Doumbia, Conte waivimbia Yanga dirisha dogo

SAA chache tu tangu kuandika taarifa kwamba viungo wa Yanga, Mousa Balla Conte na Mohamed Doumbia walikuwa mbioni kupishana na viungo kutoka Singida Black Stars, Marouf Tchakei na Mohamed Domaro, nyota wao walitua Jangwani msimu huu inadaiwa wametia mgomo kuondoka kwenda Singida BS kwa mkopo.

Inadaiwa wachezaji wao wamebadilisha upepo kwa kugoma kutolewa kwa mkopo na badala yake wanataka wavunjiwe mikataba yao waondoke jumla, jambo lililowapa kigugumizi mabosi wa Yanga ambao wanakuna vichwa kwa sasa kwa vile mchongo wa awali haukuwa wa kuvunjiana mikataba kwa lengo la kuepuka hasara ya kifedha.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata ni kwamba awali wachezaji hao walionekana kuridhia kwenda Singida ili kupata nafasi ya kucheza, lakini ghafla wamebadilika na kutaka waachwe jumla na dili la mkopo kule Singidani hawana mpango nako kabisa kwa sasa.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga na Singida Black Stars kimeliambia Mwanaspoti, ni kweli kuna mazungumzo ya kufanyika kwa biashara hiyo ya kubadilishana wachezaji hao wanne, lakini ugumu unatoka kwa wachezaji waliopo Yanga.

“Uongozi wa pande zote mbili umefanya mazungumzo kwa ajili ya mchakato huo, lakini upande wa wachezaji ambao pia wamepewa taarifa, kumekuwa na ugumu kwani kuna ambao wanataka na wengine hawataki,” kilifunguka chanzo kutoka Singida BS.

‘’Kutoa mchezaji kwa mkopo ni makubaliano baina ya uongozi na mchezaji ambaye pia anapewa nafasi ya kufanya machaguo ni timu gani anataka kucheza hivyo hilo lipo chini ya wachezaji, lakini kwa upande wa timu na timu mazungumzo yamekwenda vizuri,” kilisema chanzo hicho.

Awali, mtoa taarifa kutoka Yanga amesema sababu za kuwatoa kwa mkopo wachezaji hao wawili ni kutokana na kushindwa kuendana na ushindani uliopo ndani ya timu licha ya kuwasajili wakiwa na matarajio makubwa kutoka kwao.

“Ni kweli kulikuwa na mpango wa kuwatoa kwa mkopo wachezaji hao, kwani kumekuwa na changamoto ya kufanya kile tulichokuwa tunakitarajia kutoka kwao lakini pia hawana namba ya kudumu kikosi cha kwanza.

“Wachezaji wamepewa taarifa kuhusiana na hilo tunasubiri majibu yao kama wataridhia kwenda timu hiyo au watakuwa na machaguo yao tofauti, lakini mchakato juu ya wao umeenda vizuri kwenye mazungumzo kwamba wanatakiwa kupisha sajili mpya.”

Kwa upande wa nyota wa Singida, Damaro pekee ndiye aliyekubali kwenda Yanga na tayari ameshatambulishwa, huku kwa Tchakei aliyewahi kuhusishwa na klabu hiyo pamoja na Simba tangu msimu uliopita inadaiwa naye ametia ngumu.

“Doumbia na Conte kila mmoja ametia ngumu kuondoka kwa mkopo, wanataka wavunjiwe mkataba wasepe kimoja klabuni, kitu kinachotuvuruga kwa sababu tukivunja mikataba tutapaswa kuwalipwa na kumbuka tumewasajili msimu huu na hawajatumika sana,” kilisema chanzo hicho.

Taarifa zaidi zinasema mabosi wa Yanga wanapambana kulimaliza jambo hilo haraka, kwa sababu lengo la kuwatoa ni kwenda kupata muda mrefu wa kucheza tofauti na walivyo kikosini ambapo hawajashawishi makocha kuwapa muda mrefu na timu inakabiliwa na mechi ngumu na muhimu za kimataifa.