Matatizo ya moyo, damu yanavyochangia vifo vya ghafla

Magonjwa ya kimya kimya yanayoweza kusababisha kifo cha ghafla,  mara nyingi yanahusiana na mfumo wa moyo na mishipa ya damu.

Katika magonjwa hayo, yale yanayohusu  kusimama kwa moyo ghafla na shambulizi la moyo, ndio vinara zaidi katika kupoteza roho za watu wengi.

Mshtuko wa moyo ni tatizo la mzunguko wa damu linalosababishwa na mshipa ulioziba, ambapo mtiririko wa damu hadi sehemu ya misuli ya moyo huzuiwa na kusababisha uharibifu.

Kwa upande wa kusimama kwa moyo, hilo ni tatizo la umeme ambapo moyo huacha kupiga ghafla na bila kutarajia na kusababisha damu na oksijeni kuacha kuzunguka hadi kwenye ubongo na viungo vingine muhimu.

Shambulizi la moyo wakati mwingine huweza kusababisha kusimama kwa moyo, lakini kitabibu ni magonjwa ya dharura tofauti.

Matatizo yote mawili yanahusishwa na vifo vya ghafla duniani kwa watu wazima wenye umri wa miaka 45 na zaidi.

Ukiacha matatizo ya moyo kwa ujumla, katika sehemu nyingine za mwili yaani ubongo na figo vinaweza kupata matatizo ya kiafya na kusababisha kifo cha ghafla.

Moyo ndio ogani kubwa inayohusika na usukumaji wa damu mwilini, matatizo yake huwa ni ya kimya kimya.

Maradhi ya moyo huwa yanapiga hatua kimya kimya pasipo kujijua kwa anayeugua, mara nyingi watu hugundulika wakiwa na matatizo ya moyo baada ya kufanyiwa uchunguzi wa jumla.

Mara nyingi kuharibika kwa mishipa ya damu katika moyo,  ni sababu kubwa inayochangia matatizo mbalimbali ikiwamo mapigo ya moyo kwenda mrama, misuli ya moyo kufa na shambulizi la moyo.

Mishipa ya damu ya moyo ya ateri ikiharibika husababisha misuli ya moyo kukosa damu kabisa au kupata kiasi kidogo sana. Uharibifu hutokana na mgando wa tando ya mafuta katika kuta za mishipa hii.

Hali hii husabisha misuli kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu kwa ufanisi wa kawaida, hupiga mapigo bila mpangilio na siku yoyote isiyojulikana ghafla moyo husimama.

Misuli ya moyo kututumka pia ni sababu mojawapo kwani husababisha vyumba vya moyo kuwa na nafasi ndogo ya kupokea damu na pia kushindwa kusukuma vizuri damu.

Sababu nyingine ni pamoja na moyo kushindwa kufanya kazi, maumbile yasiyo ya kawaida ya mishipa ya damu, hitilafu au uambukizi wa valvu za moyo na kuzaliwa na moyo wenye hitilafu.

Vile vile uwepo wa matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, upungufu wa madini kama vile magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa, wingi wa mafuta mabaya mwilini na kuwa na hitilafu ya mapigo ya moyo.

Mambo mengine ambayo hayatokani na maradhi ya moyo ni kama vile sumu, mrundikano wa taka sumu, kuzuiwa kwa njia ya hewa, kuvuta hewa chafu na ajali katika ogani nyeti.

Watu walio katika hatari kupata tatizo hili ni pamoja na wale wenye shinikizo la juu la damu, wenye kiwango kikubwa cha lehemu, wenye unene, kisukari, wavutaji tumbaku na wasiofanya mazoezi.

Usipuze unapoona dalili kama vile maumivu ya ghafla ya kifua, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida, kuchoka kirahisi, uchovu, pumzi kukatika, kuona giza, kuishiwa nguvu, kupoteza fahamu, kichefuchefu, kutokwa jasho na kukosa usingizi.

Muhimu kufika mapema katika huduma za afya unapopata dalili hizo, na jenga utamaduni wa kupima afya angalau kila baada ya miezi sita.