Bei ya mchele Mbeya haishikiki, serikali yaingilia kati

Mbeya. Bei ya mchele katika masoko ya jijini Mbeya imeendelea kupanda, hali inayosababisha malalamiko miongoni mwa wananchi huku wataalamu wa uchumi wakieleza sababu za mabadiliko hayo na kuonesha matumaini kuwa hali inaweza kurejea kawaida ifikapo Mei, mwaka huu.

Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa wazalishaji wakuu wa zao la mpunga nchini, hususan katika wilaya za Kyela na Mbarali na hutegemewa kusambaza mchele katika mikoa mbalimbali ya Tanzania pamoja na baadhi ya nchi jirani.

Hata hivyo, licha ya uzalishaji huo, bei ya mchele imeendelea kuwa juu sokoni.

Kwa takribani miaka mitatu iliyopita, bei ya mchele ilikuwa kati ya Sh25,000 hadi Sh30,000 kwa ndoo kilo 20. Kwa sasa bei hiyo imepanda zaidi ya mara mbili kwa ujazo huo, kutegemeana na ubora wa mchele unaouzwa.

Uchunguzi uliofanywa katika soko la Sido jijini Mbeya, hususan katika mashine za kusaga mpunga, Mwananchi limebaini bei ya mchele imepanda hadi kufikia kati ya Sh55,000 na Sh70,000 kwa kilo 20, kulingana na aina ya mchele, hali inayodhihirisha ongezeko kubwa ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Mmoja wa wauzaji wa mchele katika soko hilo, Rehema Geofrey, amesema ongezeko la bei limetokana na kupungua kwa uzalishaji wa mpunga mashambani kutokana na ukame kwa  msimu uliopita.

Geofrey amesema hata bei ya mpunga shambani imepanda, gunia linalobeba debe saba linauzwa hadi Sh180,000 ikilinganishwa na Sh80,000 iliyokuwa ikiuzwa awali, hali inayochangia kupanda kwa bei ya mchele sokoni.

Hata hivyo, Geofrey amesema matumaini ya kushuka kwa bei yapo ifikapo Mei msimu wa uzalishaji utakapoanza.

Hata hivyo amesema wanaomba Mungu mvua ziendelee kunyesha kwa wingi ili kuimarisha uzalishaji.

Amesema kilimo cha umwagiliaji hakitoshekezi kustawisha zao la mpunga katika kipindi cha ukame.

Kwa upande wake, Denis Christopher amesema mabadiliko ya bei ya mchele yalianza kuonekana mwishoni mwa Oktoba mwaka jana kufuatia  matukio ya vurugu za Oktoba 29, pamoja na ongezeko la mahitaji wakati wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.

Amesema matumaini yaliyopo ni kuanza kwa msimu wa mavuno mwishoni mwa Aprili, akiwataka wananchi kutokata tamaa kwani hali ya sasa ni ya muda mfupi.

Christopher amesema iwapo hali ya hewa itaendelea kuwa nzuri, bei ya mchele inaweza kushuka hadi kufikia Sh30,000 kwa kilo 20, akisisitiza kuwa mabadiliko ya bei yaliyopo yamesababishwa zaidi na mazingira ya soko katika kipindi husika.

Naye mmoja wa wananchi wa jijini Mbeya, Lovenes Paschal amesema kutokana na ugumu wa maisha unaoendelea, serikali inapaswa kuingilia kati kuwasaidia wananchi wasio na uwezo wa kumudu gharama.

Amesema si mchele pekee uliopanda bei, bali pia bidhaa nyingine kama sabuni na sukari, jambo linaloongeza mzigo kwa wananchi.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa uchumi jijini Mbeya, Victor Kahangwa, mabadiliko ya bei ya bidhaa sokoni hutegemea hali ya uzalishaji, mahitaji ya soko na mabadiliko ya biashara ndani na nje ya nchi.

Amesema bei ya mchele iliyopo inaashiria kuwepo kwa mahitaji makubwa ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya, hadi kufikia soko la kimataifa, huku akiwashauri wananchi kuendana na mabadiliko ya kiuchumi badala ya kuishi kwa mazoea.

Kahangwa ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi nayo yana mchango mkubwa katika kupanda kwa bei ya bidhaa, akisisitiza kuwa si kila ongezeko la bei hutokana na matakwa ya mfanyabiashara mmoja mmoja.

Akizungumzia hatua za serikali, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amesema tayari serikali imeanza kuchukua hatua kwa kuwafuatilia wafanyabiashara wanaopandisha bei za bidhaa sokoni kiholela.

Amesema kuna timu maalumu zinazopita katika masoko mbalimbali kuwabaini wahusika, huku akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukiuka sheria.