Somalind. Maelfu ya Wasomali wamejitokeza katika mitaa mbalimbali nchini humo kupinga hatua ya Israel kuitambua Somaliland, eneo lililojitangaza kujitenga ambalo Somalia inalichukulia kuwa sehemu ya ardhi yake, huku wakimlaumu Waziri Mkuu wa Israel, Benyamin Netanyahu kwa uamuzi huo.
Makundi makubwa ya watu yalikusanyika katika mji mkuu, Mogadishu jana Jumanne Desemba 30, 2025, kuelekea kwenye uwanja wa taifa, ambako viongozi wa dini waliongoza mikutano ya hadhara wakitoa wito wa umoja na kulaani hatua hiyo kama shambulio dhidi ya uadilifu wa mipaka ya Somalia.
Maandamano kama hayo yaliripotiwa pia katika miji ya Baidoa, Guriel, Dhusamareeb, Las Anod na Buhoodle, huku waandamanaji wakipeperusha bendera za Somalia na kupiga kelele za kupinga kutambuliwa Somalind.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Abdisalam Abdi Ali ameonya kuwa uamuzi wa Israel unaweza kuwa na madhara makubwa kwa ukanda mzima.
Amesema hatua hiyo inatishia usalama Afrika na maeneo ya jirani, ikiwemo Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden na inaweza kuzipa nguvu zaidi makundi yenye misimamo mikali yanayoendesha shughuli zake katika eneo hilo.
Katika mji wa Las Anod, waandamanaji walmefanya maandamano hayo na kutoa kilio chao kama ishara ya mshikamano wa kitaifa. “Ninaunga mkono umoja wa watu wa Somalia, popote walipo,” amesema mwandamanaji Mohamed Ismail.
“Tunapinga aina zote za uchokozi kutoka kwa serikali ya Israel, hasa Benjamin Netanyahu na harakati zake za Kizayuni.”
Somaliland ilitangaza kujitenga na Somalia mwaka 1991, lakini haikuwa imetambuliwa rasmi na nchi yoyote hadi wiki iliyopita. Zaidi ya mataifa 20 yameilaumu Israel kwa hatua hiyo. Somalia pia iliwasilisha suala hilo katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ikidai kuwa utambuzi huo unatishia uthabiti wa eneo hilo, madai ambayo Israel imeyakataa.
Imepita miaka 34 Somaliland bila kutambuliwa kama taifa huru na wiki iliyopita Israel ikiwa nchi ya kwanza duniani imelitambua taifa hilo.
Somalia ilitengana na Somaliland tangu mwaka 1991, eneo ambalo lenye watu zaidi ya milioni 3.
Kupitia mazungumzo ya kwenye simu viongozi hao wawili Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Rais wa Somaliland, Abdirahman Abdullahi wakati walisaini hati inayothibitisha hatua hiyo alimpongeza Rais huyo na kumwalika kutembelea Israeli.
Netanyahu aliuita urafiki kati ya mataifa hayo mawili muhimu na wa kihistoria na akazungumzia kuhusu kupanua ushirikiano katika nyanja za kiuchumi, kilimo, katika nyanja za maendeleo ya kijamii.
