Arusha. Mahakama ya Rufaa ya Tanzania imebatilisha hukumu ya kifungo cha miaka 20 jela na faini ya Sh343.8 milioni aliyohukumiwa raia wa Nigeria, Okwudili Agu, kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini.
Agu alitiwa hatiani baada ya kukiri kosa la kusafirisha heroini yenye uzito wa gramu 1,273.69, yenye thamani ya Sh114.6 milioni. Alikamatwa Desemba 29, 2013 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Alipofikishwa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa awali alikana shtaka lakini miaka miwili baadaye, alikiri na kuhukumiwa adhabu hiyo.
Mshtakiwa alikata rufani Mahakama ya Rufaa akipinga hukumu, akidai alikiri kosa hilo kwa kutoelewa mashtaka kwani kipindi chote cha kesi alikuwa amekana kutenda kosa hilo.
Majaji wa Mahakama ya Rufaa Ferdinand Wambali (kiongozi wa jopo), Lilian Kairo na Deo Nangela, wamebaini kukiri kosa kwa mshtakiwa hakukufanywa kwa kufuata taratibu za kisheria, hivyo hukumu dhidi ya mrufani haikuwa sawa kisheria.
Katika hukumu iliyotolewa Desemba 29, 2025 na kupakiwa kwenye mtandao wa mahakama, majaji hao wamesema Mahakama Kuu ilifanya makosa kumtia hatiani Agu kwa kukiri kosa ilhali ukweli wa kesi haukuwekwa wazi wala kurekodiwa inavyotakiwa kisheria.
“Mahakama imejiridhisha kuwa kukiri kosa kwa mshtakiwa hakukuwa wazi na pasipo kuacha shaka, kwani ukweli wa kesi aliodaiwa kukiri haukuwasilishwa na kurekodiwa kikamilifu katika kumbukumbu za mahakama,” amesema Jaji Wambali katika hukumu hiyo.
Kutokana na hilo, mahakama imebatilisha hukumu iliyotolewa Novemba 26, 2021, imefuta hatia na kuweka kando adhabu ya kifungo na faini aliyokuwa amepewa Agu.
Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa haikumwachia huru mshtakiwa, badala yake imeamuru kesi irudishwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kuanzia hatua iliyokuwa imefikiwa Juni 19, 2019, ambapo mashahidi watatu wa upande wa Jamhuri walikuwa wameshatoa ushahidi.
Mahakama imeamuru mrufani ataendelea kushikiliwa mahabusu akisubiri kuendelea kwa kesi dhidi yake katika Mahakama Kuu.
Awali, Mahakama Kuu ilimtia hatiani mrufani kwa kosa la usafirishaji haramu wa dawa za kulevya kinyume cha kifungu cha 16(b) cha Sheria ya Dawa za Kulevya na Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Dawa za Kulevya, Sura ya 95.
Katika usikilizwaji wa awali, mshtakiwa alikana kutenda kosa. Shauri lilipelekwa Mahakama Kuu na hadi Juni 19, 2019 mashahidi watatu wa upande wa jamhuri walikwishatoa ushahidi na kuwasilisha vielelezo vitano.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za rekodi ya rufaa, kesi hiyo iliendelea Novemba 26, 2021, siku mbayo mshtakiwa alikiri hatia katika kosa hilo.
Jaji Wambali katika hukumu amesema awali, rufaa hiyo iliahirishwa kusikilizwa kwa sababu mrufani alionyesha nia ya kutafuta wakili, lakini baadaye alisitisha nia hiyo akaiomba mahakama ikubali rufaa yake na kumwachia huru.
Katika hoja zake, alidai alikiri kosa kwa sababu ya kutoelewa makosa.
Sababu nyingine alidai rekodi ya kesi inaonyesha alikiri kosa mara mbili, huku maneno yanayorekodiwa yakiwa ni tofauti.
Katika uwasilishaji wake, kwanza, amerekodiwa akisema: “Ni kweli. Ninakiri kosa”. Pili, anasema: “Bwana wangu ninakiri kosa kwa shtaka. Ni wakati”.
Mrufani alidai mbali na kurekodiwa kwamba alikiri kosa mara mbili na kukiri kosa kuliwasilishwa na mahakama ya chini, haijulikani ni kwa nini maneno anayodaiwa kusema wakati wa maombi hayo yanatofautiana na kuwa, jaji alihitimisha kimakosa kwamba ombi lake ni kinyume cha mwongozo uliowekwa, ambao lazima uzingatiwe katika kufikia uamuzi kama huo.
Ili kuunga mkono msimamo wake kuhusu mazingira ambayo madai ya kukiri kosa yanaweza kupingwa, alirejea uamuzi katika kesi kadhaa zilizoamuliwa na mahakama.
Pia alidai rekodi ya kesi inaonyesha ukweli ulioandikwa ulisomwa kwake, hata hivyo, hauonekani katika rekodi ya rufaa. Alidai rekodi ya kesi inaonyesha ni baadhi tu ya vielelezo vilivyowasilishwa, huku vingine vikiwasilishwa wakati wa kesi.
Mrufani alieleza kukiri ukweli wote kulijumuisha vielelezo vitano vilivyowasilishwa wakati wa kesi lakini hakusomewa.
Kwa kuzingatia makosa hayo, alieleza haijulikani ni ukweli gani alikiri kuwa sahihi na haiwezi kuhitimishwa kwamba mrufani alikiri ipasavyo kwamba ukweli na vielelezo vilikuwa sahihi na vya kweli.
Wakili wa mjibu rufaa alikubaliana na mawasilisho ya mrufani akaiomba mahakama ikubali rufaa hiyo, kufuta hatia na kuomba badala ya kumwachia mrufani kama alivyoomba, mahakama iwasilishe jalada hilo Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea na kesi kutoka pale ilipoishia kabla ya kuharibika.
Jopo la majaji baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, lilieleza ni muhimu kupitia mwenendo wa kesi ukiwamo wa Novemba 26, 2021 unaoonyesha mshtakiwa alikumbushwa shtaka dhidi yake na akakiri hatia na kutiwa hatiani.
Jaji Wambali amesema kabla ya mahakama kumtia hatiani mshtakiwa kwa kukiri hatia, ni lazima iridhike bila shaka kwamba, ukweli uliotolewa na upande wa mashtaka unathibitisha au kufichua vipengele muhimu vya kosa ambalo ameitwa kukiri na amekiri kweli.
Amesema muhimu zaidi, mahakama imeweka vigezo ambavyo vinaweza kuzingatiwa kabla ya kuhitimisha hoja ya mshtakiwa kuwa haina shaka, ikiweka misingi kadhaa ikiwamo mtu anaposhtakiwa, shtaka na maelezo yote yanapaswa kusomwa kwake, kadri iwezekanavyo katika lugha yake, lakini ikiwa hilo haliwezekani, basi kwa lugha ambayo anaweza kuzungumza na kuelewa.
Pia, anapaswa kuelezwa vipengele vyote muhimu vya kosa analoshtakiwa na ikiwa mshtakiwa anakubali vipengele hivyo vyote muhimu, inapaswa kurekodiwa kile mshtakiwa amesema na kisha kukiri rasmi hatia.
Jaji amesema baada ya kupitia wameona haijulikani ni kwa nini mrufani aliitwa kukiri mara mbili na katika matukio yote mawili, inadaiwa alikiri bila shaka hatia, ingawa taarifa iliyorekodiwa kuhusu ombi lake ilitofautiana.
Majaji walifikia uamuzi wa kubatilisha mwenendo wa kesi wa Novemba 26, 2021, kufuta hatia na kuweka kando hukumu iliyotolewa kwa mrufani na jalada lirejeshwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kuendelea na kesi.
