MABINGWA watetezi wa Kombe la Mapinduzi, Mlandege FC, hesabu zinaonyesha wameumaliza mwendo katika michuano hiyo baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza hatua ya makundi.
Mlandege ilianza kufungwa 3-1 na Singida Black Stars (Desemba 28, 2025), kisha ikalambwa 1-0 na URA ya Uganda (Desemba 31, 2025) mechi zote zikichezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.
Kocha Msaidizi wa Mlandege, Sabri Ramadha China, amezungumzia vipigo hivyo akisema hawana namna, wamekubali kuvipokea huku akibainisha licha ya kutokuwa na nafasi ya kutetea ubingwa, lakini wanataka mechi ya mwisho kuimaliza kwa heshima.
China aliendelea kwa kusema, kupoteza mechi hizo kumechangiwa na kikosi chao kuundwa na nyota wengi ambao hawana uzoefu kulinganisha na wapinzani waliokutana nao.
“Tunahuzunika kuona mabingwa watetezi tumefungwa mechi mbili mfululizo, kimtazamo ni kama hatuna nafasi nzuri ya kufuzu hatua inayofuata, lakini tunakwenda kujiandaa kuhakikisha tunamaliza vizuri.
“Mazoezini wachezaji tunawafundisha vizuri, lakini kwenye mechi wanashindwa kufanyia kazi. Tuna tatizo la umaliziaji ambalo tukiwa uwanja wa mazoezi tunalifanyia kazi, ni tatizo kubwa tunaloendelea kuliboresha.
“Tumeamua kubaki na wachezaji wazawa kwani kama wazawa wasipocheza mechi hizi haitakuwa na maana yoyote, lakini wachezaji hao hawana uzoefu wa kutosha,” amesema China.
Leo Ijumaa Januari 2, 2026, Mlandege itakamilisha hatua ya makundi kwa kucheza dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kuanzia saa 2:15 usiku.
