Mbotoni na Pazi, jela miaka 20 kila mmoja kwa kukutwa na vipande vya meno ya tembo

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu wafanyabiashara wawili Mohamed Mbotoni (47) na Abdallah Pazi (54) kutumikia kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kukutwa na kumiliki meno yenye thamani ya Sh103milioni, Mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pia, Mahakama hiyo imetoa amri ya vipande hivyo nane vitaifishwe na kuwa mali ya Serikali, ambapo vitapelekwa Maliasili.

Washtakiwa hao wakazi wa Temeke Wiles, wanakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha nyara hizo bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Walitenda kosa hilo Mei 23, 2022 katika maeneo ya Uwanja wa Taifa, wilaya ya Temeke ambapo walikamatwa na vipande vinane vya meno ya tembo, vyenye thamani ya Sh 103,099,000.05 (zaidi ya Sh103 milioni) bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Ijumaa Januari 2, 2026 na Hakimu Mkazi Mwandamizi , Geofrey Mhini, ambaye alisema kuwa mahakama imewatia hatiani mshtakiwa kama walivyoshtakiwa.

Hakimu Mhini alisema upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanane na vielelezo kadhaa ambavyo vimeweza kuthibitisha mashtaka dhidi ya mshtakiwa huyo.

“Upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka pasina kuacha shaka dhidi ya washtakiwa wote” alisema Hakimu Mhini

Akipitia baadhi ya ushahidi, Hakimu Mhini alisema  vipande hivyo vilikutwa nyumbani kwa Mbotoni vikiwa vimefichwa  kwenye banda la kuku na wote walikuwa wanafahamiana.

Alisema Mbotoni alimualika Pazi nyumbani kwake ili waweze kujadiliana na kupanga mipango ya kufanya biashara ya meno ya tembo na kwamba hata Serikali ya mtaa inajua kuwa Mutono alikuwa anafanya biashara ya meno ya tembo.

Hata hivyo, Mei 23, 2022 kikosi kazi cha Kuzuia na Kupambana na Ujangili  kilipata taarifa kuwa kuna watu wanafanya biashara ya meno ya tembo.

” Kikozi kazi kiliunda timu na mmoja wao alijifanya ni mnunuzi wa meno ya tembo na hivyo, siku hiyo mchana alimpigia simu  Mbotoni na kukubaliana kuonana mchana maeneo ya Uwanja wa taifa kwa ajili ya kuuziana meno ya tembo” allisema

Kikosi hicho kabla ya kuwenda uwanja wa taifa kwa ajili ya kukutana na Mutono, walipita kituo cha Polisi Chang’ombe kwa ajili ya kutoa taarifa na kupewa hati ya ukamataji.

Baada ya hapo walienda uwanja wa Taifa na kukutana na Mbotoni, walimkamata  na kumuweka chini ya ulinzi, huku wakisubiri mjumbe wa Sarikali za Mtaa wa eneo hilo.

” Baada ya hapo, walienda nyumbani kwa Mbotoni na kuanza upekuzi, ambapo mshtakiwa huyo alidai kuwa vipande nane vya meno ya tembo ameviweka katika banda ya kuku, hivyo waliongozana na maofisa hao na kuvichuku” alisema Hakimu, wakati akipitia baadhi ya mashahidi wa upande wa Jamhuri.

Mshtakiwa baada ya kuhojiwa alikiri kufanya biashara hiyo yeye na mwenzake Pazi na kisha hati ya ukamataji mali ilisainiiwa na washtakiwa walipelekwa kituo cha Polisi Chang’ombe kwa ajili ya mahojiano na baadae walifikishwa mahakamani.

Vipande hivyo ya meno, vilithibitishwa na ofisa wa wanyamapori kuwa vina thamani ya dola za kimarekani 45,000 ambazo ni sawa na fedha ya Kutanzania Sh 103milioni.

Washtakiwa baada ya kusomewa maelezo hayo, walikubali majina yao, umri wao, dini zao, mahali wanaoishi na siku walipofikishwa mahakamani na wamekama mashtaka yanayowakabili.

Novemba 26, 2024 washtakiwa walisome PH na kesi hiyo ilianza kusikilizwa ushahidi wa upande wa mashtaka Januari 16, 2025

Awali, kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali Christopher Olembille, aliiomba mahakama kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria kwa sababu utalii ni moja kati ya chanzo cha Mapato kwa Serikali hivyo kuua wanyama kunahatarisha Sekta hiyo.

Hata hivyo Mahakama iliwapa nafasi Mbotoni na Pazi kujitetea, ambapo washtakiwa hao waliomba wapunguziwe adhabu na kwa kuwa wanayegemewa na familia zao

Hakimu Mhini alisema kulingana shufaa alizotoa washtakiwa  na upande wa mashtaka, mahakama hiyo inawapa adhabu ya kila mmoja kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani.

” Mahakama imewatia hatiani kama mlivyoshtakiwa na kwa kesi hii adhabu ya chini ni kifungo cha miaka 20 jela, hivyo Mahakama inawahukumu kila mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 20 jela, ili iwe fundisho na haki ya kukata rufaa ipo wazi endapo hamjaridhika na uamuzi uliotolewa na mahakama hii” alisema Hakimu Mhini.