Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiukaribisha mwaka mpya wa 2026, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wameeleza mambo muhimu yanayopaswa kuzingatiwa ili kuimarisha amani, umoja, utulivu na maendeleo ya nchi.
Viongozi hao wamesisitiza kuwa 2026 unapaswa kuwa mwaka wa mabadiliko chanya utakaojikita katika haki, maridhiano na uwajibikaji, pamoja na kuweka juhudi za makusudi za kupunguza gharama za maisha na kuimarisha fursa za ajira kwa vijana.
Aidha, wametaja umuhimu wa kuanza kuhuisha mchakato wa Katiba mpya kama nguzo muhimu ya kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria nchini.
Pamoja na kutoa mwelekeo wa matarajio kwa mwaka unaoanza, viongozi hao pia wamewashauri Watanzania kutumia kipindi cha mwaka mpya kutafakari matukio yaliyolikumba Taifa mwaka 2025, yakiwemo mauaji ya wananchi yaliyotokea Oktoba 29, pamoja na matukio ya ‘utekaji’ na watu kupotea, wakisisitiza haja ya kuyakabili kwa misingi ya haki na uwazi.
Kauli hizo zimetolewa leo Jumatano, Desemba 31, 2025, katika mazungumzo yao na Mwananchi kwa nyakati tofauti, walipokuwa wakitoa salamu na maoni yao kuhusu matarajio ya mwaka 2026 unaoanza kesho Alhamisi.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) Bara, Benson Kigaila, amesema Watanzania wanahitaji mabadiliko katika maeneo mbalimbali, ikiwamo kwenye mifumo itakayowezesha upatikanaji wa Katiba mpya.
“Licha ya 2026 kuwa mwaka unaoanza na maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika 2030, tunategemea utaanza na mabadiliko, yakiwemo ya kijamii, Katiba, kisheria na kimfumo,” amesema Kigaila.
Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Chama cha Wananchi (CUF), Mohamed Ngulangwa, amesema Watanzania wanapoanza mwaka 2026 ni wajibu wa Taifa kutafakari kwa kina yaliyotokea 2025, kwa kuwa yameacha funzo.
“Mwaka 2025 umeacha funzo zito kwamba maendeleo ya kweli hayawezi kusimama bila haki, uwazi, ushiriki wa wananchi na uongozi unaosikiliza sauti za watu wake. Amani ya kudumu haiwezi kujengwa kwa hofu, bali kwa haki na maridhiano ya kweli,” amesema Ngulangwa.
Amesema 2026 unapaswa kuwa mwaka wa kurekebisha mwelekeo wa Taifa. “Ni lazima kuanza kwa mageuzi ya dhati ya kisiasa na kikatiba, yatakayorejesha imani ya wananchi katika demokrasia, kuheshimu uhuru wa vyama vya siasa na kulinda haki za msingi za raia bila ubaguzi,” amesema.
Aidha, Ngulangwa amesema 2026 lazima uwe wa uchumi unaomlenga mwananchi wa kawaida, sambamba na kupunguza gharama za maisha, kuimarisha ajira kwa vijana na kulinda wafanyabiashara wadogo na wa kati.
“Ukuaji wa uchumi unaoonekana kwenye takwimu tunataka uonekane pia mezani kwa mwananchi. Pia, kipaumbele kiwekwe kwenye upatikanaji wa umeme wa uhakika, maji safi, afya bora na elimu yenye ubora. Zaidi ya yote, 2026 uwe mwaka wa kusikilizana kama Taifa,” amesema kiongozi huyo.
Amesema mazungumzo ya kitaifa, uwajibikaji wa viongozi na kuheshimu Katiba viwe msingi wa safari mpya ya kujenga Tanzania yenye haki, fursa na usawa kwa wote.
Ngulangwa amesema kutokana na yale yaliyojitokeza 2025, hivyo mwaka 2026 ukawe wa kulitibu Taifa kwa kujifunza na kuhakikisha kunakuwa na mwafaka wa kweli.
Akizungumzia hilo, Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amesema chama hicho kingependa 2026 ukawe mwaka wa matumaini mapya katika kujenga Taifa lenye demokrasia ya kweli na kufanikisha maendeleo kwa Watanzania.
“Tunawatakia kheri ya mwaka mpya 2026 Watanzania wote, tunaupokea mwaka huu tukikumbuka matukio yaliyotokea mwaka 2025, ikiwemo mauaji ya Oktoba 29 na utekaji. Tunatoa pole kwa familia zote zilizoathirika na tunasisitiza kuwa haki ya kuishi ni ya msingi,” amesema Semu na kuongeza;
“Tunaitaka Serikali kutekeleza wajibu wake wa kikatiba kwa uwajibikaji, uwazi na utawala wa sheria. Mwaka 2026 uwe wa haki, amani na maendeleo ya watu na mshikamano wa kitaifa.”
Itakumbukwa Oktoba 29, 2025, Tanzania ilifanya uchaguzi mkuu, lakini kulitokea vurugu zilizosababisha uharibifu wa miundombinu, mali za umma na watu binafsi, vifo na majeruhi katika majiji na miji ya mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Geita, Songwe, Dodoma na Arusha.
Hali hiyo ilisababisha kadhia kwa wananchi waliolazimika kubadilisha mtindo wa maisha, kutokana na polisi kuweka zuio la kutotembea barabarani baada ya saa 12 jioni.
Novemba 18, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kuunda tume ya kuchunguza matukio hayo chini ya Jaji Othman Chande na imeshaanza kufanya kazi.
Mwenyekiti wa Ada Tadea, Jumaa Ali Khatibu, amesema 2026 ukawe mwaka wa ushirikiano na kuijenga Tanzania na kudumisha amani na utulivu uliokuwapo tangu enzi na enzi.
“Tujenge Taifa letu, tudumishe uzalendo na tudumishe amani na utulivu kwa kuwataka vijana kutokubali kutumika na watu wasioitakia mema Tanzania,” amesema Khatibu.
Khatibu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, amesema, “2026 uwe mwaka utakaotuweka pamoja Watanzania ili tupate maendeleo. Kikubwa, Serikali itoe elimu ya uraia kwa baadhi ya vijana wetu wasiojua maana ya kuwa raia mwema.”
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha NLD, Hassan Doyo, amesema anatarajia kuona mwaka 2026 unakuwa wa mabadiliko ya kisheria na kikatiba, akisema malalamiko ya baadhi ya wanasiasa na Watanzania yafanyiwe kazi.
“Uwe mwaka wa mabadiliko ili kukata kiu ya wadau wanaona kuna haja ya kufanya hivyo,” amesema Doyo.
Mbali na hilo, Doyo, aliyekuwa mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita, amesema kumekuwa na mjadala kuhusu amani na haki, lakini anaamini kuwa amani hutangulia, kisha haki hufuata.
“Kuna mawazo kinzani yanasema kunapokosekana haki amani inatoweka, unaweza kutaka amani, lakini kwa sababu haki haifuatwi, amani hiyo haiwezi kudumu. Natamani 2026 uwe mwaka wa haki, uzalendo na maendeleo yatakayozaa amani,” amesema Doyo.
Katika hatua nyingine, Mwananchi liliwatafuta viongozi waandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwemo Katibu Mkuu (Dk Asha-Rose Migiro) na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo (Kenan Kihongosi), kutaka kujua chama hicho kina salamu gani za mwaka mpya kwa Watanzania, simu zao ziliita bila kupokelewa.
