetu. Takwimu zinaonesha ifikapo mwaka 2050 Tanzania itakuwa na watu milioni 120, wengi wao wakiwa vijana. Serikali haiwezi kuwaajiri vijana wote, hivyo ni lazima iwekeze kwenye elimu ya ujuzi ili vijana waweze kujiajiri,” amesema Jovin.

Ameongeza kuwa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi (VETA) vikitumika ipasavyo kuwapatia vijana ujuzi wa ufundi na teknolojia, vitawawezesha kujiajiri, kuzalisha na kuchangia uchumi, badala ya kuwaacha mitaani bila ajira na bila mwelekeo, hali inayosababisha chuki dhidi ya Serikali na shinikizo la kudai ajira.

Jovin amesisitiza vijana wengi wamekosa mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa kutokana na kukosa ujuzi na ajira, akisema endapo watapatiwa fursa za mafunzo na mazingira rafiki ya kujiajiri, watanufaika na kuchangia maendeleo ya nchi.

Kuhusu mustakabali wa vijana katika siasa, Jovin ametilia shaka mifumo ya kisiasa iliyopo akisema inawabana vijana wengi kushiriki kikamilifu na kupata nafasi za uwakilishi.

Ameeleza kuwa ni vijana wachache wenye watu wa kuwashika mkono ndio wanaofanikiwa ndani ya vyama vya siasa.

“Mfumo wa siasa zetu hautoi nafasi sawa kwa kila mtu. Kuna mlolongo wa watu wakubwa wanaopitisha watu wanaowataka. Vijana wengi ambao hawapo kwenye mifumo hiyo hawaonekani na hawapati fursa kwa urahisi, bila kujali uwezo wao,” amesema.

Amesema endapo Katiba itabadilishwa na kuruhusu wagombea binafsi, itasaidia vijana wengi wanaokwama ndani ya vyama kugombea nafasi mbalimbali na kupata fursa ya kujitokeza mbele ya jamii.

“Mifumo ya siasa kama huna mtu wa kukutetea, hata uwe na uwezo kiasi gani, wakiamua kukudhibiti hupati nafasi kabisa. Mimi ninaona kama Katiba ikibadilishwa na kutoa nafasi ya mgombea binafsi, vijana wengi watakimbilia huko baada ya kuwekewa vikwazo ndani ya vyama,” ameongeza.

Kwa upande wa vijana waliojiajiri katika sekta ya usafirishaji wa bodaboda na bajaji, wamesema kundi hilo linajumuisha vijana wa ngazi mbalimbali za elimu, kuanzia darasa la saba hadi wahitimu wa vyuo vikuu, kila mmoja akiwa na ndoto zake.

Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dar es Salaam na Taifa, Said Kagomba amesema vijana wengi wameingia kwenye sekta hiyo kwa sababu ya urahisi wa kujiajiri huku wakisubiri fursa za taaluma zao.

“Huku kwetu kuna vijana wa makundi yote; wapo wa darasa la saba, waliomaliza sekondari na hata wahitimu wa vyuo vikuu. Wote wameingia hapa kwa sababu ya urahisi wa kujiajiri huku wakisubiri fursa nyingine,” amesema Kagomba.

Ameitaka Wizara ya Maendeleo ya Vijana kulitambua kundi hilo, akidai limekuwa likiumizwa na mikopo kandamizi ya kumiliki pikipiki na bajaji, huku mikopo ya vijana kutoka serikalini ikiwa na masharti magumu na mifumo mirefu ya kuifikia.

“Nashauri wizara ya vijana itufikie na sisi tuzungumze. Kilio kikubwa cha vijana ni kukosa fursa za ajira. Vijana wengi wanamiliki bajaji kwa mikataba kandamizi; mfano bajaji inaweza kuchukuliwa kwa mkataba wa zaidi ya Sh milioni 10, ilhali thamani yake ni hadi Sh6 milioni,” amesema.

Ameongeza kuwa vijana wanaingia kwenye mikataba hiyo kutokana na ugumu wa kupata ajira na vikwazo katika kupata mikopo, akisisitiza kuwa wizara ina wajibu wa kuhakikisha fursa za vijana, ikiwemo mikopo, zinawafikia kwa wakati.

“Bodaboda na bajaji tunalipa kodi na kuchangia pato la Taifa, lakini hakuna mpango kazi mzuri wa kutuwezesha. Wizara ya vijana inapaswa kuhakikisha fursa na fedha za mikopo zinawafikia vijana kwa wakati,” amesema.

Kagomba amesema endapo vijana watapatiwa mikopo yenye masharti nafuu, wataweza kununua vyombo vyao wenyewe na kuinuka kiuchumi badala ya kuendelea kubebeshwa mikopo kandamizi.

“Sisi lengo letu ni kuona kijana anakua kiuchumi; atoke kwenye pikipiki ya matairi mawili, anunue bajaji, na hatimaye amiliki gari. Hilo halitawezekana bila wizara kuwawezesha vijana,” amesema.

Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Dar es Salaam, Namoto Yusuph amesema vijana waliamua kujitafutia kipato kupitia biashara hizo lakini wanakabiliwa na changamoto ya kukosa maeneo rafiki ya biashara na mikopo yenye masharti nafuu.

Amesema kundi hilo linakumbwa na mikopo yenye masharti magumu na riba kubwa huku likifanya biashara katika mazingira yasiyo rafiki.

“Kijana yeyote anayefanya biashara ya machinga akiguswa, atakuambia changamoto ni maeneo ya kufanyia biashara na ukosefu wa mikopo rafiki. Hata mikopo ya halmashauri kwa vijana na wanawake, vijana wengi huizungumza tu; wakifuatilia taratibu zinakuwa nyingi hadi wanakata tamaa,” amesema.

Namoto amesema licha ya juhudi mbalimbali za Serikali, vijana bado wanahitaji kuwezewa mazingira rafiki ya biashara ili kuvutia wengi kujiajiri na kupunguza umasikini miongoni mwao.