…………
CHATO
“Kutoa ni moyo wala si utajiri” ni methali ya kiswahili inayo maanisha ukarimu wa kweli hutoka moyoni na hauhusiani na kiasi cha mali ulichonacho.
Msemo huo umeonekana kuungwa mkono kwa vitendo na Mbunge wa Jimbo la Chato kusini, Pascal Lukas Lutandula, baada ya kuwatembelea wajawazito, na wazazi waliojifungua siku ya mwaka mpya 2026 kwenye kituo cha afya Bwanga, kisha kushiriki nao chakula na kuwapatia fedha taslimu kwaajili ya mahitaji yao.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa matendo ya huruma ambayo yamekuwa yakifanywa na Mbunge huyo kwa wagonjwa waliolazwa kwenye vituo vya afya jimboni humo.
Akiwa kwenye kituo cha afya Bwanga, Lutandula amewapongeza wazazi waliojifungua watoto siku ya Januari 1, 2026 huku akiwatakia malezi mema na ulinzi wa Mwenyezi Mungu katika makuzi bora ya watoto wao.
Vilevile amewatakia heri wajawazito wote wanaosubiria kujifungua katika kituo hicho cha afya na kwamba anayo Imani kubwa kuwa watajifungua salama kutokana na uwekezaji mkubwa wa serikali kwa wataalam wa afya na vifaa tiba.
Pamoja na mambo mengine, ameshiriki chakula maalumu cha jioni alichokiandaa kwaajili ya wagonjwa kisha kuwapatia kiasi cha shilingi 50,000 kila mjamzito na wazazi waliokwisha kujifungua ili ziwasaidie katika mahitaji mbalimbali ya watoto wao.
Lutandula amesema amelazimika kutumia sehemu ya kipato chake katika kumheshimu Mungu wa mbinguni, akimaanisha kuwa Imani ya kweli si tu maneno au Ibada, bali ni matendo ya huruma na msaada kwa wale wanaohitaji.
Muuguzi wa zamu katika kituo hicho, Bernado Komanya, amemshukuru Mbunge huyo kwa kuandaa na kushirikia chakula cha pamoja na wagonjwa waliolazwa eneo hilo na kwamba ameonyesha uzalendo mkubwa unaopaswa kuigwa na watu na taasisi zingine za kijamii.
Baadhi ya wanufaika wa msaada huo ambao ni mama waliojifungua, Astelia Charles na Mariam Richard, wamemshukuru Mbunge huyo kwa kuendelea kujitoa kwaajili ya wananchi wake,huku wakimtakia mema katika utumishi wake.
“Tunamwombea kwa Mungu, mbunge wetu azidi kuwa na moyo wa huruma kwa watu wote wakiwemo wajawazito, watoto wachanga na wagonjwa wengine wenye matatizo mbalimbali” amesema Astelia.


