Dar es Salaam. Hakika miongoni mwa ukamilifu wa kumtukuza Allah Mtukufu ni kukitukuza kila alichokifanya kuwa kitukufu miongoni mwa alama za dini na ibada. Miongoni mwa utukuzaji huo ni kuitukuza miezi mitukufu aliyoipa heshima maalumu na ameitaja katika Qur’an, ambayo ambayo ni Rajab, Dhulqada, (mfungo pili), Dhulhijja (mfungo tatu) na Muharram (Mfungo nne) .
Allah Mtukufu amesema: “Hakika idadi ya miezi mbele ya Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na miwili katika hukumu ya Mwenyezi Mungu tangu siku Alipoumba mbingu na ardhi; miongoni mwa miezi hiyo minne ni mitukufu..” (9: 36).
Kadhalika Mtume (Rehema na amani ziwe juu yake ) amesema: “Hakika wakati umerejea katika hali yake ya awali tangu siku Allah alipoumba mbingu na ardhi. Mwaka una miezi kumi na miwili, miongoni mwa hiyo minne ni mitukufu: Mitatu imefuatana, nayo ni Dhulqada, Dhulhijja na Muharram na (mmoja upo peka yake nao) ni Rajab…”.
Wanazuoni wamejitahidi kubainisha hekima ya utukufu wa miezi hii na siri ya kupangwa kwake kwa mpangilio huo. Imamu Ibn Kathir ( Allah amrehemu) amesema: “Kwa hakika miezi mitukufu imefanywa minne, mitatu imetajwa mfululizo na mmoja peke yake, kwa ajili ya utekelezaji wa ibada za Hija na Umra. Mwezi wa Dhulqaada umekuwa mtukufu, kwa sababu watu huacha mapigano ndani yake; na utukufu wa mwezi wa Dhulhijja kwa kuwa watu hushughulika na utekelezaji wa ibada ya Hijja.
Na utukufu wa mwezi wa Muharram ili watu warudi katika maeneo yao ya mbali wakiwa salama; na utukufu wa mwezi wa Rajab uliopo katikati ya mwaka ni kwa ajili ya kuzuru Nyumba Tukufu (Kaaba) na kufanya ibada ya Umra kwa wale wanaokuja kutoka maeneo ya mbali ya Bara Arabu, wazuru kisha warudi makwao wakiwa salama.”
Imamu Ibn Ashura (Allah Amrehemu) anaeleza kuwa utukufu wa miezi hii ni miongoni mwa sharia walizowekewa watu tangu zama za Nabii Ibrahim (Amani iwe juu yake), kwa ajili ya maslahi ya watu na kusimamisha ibada ya Hija.
Anasema: “Mwenyezi Mungu ameifanya Kaaba (Nyumba Tukufu) kuwa ni tegemeo la watu, na amefanya mwezi mtukufu kuwa ni sababu ya amani” (5: 97).
Mwezi wa Rajab ni miongoni mwa miezi mitukufu Imepokewa kwamba Mtume wa Allah alikuwa unapouingia mwezi wa Rajab alikuwa akisema: “Ewe Allah, tubariki katika mwezi wa Rajab na Shabaan, na utufikishe katika mwezi wa Ramadhani.” Lakini mwanazuoni Ibn Taymiyya (Allah Amrehemu), baada ya kuitaja Hadithi hii, amesema: “Haikuthibiti kutoka kwa Mtume wa Allah Hadithi yoyote nyingine kuhusu fadhila ya mwezi wa Rajab. Bali Hadithi zote zilizopokelewa kuhusu hilo kutoka kwa Mtume ni za kubuniwa (si sahihi).”
Kwa hakika, wazushi wamebuni hadithi nyingi kuhusu fadhila za mwezi huu mtukufu (Rajab), pamoja na kuuhusisha na baadhi ya ibada maalumu, kama vile swala na kufunga.
Miongoni mwa waliobainisha jambo hili ni mwananzuoni nguli wa fani ya Hadithi katika madhehebu ya imamu Shafi Ibn Hajar katika risala yake “Tabyiin Al’ajab bimaa Warada fii Fadhli Rajab”. Amesema: “Haikupokelewa hadithi yoyote sahihi inayoweza kuwa hoja kuhusu fadhila ya mwezi wa Rajab, wala kuhusu kuufunga wote, wala kufunga siku maalumu ndani yake, wala kusimama kwa ibada (Qiyaam) katika usiku maalumu wake.”
Kisha akasema kuwa hadithi zote zilizopokelewa kuhusu jambo hilo kwa ujumla wake ni dhaifu, na akabainisha hukumu yake juu ya hadithi hizo.
Na Ibn Rajab amesema: “Haikuthibiti Hadithi yoyote kuhusu fadhila ya kufunga mwezi wa Rajab si kutoka kwa Mtume, wala kutoka kwa Maswahaba wake.”
Kwa sababu hiyo, wema wengi waliotangulia walichukia kuutenga mwezi wa Rajab kwa kufuunga.
Na Abubakr At-Turtushi amelifafanua suala hili kwa kusema kwamba kuchukia kufunga Rajab kuna sababu nyingi miongoni mwa hizo:
Mosi, Ikiwa Waislamu watauzoea kuufunga kila mwaka, watu wa kawaida wanaweza kudhani kuwa kufunga mwezi wa Rajab ni faradhi kama ilivyo kwa mwezi wa Ramadhani. Pili, watu wanaweza kudhani kuwa ni Sunna iliyo thabiti.
Tatu, watu wangedhani kufunga ndani yake kuna fadhila maalumu kuliko miezi mingine, ilhali hilo halijathibiti. Ameendelea kusema: Lau ungekuwa mwezi huo una fadhila maalumu Mtume wa Allah angeufunga, au angeiamrisha Masahaba wake kufunga. Lakini kufunga siku hiyo si faradhi wala si Sunna kwa makubaliano ya wanazuoni.
Kisha akasema: Ikiwa mtu atafunga mwezi huo kwa nia ya kujizoesha (kuidhibiti) nafsi, na akaweza kuzuia njia za kuenea kwa watu dhana potofu kuwa kufunga Rajab ni faradhi au Sunna maalumu, katika hali hiyo hakuna ubaya kufanya hivyo.
Ama kutekeleza ibada ya Umra ndani ya mwezi wa Rajab, wema wengi waliotangulia wamesema kuwa ni jambo linalopendelewa (mustahab). Miongoni mwao ni khalifa Umar bin Khattaab na na mama wa Waumini Aisha ( Allah Awaridhie). 0712 6908 11
