OFISA Habari wa Singida Black Stars, Hussein Massanza, amesema moto alioanza nao mshambuliaji wa timu hiyo, Joseph Guede, unamkumbusha alivyokuwa Jonathan Sowah.
Guede ambaye amerejea Singida Black Stars baada ya awali kuitumikia kwa takribani miezi mitano msimu wa 2024-2025, ameanza vizuri kwa kufunga mabao mawili katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 inayoendelea kisiwani Unguja kwenye Uwanja wa New Amaan Complex.
Mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast, mechi ya kwanza dhidi ya mabingwa watetezi, Mlandege iliyochezwa Desemba 28, 2025, alifunga bao la mwisho katika ushindi wa 3-1, kisha akasawazisha kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Azam, Desemba 31, 2025.
Akizungumza na Mwanaspoti, Massanza amesema Guede ni mshambuliaji ambaye akiwa fiti na akapewa nafasi, kuna kitu cha tofauti huwa anakionyesha ndani ya uwanja na tayari ameanza kufanya hivyo katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026.
“Singida huwa hatusajili kwa fasheni, ukiona mtu anakuja kwetu ujue hiyo ni mali ndio maana kuna timu huwa zinakuja kupiga hodi kutaka wachezaji wetu.
“Ukimuangalia Guede anachokifanya ndani ya uwanja utaamini kile ninachokisema. Mwanzo alipokuja alishindwa kufanya vizuri kwa sababu ya majeraha, lakini tumemrudisha baada ya kujiridhisha amepona.
“Nikimuangalia Guede ananikumbusha Sowah wakati amekuja kwetu, alikuwa anafunga karibia kila mechi anayocheza, hivyo kwa namna alivyoanza naamini atafunga sana msimu huu. Kwa sasa ana wastani wa kufunga kila mechi,” amesema Massanza.
Guede ambaye aliitumikia Yanga nusu msimu wa 2023-2024 akitua dirisha dogo, alihamia Singida Black Stars mwanzoni mwa 2024-2025, lakini Desemba 2024 akaondoka na sasa amerejea kipindi hiki cha dirisha dogo.
Kwa upande wa Sowah, alitua Singida Black Stars dirisha dogo 2024-2025, akafanikiwa kumaliza Ligi Kuu Bara na mabao 13 katika mechi 14. Hivi sasa mshambuliaji huyo anaichezea Simba aliyojiunga nayo mwanzoni mwa msimu huu 2025-2026.
