Kamati ya usalama yafanya ziara ya kushtukiza madukani, waahidi bei kurejea ndani ya siku tatu

Mbeya. Siku moja baada ya gazeti la Mwananchi kuripoti kupanda kwa bei ya bidhaa jijini Mbeya, Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani humo, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Solomon Itunda, imefanya ziara ya kushtukiza katika baadhi ya maduka na kuwahakikishia wananchi kuwa hatua za kudhibiti hali hiyo zinachukuliwa.

Mbali na ziara hiyo, kamati imeunda timu ya wataalamu 11 watakaobaini chanzo cha kupanda kwa bei za bidhaa na kuwasilisha ripoti ndani ya saa 72, ifikapo Jumatatu Januari 5, mwaka huu, huku ikieleza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa watakaobainika kuhusika.

Hatua hiyo inafuatia taarifa ya gazeti la Mwananchi la Januari 1, 2026, lililoripoti ongezeko la bei za bidhaa sokoni, ikiwemo mchele kufikia Sh70,000 kwa kilo 20, sukari kuuzwa Sh4,000 kwa kilo kutoka Sh3,000 na sabuni mche kufikia Sh4,200, hali iliyozua malalamiko ya wananchi waliotaka Serikali kuingilia kati.

Leo Januari 2, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, akiambatana na viongozi mbalimbali wakiwamo wataalamu na vyombo vya usalama, amefanya ziara katika baadhi ya maduka na kwa wafanyabiashara ili kujiridhisha na hali ya kupanda kwa bei ya bidhaa na kutoa mwelekeo kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika katika soko la Mwanjelwa jijini Mbeya, Itunda amesema hatua hiyo imechukuliwa kufuatia malalamiko ya wananchi, hivyo kamati imeamua kufika moja kwa moja kwa wafanyabiashara na maduka kujionea hali halisi ilivyo.

Ameeleza kuwa baada ya ziara hiyo, imeundwa timu ya wataalamu 11 watakaofuatilia kwa kina chanzo cha kupanda kwa bei za bidhaa, hususan sukari, kuanzia viwandani, gharama za usafirishaji hadi uhakiki wa nyaraka za manunuzi.

“Tumeunda timu ya watu 11 wakiwamo wajumbe kutoka vyombo vya usalama na watalaamu kutoka Halmashauri zetu za Mbeya Jiji na Mbeya DC, tumewapa siku tatu ambapo Jumatatu wanapaswa kuwasilisha taarifa kwenye kamati ya usalama.

“Baada ya ripoti hiyo itatusaidia kuwajua hao wafanyabiashara wasio waaminifu wanaamua kwa makusudi kuigombanisha Serikali na wananchi wake, tutachukua hatua kwa watakaobainika kupandisha bei ya sukari na bidhaa nyingine kuchukuliwa hatua,” amesema Itunda.

Picha mbali mbali zikimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda (aliyevaa suti) akiwa na kamati ya ulinzi na usalama wakiwa katika ziara ya kushtukiza kwenye maduka ya wafanyabiashara katika soko la Mwanjelwa jijini humo kujiridhisha na kupanda kwa bei ya bidhaa. Picha na Sadam Sadick

Mkuu huyo pia amewataka wananchi halmashauri za Wilaya za Mbeya Jiji na DC kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki kifupi ambapo baada ya ripoti na hatua zitakazochukuliwa bei ya bidhaa zitarejea katika hali ya kawaida.

Mfanyabiashara wa bidhaa za jumla na rejareja katika soko la Mwanjelwa, Andrea Mahenge amesema kupanda kwa bei ya sukari hutokea kati ya miezi Machi hadi Juni kutokana na ukarabati wa viwanda.

“Hali hii hutokea mara chache sana na siyo kila siku, asilimia kubwa huwa kati ya miezi fulani kuanzia Machi, Aprili, Mei na Juni kutokana na ukarabati wa viwanda mzigo unapotoka,” amesema Mahenge.

Kwa upande wake muuza bucha katika soko hilo, Nuhu Ambangile amesema kwa sasa nyama imepanda hadi kufikia Sh11,000 baada ya changamoto ya marisho ya ng’ombe na gharama za usafirishaji.

“Mara kadhaa bei hupanda haswa kwa miezi hii kutokana na kukosekana kwa sehemu ya malisho, ambapo wenye mifugo husafirisha vijijini na kufanya sisi wauza nyama kutumia gharama kubwa, awali iliuzwa kilo moja Sh 10,000,” amesema Ambangile.

Picha mbali mbali zikimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda (aliyevaa suti) akiwa na kamati ya ulinzi na usalama wakiwa katika ziara ya kushtukiza kwenye maduka ya wafanyabiashara katika soko la Mwanjelwa jijini humo kujiridhisha na kupanda kwa bei ya bidhaa. Picha na Sadam Sadick

Naye muuza duka la rejareja, Triza Selestine amesema bidhaa nyingi zimepanda ikiwamo unga wa ngano, akieleza kuwa suala la sukari limekuwa changamoto sana hadi kwenye maduka ya jumla.

“Kwa miezi miwili nyuma haikuwa bei sana, ngano nayo imepanda kuanzia maduka ya jumla, hivyo hata mimi najikuta napata Sh1,000 katika mfuko,” amesema Triza.