Rombo. Kanisa la The Sowers Evangelical International Church limeanza ujenzi wa zahanati katika Kata ya Tarakea Motamburu, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, hatua inayolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa wakazi wa maeneo ya pembezoni na ya mpakani ya mji wa Tarakea.
Zahanati hiyo, itakayojulikana kama Zahanati ya Judwil, ikikamilika inatarajiwa kuondoa adha ya wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya na kupunguza gharama za usafiri, huku ikiboresha kwa kiasi kikubwa huduma za afya kwa jamii inayozunguka eneo hilo.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Mchungaji wa kanisa hilo ambaye pia ni msimamizi wa zahanati hiyo, Wilirk Hamis, amesema ujenzi wa zahanati unatokana na uhitaji mkubwa wa huduma za afya katika eneo la Tarakea ambalo lina mwingiliano mkubwa wa watu.
“Adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya imekuwa changamoto kubwa kwa wananchi. Kupitia zahanati hii, tunalenga kuwasaidia kupata huduma kwa karibu, kwa haraka na kwa gharama nafuu,” amesema Mchungaji Hamis.
Amesema kanisa linaendelea kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na huduma kuanza kutolewa mapema iwezekanavyo.
Aidha, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayowezesha taasisi binafsi na za kidini kushiriki katika utoaji wa huduma za kijamii, hususan sekta ya afya.
“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi. Hili limetoa fursa kwa taasisi kama sisi kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,” amesema.
Pia, amempongeza Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda, kwa kuendeleza ushirikiano mzuri na taasisi za dini na zisizo za dini katika kuwahudumia wananchi.
“Profesa Mkenda amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na taasisi mbalimbali bila ubaguzi. Msaada na ushauri wake umekuwa chachu ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” ameongeza.
Kwa upande wake, Profesa Mkenda amesema ujenzi wa zahanati hiyo ni mchango muhimu katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya wilayani humo.
Amesema Wilaya ya Rombo kwa sasa ina hospitali moja ya wilaya iliyopo Kirongo Samanga, vituo vya afya saba na zahanati 29, hali inayoonesha bado kuna uhitaji mkubwa wa huduma zaidi kutokana na ukubwa wa wilaya hiyo.
“Wilaya ni kubwa na mahitaji ya huduma za afya ni makubwa. Tunashukuru sekta binafsi kwa kusaidia kuongeza vituo vya kutolea huduma za afya,” amesema.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa Zahanati ya Judwil kutaongeza idadi ya zahanati zinazoendeshwa na taasisi binafsi kufikia 15, hatua itakayowawezesha wananchi kuwa na uhuru wa kuchagua huduma wanazozipendelea.
Kwa upande wa wananchi, Jakaya Atanas amesema ujenzi wa zahanati hiyo utapunguza gharama na hatari zinazotokana na kusafiri umbali mrefu kutafuta matibabu.
“Wakati mwingine tunalazimika kwenda hadi Hospitali ya Karume ambayo ni mbali. Kuna wagonjwa huchoka njiani kabla ya kufika,” amesema.
Naye Kastisma Kimario amesema umbali mrefu wa kufuata huduma za afya umekuwa ukisababisha baadhi ya wagonjwa kufika hospitalini wakiwa tayari katika hali mbaya zaidi.
Ujenzi wa Zahanati ya Judwil unatajwa kuwa mkombozi kwa wakazi wa Tarakea na maeneo jirani, huku ukiongeza matumaini ya kuboreshwa kwa huduma za afya na ustawi wa jamii.
