Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuvuka lengo la makusanyo ya kodi katika robo ya mwaka ya Oktoba hadi Desemba, 2025, ikikusanya Sh9.8 trilioni kati ya Sh9.6 trilioni zilizotakiwa kukusanya.
Makusanyo hayo ni ufanisi wa asilimia 101.2 huku ukiwa umechangiwa na uchumi himilivi uliojengwa, ulipaji kodi kwa hiari na sera bora za kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Januari mosi, 2026 na Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda wakati akitoa taarifa ya utendaji wa makusanyo ya kodi katika robo hiyo ya mwaka.
Utendaji huu unashuhudiwa licha ya nchi kupitia katika kipindi cha misukosuko baada ya uchaguzi, iliyofanya baadhi ya biashara kufungwa kwa siku kadhaa kabla ya kurejesha tena baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuapishwa rasmi kuongoza nchi kwa miaka mitano ijayo.
Mwenda amesema katika kipindi hicho, walipakodi walitimiza jukumu lao kwa hiari wakati ambao TRA iliendeleza madawati ya kuwezesha biashara nchi nzima.
“Hali hii ilifanya utendaji kazi wa TRA katika robo hiyo ya mwaka kuwa nzuri pamoja na changamoto zilizotokea kati ya Oktoba hadi Desemba lakini haikuathiri utendaji wetu,” amesema Mwenda.
Amesema TRA katika kipindi hicho ilipaswa kukusanya Sh9.6 trilioni lakini walikusanya Sh9.8 trilioni.
“Makusanyo yalikuwa makubwa zaidi Desemba mwaka huu kwani tuliweza kukusanya Sh4.13 trilioni ikilinganishwa na Sh3.5 trilioni iliyopatikana mwaka jana,” amesema.
Amesema kiasi kilichokusanywa Desemba mwaka jana ni kikubwa kuwahi kufikiwa katika makusanyo ya kila mwezi, jambo ambalo limefanya wastani wa ukusanyaji wa mapato kwa mwezi kuongezeka kutoka Sh2.7 trilioni hadi Sh3.1 3 trilioni kwa mwezi mwaka jana.
“Ujenzi wa uchumi himilivu uliofanyika ni moja ya jambo lililofanya mapato hayo kutoteteleka, Oktoba haikushuka chini kwa kiwango kilichopaswa kukusanywa kwani tulikuwa zaidi ya asilimia 100,” amesema kamishna huyo.
Akitaja sababu ya Desemba kufanya vizuri zaidi, Mwenda amesema biashara zilifanyika kwa kiasi kikubwa kuliko miezi mingine huku mfumo wa kodi uliojengwa wenye uwezo wa kuhimili misukosuko iliyotokea ni miongoni mwa sababu.
“Tunawashukuru sana watumishi wetu waliojitoa kufanya kazi hadi mwisho wa mwaka huu,” amesema.
Amesema kukua kwa mapato hayo ni ishara kuwa nchi inaweza kujitegemea endapo wananchi wataamua kushirikiana na TRA na watumishi.
“Na tunaweza kusimama wenyewe bila kuongeza ugumu wa kodi kwa walipakodi bali kuongeza wigo wa kodi na kupunguza ukwepaji kodi huku sisi tukiimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi. Tutaendelea kuwasikliza wafanyabiashara, kushirikiana nao kuwezesha biashara zao,” amesema.
Kwa mwaka huu, Mwenda amesema wamejipanga kuongeza wigo wa kodi na kusimamia sheria ili kuweza kuondoa mapengo na kupambana na wakwepa kodi.
“Tutaboresha huduma na kuimarisha weledi wa watumishi na kusimamia uadilifu ili kuwe na usawa na kuondoa ukiritimba na urasimu,” amesema.
Amesema hilo litakwenda sambamba na usimamizi wa mfumo wa Idras ambao utasimamia malipo ya kodi za ndani na kuondoa usumbufu wa walipa kodi.
Mfumo huo utafanya mambo mengi kufanyika mtandaoni na kuondoa ulazima wa watu kwenda ofisi za TRA kufuata baadhi ya huduma.
“Mfumo huu utapunguza malalamiko ya mapitio ya kodi ambayo yanaonesha si ya haki, itaboresha huduma kwa walipakodi, tumejipanga na tutawajua walipa kodi wengi na tutakuwa na maamuzi ya kikodi yanayotegemeana na takwimu tofauti na ilivyokuwa awali,” amesema.
Akizungumzia tozo ya Ukimwi inayotozwa kupitia magari yanayoingizwa, Mwenda amesema iko kwa mujibu wa sheria baada ya kupitishwa katika bajeti ya fedha ya mwaka 2025/2026.
“Siyo mpya ilianza Julai mosi mwaka jana na inalipwa kilingana na ukubwa wa gari, inaanza Sh50,000, Sh100,000 na magari makubwa ni Sh200,000 na vifaa vikubwa ni Sh250,000. Si kodi mpya na ipo kwa ajili ya kusaidia kuboresha afua hiizi,” amesema.
Kamishna wa Forodha wa TRA, Juma Bakari amesema tozo hiyo inasaidia kujenga mfuko wa Ukimwi ambao awali ulikuwa unapata ufadhili kutoka nje.
“Lakini ufadhili huo ulikatika, hivyo tozo hii ilibuniwa ili kufidia kile kinachokosekana. Tutaendelea kuikusanya hadi mwaka wa fedha utakapoisha au utakapotangazwa tena,” amesema.
