Azam yaichapa Mlandege, yaiachia msala Singida BS

MABAO mawili yaliyofungwa katika kila kipindi, yameipa Azam FC ushindi wa kwanza katika Kombe la Mapinduzi 2026 ulioifanya kuacha msala kwa Singida Black Stars na URA.

Azam imepata ushindi huo katika mechi yake ya pili iliyochezwa leo Januari 2, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja ambapo imeiacha Mlandege ikivuliwa ubingwa kwa aibu.

Zidane Sereri alianza kuifungia Azam dakika ya sita baada ya kuunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Ashrafu Kibeku kutokea upande wa winga ya kulia.

Bao hilo la mapema, liliivuruga Mlandege ambayo imeruhusu tena bao muda huo baada ya mechi iliyopita dhidi ya URA ambapo mfungaji alikuwa Amaku Fred.

AZA 01

Mashambulizi ya hapa na pale sambamba na kuchezeana kibabe baina ya wachezaji wa pande mbili, ikahitimisha dakika 45 Azam ikiwa mbele kwa bao 1-0 dhidi ya Mlandege.

Mapema kipindi cha pili dakika ya 54, nahodha Himid Mao, akaongeza bao la pili kwa Azam lililofanikisha ushindi huo wa 2-0.

Ushindi huo unaifanya Mlandege kuvuliwa ubingwa ikiwa haijashinda mechi hata moja katika kundi A ikianza kufungwa 3-1 na Singida Black stars, kisha 1-0 na URA, ikamaliza na kichapo cha 2-0 kutoka kwa Azam.

Kwa Azam, ushindi huo unaacha msala upande wa Singida Black Stars na URA ambazo kesho Jumamosi Januari 3, 2026 zitakutana saa 10:15 jioni.

AZA 02

Singida kesho inahitimisha mechi za hatua ya makundi ambapo sasa ina pointi nne sawa na Azam, inatakiwa kushinda ili kujihakikisha kufuzu nusu fainali kwani ushindi kwao itafikisha pointi saba ambazo URA haiwezi kuzifikia.

Endapo Singida itapoteza, maana yake itabaki na pointi nne na kuiacha URA kukata tiketi ya nusu fainali ikifikisha pointi sita baada ya sasa kuwa nazo tatu zilizotokana na kuifunga Mlandege mechi ya kwanza.

Azam na URA zitahimitisha hatua ya makundi Januari 5, 2026 ambapo matokeo ya mechi hiyo yatamaliza utata wa timu gani mbili kutoka kundi A zitafuzu nusu fainali.