Mwaka mpya, mambo ya zamani kwa mstaafu!

Ni miaka ilee tulipokuwa tukiijenga nchi kwa jasho na damu mpaka kufika hapa, pa wawakilishi wetu wa wananchi kulipwa mshahara wa Shilingi… mama wee!… Milioni 14 kwa mwezi, wakati sisi tulioijenga nchi tukilipwa pensheni ya Shilingi… mama wee!… Laki moja na hamsini elfu! Yale yale ya ‘shamba la wanyama’!

Kwenye kuijenga nchi huko, tukakutana na hawa wenye lugha yao waliotushauri jambo moja muhimu la kuwa na kawaida ya kila mwanzo wa mwaka kuwa na utamaduni wa kujiwekea kile walichokiita ‘New Year resolutions’, ambayo ni kujiwekea mipango na mikakati ya ulichotarajia kukifanya na kukitimiza kwa mwaka mzima unaofuata.

Kilitusaidia sana wengi tuliokuwa tunaishi kwa kadri siku ilivyokucha, tukijifariji na misemo yetu kama ule wa ‘kulivuka daraja unapolifikia’! Tukajikuta tukiweka new year resolutions zetu zikiwa ni pamoja na kumaliza kibanda unachojenga kwa mbinde, kumiliki baiskeli ama kulipa deni la Shilingi nyingi mia tatu, karibu mshahara mzima, uliyokuwa ukidaiwa na Mpemba mwenye duka wa mtaa!

Yale ya binafsi ya kujiwekea new year resolutions mengi tuliyaweza. Ni baadaye sana tulipoanza kuwaza kuwa tuliokuwa tukimudu kujiwekea mikakati ya mwaka ilikuwa ni sisi ‘walalahoi’ tu, lakini kuweka new year resolutions za kitaifa ikawa ‘paukwa pakawa’ nyingi kwa waheshimiwa wahusika.

Ndiyo maana mstaafu wetu wa kima cha chini akapokea pensheni ya mwezi ya Shilingi laki moja na elfu tano kwa miaka ishirini toka astaafu, bila hata mheshimiwa mmoja anayehusika na wastaafu kujiwekea new year resolution yake binafsi kwa suala la kitaifa!

Kwamba mwaka mmoja atafanya kila awezalo kufanya ili aweze kupandisha pensheni ya wastaafu aliojenga nao nchi! Kwa kuwa waheshimiwa wetu hawana utamaduni wa kujiwekea new year resolutions kwa jambo la kitaifa, mambo yameishia kuwa ‘nehi’, chambilecho Wahindi!

Wastaafu tunaishia kuuzeshwa haraka ama kusindikizwa Kinondoni fasta tunaposikia tetesi za Watanzania kutakiwa kuchangia Shilingi milioni 100 mpaka 200 kwa kila goli moja,  rudia hapo kwa kila goli moja litakalofungwa na kijana wetu kwenye mashindano muhimu ya Afrika. Yaani vijana wetu wakifunga magoli, Shilingi milioni 10 kwa goli moja? Mama wee!

Yaani Watanzania, tukiwemo wastaafu, tutoe zawadi ya Shilingi milioni mia moja kwa kijana wetu aliyefunga goli ndani ya dakika 90, huku mstaafu wetu wa kima cha chini amepata Shilingi milioni 30 kwa miaka 40 aliyofanya kazi ya kuijenga nchi, ikiwemo kujenga viwanja vizuri vya michezo, japo sasa hivi mchezo pekee uliobaki ni kandanda, kwa wanaume na wanawake!

Yaani kijana apewe Shilingi milioni mia moja akifunga goli moja ndani ya dakika 90, na mzee wake apewe Shilingi milioni 30 kwa miaka yake 40 aliyotumia kuijenga nchi na viwanja vya michezo!

Mstaafu anaipenda sana timu yake ya Taifa, lakini hili la milioni 100 kwa goli moja kwa dakika 90 mtamsamehe, na msimfanye aombe timu ya vijana wake iwe inatoka sare tena ya kutofungana goli mechi zake zote. Isifungwe, lakini nayo isifunge goli katika dakika 90 ili Shilingi milioni 100 iyeyuke!

Wastaafu tunazihitaji sana hizi hela ili tupate nyongeza ya pensheni ya japo Shilingi laki tano kwa mwezi. Inawezekana. Ni utashi tu wa wahusika. Wastaafu wenyewe wa kima cha chini wamebaki wangapi, na itapata hasara ipi ili waweze kwenda Kinondoni kwa amani?

Vijana wetu hawawezi kuipenda nchi yao kwa Shilingi milioni 100 kwa dakika tisini. Shilingi milioni tano kwa goli, kama si milioni mbili, itawatosha vijana kuipenda nchi yao. Posho zao ziongezwe tu maradufu. Sembuli, Sunday na Kibadeni waliona fahari kuchezea tu timu ya Taifa, siyo kwa kupewa Shilingi milioni 100 kwa dakika 90!

Ndiyo maana new year resolution ya mstaafu wetu wa kima cha chini ni kuweweseka tu anapoiona Kinondoni ilee, inamjia fasta, ikihimizwa na waheshimiwa wanaoweka new year resolutions za kuwapatia vijana wetu zawadi ya Shilingi milioni 100 wakifunga goli moja katika dakika 90, huku mstaafu akipiga miayo!

Karibu tuweweseke pamoja.