Kitendawili cha Dida, Sululu kusalia Geita

KIPA namba moja wa Geita Gold iliyopo Ligi ya Championship, Deogratius Munishi ‘Dida’ na beki Fredy Juma Sululu waliosimamishwa ghafla mara baada ya timu hiyo kutoka sare ya 2-2 na KenGold huenda wakavunjiwa mikataba kwa tuhuma zisizowekwa wazi na mabosi wa klabu.

Inadaiwa wachezaji hao walisimamishwa na kuachwa katika kikosi kilichosafiri kwenda kuvaana na Songea United, bila kuelezw sababu, jambo limewafanya wachezaji kushindwa kujua kinachoendelea, licha awalui kujulishwa kuwa watavunjiwa mikataba yao ili waondoke ktika klabu hiyo.

Ipo hivi. Mwanaspoti lilipata taarifa hizo zilizoelezwa baada ya mechi hiyo, mmoja wa kiongozi wa juu aliwaita Dida na beki huyo wakaambiwa watavunjiwa mkataba, lakini hawakuambiwa sababu, ila wakashangaa wakiachwa kwa ajili ya mechi ya jana dhidi ya Songea United.

“Alhamisi ndio ilikuwa mwisho wa wachezaji hao kuendelea kuwepo na timu, lakini yalitokea yote hayo baada ya sare ya mabao 2-2 nyumbani hivyo waliona kama wamecheza chini ya kiwango,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:

“Dida alidaka mechi 12 na hiyo haikuwa sare ya kwanza sasa sijui kipi kilitokea hadi kufikia hatua hiyo, maana amebakiza mkataba wa miezi sita alisaini mwaka mmoja.”

Alipotafutwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Gilbert Mwori amesema: “Siwezi kulizungumzia hilo, mtafute mkurugenzi ama katibu, atalifafanua kwa uzuri.”

Alipotafutwa Dida kuthibitisha ishu hiyo alijibu, “ni vizuri ukawatafuta viongozi ndio wenye nafasi nzuri zaidi ya kuzungumzia masuala ya wachezaji. Hivyo utaniwia radhi kwa jambo hilo.”

Kwa upande wa beki Juma alidai: “Siwezi kuzungumza lolote kwa sasa, ni vizuri ungewapigia viongozi hao ndio wanaweza wakawazungumzia wachezaji wao waliowaajiri.”

Geita iliyoshuka daraja misimu miwili iliyopita sambamba na Mtibwa Sugar ambayo imesharejea Ligi Kuu Bara kwa sasa, ndio inayoongoza msimamo wa Ligi ya Championship ikiwa na pointi 30 kama ilizonazo Kagera Sugar na jana timu hzo zilikuwa uwanjani katika viwanja tofauti kusaka pointi tatu katika mbio za kurudi Ligi Kuu msimu ujao.