Miili sita ajali ya Moro kutambuliwa kwa DNA

Morogoro.  Siku tatu tangu kutokea ajali iliyoua watu 10 mkoani Morogoro, ni miili minne pekee iliyotambuliwa, hali inayolazimu uchunguzi wa vinasaba (DNA) kutumika katika utambuzi kutokana na kuungua kwa kiasi kikubwa.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Dk Joseph Kway, amesema tayari timu ya wataalamu kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imewasili hospitalini hapo kwa ajili kuchukua sampuli za DNA kutoka kwenye miili hiyo, ili kuhusianisha na vinasaba vya ndugu wanaoendelea kujitokeza kuwatambua ndugu zao.

Akitoa taarifa leo Januari 2, 2026, Dk Kway amesema miili minne imetambuliwa na ndugu kwa kuwa baadhi ya viungo na sehemu nyingine za miili yao hazikuungua kwa kiasi kikubwa.

Ajali hiyo ilitokea jioni ya Desemba 31, 2025, katika Kijiji cha Maseyu, Kata ya Gwata, barabara kuu ya Morogoro – Dar es Salaam.

Sehemu ya mabaki ya Lori la mizigo lililokuwa limebeba shehena ya mbolea kutoka Dar es salaam kuelekea Mbeya baada ya kugongana uso kwa uso na basi la abiria Januari Mosi 2025 lililokuwa likitokea Msamvu kuelekea Mombo Mkoani Tanga. Picha na Jackson John.

Taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi ilisema mbali ya vifo vya watu 10, watu 23 walijeruhiwa katika ajali hiyo iliyohusisha basi la abiria aina ya Mitsubishi Fuso, mali ya Kampuni ya Bill Mawio na lori la mizigo aina ya Howo lenye tela, mali ya Kampuni ya Kikori. Magari yote mawili yaliteketea kwa moto baada ya ajali hiyo.

Basi la abiria lilikuwa likiendeshwa na Swalehe Adamzi, likitokea Stendi ya Msamvu, Morogoro kwenda Tanga, huku lori likiwa na shehena ya mbolea likitokea Dar es Salaam kwenda Mbeya.

Dk Kway amesema: “Katika ajali hii jumla ya watu 10 walifariki dunia lakini sisi katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro tulipokea miili tisa, mmoja ulihifadhiwa Kituo cha Afya Mikese na ni miongoni mwa iliyotambuliwa na kuchukuliwa na ndugu kwa ajili ya mazishi.”

Akizungumzia hali za majeruhi, amesema waliobaki hospitalini ni 17 kati ya 23 waliofikishwa hapo na afya zao zinaendelea kutengemaa.

Sehemu ya mabaki ya Lori la mizigo lililokuwa limebeba shehena ya mbolea kutoka Dar es salaam kuelekea Mbeya baada ya kugongana uso kwa uso na basi la abiria Januari Mosi 2025 lililokuwa likitokea Msamvu kuelekea Mombo Mkoani Tanga. Picha na Jackson John.

Amesema majeruhi wawili wamepewa rufaa ya kwenda Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) kwa ajili ya huduma za kibingwa bobezi, huku watatu wakiruhusiwa kurejea nyumbani kwa kuwa hali zao zinaendelea vizuri.

“Nitoe wito kwa wananchi wa Morogoro na mikoa mingine ambao wana uhakika au wana wasiswasi kuwa ndugu zao walisafiri Desemba 31 kwa kutumia barabara ya Morogoro -Dar es Salaam na kwa sasa hawapatikani kwenye simu wala hawajui walipo; wafike hapa hospitali kwa ajili ya kuchukuliwa vinasaba ambavyo vitasaidia kutambua kama miili iliyopo hapa ni ndugu zao,” amesema.

Sehemu ya mabaki ya Lori la mizigo lililokuwa limebeba shehena ya mbolea kutoka Dar es salaam kuelekea Mbeya baada ya kugongana uso kwa uso na basi la abiria Januari Mosi 2025 lililokuwa likitokea Msamvu kuelekea Mombo Mkoani Tanga. Picha na Jackson John.

Athumani Mohamed, ambaye ni mpwa wa marehemu Suwedi Spiki (28), aliyekuwa kondakta wa basi lililopata ajali, amesema amemtambua kupitia alama za miguuni na pensi aliyovaa ambayo haikuungua katika ajali hiyo.

Amesema mpwa wake alikuwa kodakta wa basi hilo lililokuwa likifanya safari kati ya Morogoro na Tanga.

Baada ya ajali kutokea, amesema familia ilifuatilia hospitalini na kuutambua mwili wake.

“Baada ya kuutambua tumekabidhiwa mwili wa kijana wetu na tunasafirisha kwenda Magole Dumila, wilayani Kilosa kwa ajili ya mazishi,” amesema.

Sehemu ya mabaki ya Lori la mizigo lililokuwa limebeba shehena ya mbolea kutoka Dar es salaam kuelekea Mbeya baada ya kugongana uso kwa uso na basi la abiria Januari Mosi 2025 lililokuwa likitokea Msamvu kuelekea Mombo Mkoani Tanga. Picha na Jackson John.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, katika taarifa kwa vyombo vya habari alieleza chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa lori kutaka kuyapita magari ya mbele yake bila ya kuchukua tahadhari, hivyo kwenda kugongana uso kwa uso na basi la abiria na kusababisha magari hayo kuwaka moto.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, leo Januari 2, 2026 amefika hospitalini kuwajulia hali majeruhi wa ajali hiyo.

Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza hospitalini hapo kutoa taarifa zitakazosaidia utambuzi wa miili ya ndugu zao waliofariki dunia katika ajali hiyo.

Wakati huohuo, Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, kufuatia vifo vya watu hao.

Kupitia taarifa ilitolewa jana na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Shaaban Kissu,  Rais Samia ametoa pole kwa familia za wafiwa na kuziombea roho za marehemu zipumzike kwa Amani na waliojeruhiwa wapate uponyaji wa haraka. Aidha, amewataka madereva na watumiaji wa barabara kuzingatia kikamilifu sheria na kanuni za usalama barabarani.