Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney, amewaonya watu wote waliovamia maeneo ya taasisi za Serikali kuondoka mara moja, akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria dhidi ya yeyote atakayekiuka agizo hilo.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 2, 2026 katika Kijiji cha Mwamitumai, kufuatia migogoro ya ardhi katika shule za msingi Mwamitumai, Binza na Nyabubinza, ambapo baadhi ya wananchi walijenga au kufanya kilimo katika maeneo hayo.
Dk Anney amesisitiza kuwa shule, zahanati, vituo vya afya na maeneo mengine ya Serikali yako chini ya halmashauri ya wilaya na hairuhusiwi kugawiwa au kuvamiwa na mtu yeyote.
“Serikali ya kijiji haina mamlaka ya kugawa au kuruhusu uvamizi wa maeneo ya taasisi za umma. Yeyote atakayekiuka atachukuliwa hatua kali za kisheria bila kujali nafasi yake,” amesema.
Ameongeza kuwa uvamizi huo unahatarisha usalama wa wanafunzi na wananchi, na kuchelewesha maendeleo ya huduma za jamii.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mwamitumai wilaya ya Maswa ambao walihudhuria mkutano wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk Vcent Anney (hayupp pichani). Picha na Samwel Mwanga
Dk Anney ameelekeza pia maeneo yote ya taasisi za Serikali wilayani Maswa yapimwe na kupewa hati miliki ili kulinda matumizi yake kwa sasa na vizazi vijavyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema tayari uhakiki wa mipaka ya maeneo yaliyoathirika umeanza na mipaka hiyo itapimwa kisheria ili kuzuia migogoro ya mara kwa mara.
Amesisitiza wananchi kushirikiana na Serikali kwa kuheshimu sheria, haki na uwajibikaji ili maendeleo ya kweli yafanikishwe.
Baadhi ya wananchi wamepongeza hatua hiyo. Jumanne Shija wa Mwamitumai alisema uvamizi wa ardhi karibu na shule ni hatari kwa watoto, huku Rehema Alexander wa Binza akisema hatua ya Serikali itasaidia kurejesha amani na kuboresha mazingira ya elimu.
