Musoma. Zikiwa zimepita siku 46 tangu Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya mkoani Mara litangaze kumkamata mwanajeshi wa Marekani mwenye uraia pacha wa Kenya na Marekani akiwa na mabomu yaliyoelezwa ni hatari, hatima ya mtuhumiwa huyo bado haijawekwa wazi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi iliyotolewa Novemba 16, 2025, mtuhumiwa huyo, Charles Onkuri Ongeta (30), alikamatwa saa 6 mchana katika eneo la Sirari, mpakani mwa Tanzania na Kenya, akitokea Kenya kuingia Tanzania akiwa na mabomu aina ya CS M68.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mara baada ya kukamatwa kwake, Polisi walianza uchunguzi wa kina na kuahidi kuchukua hatua zaidi baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Novemba 16, 2025, Ongeta alikamatwa saa 6 mchana katika eneo la Sirari, mpakani mwa Tanzania na Kenya, akitokea Kenya akiwa na mabomu ya aina ya CS M68.
Polisi walisema mara baada ya kukamatwa kwake walianza uchunguzi wa kina na kuahidi kuchukua hatua zaidi baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo. Hata hivyo, hadi sasa hakuna taarifa rasmi iliyotolewa kuhusu hatua zilizochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.
Kwa siku kadhaa Mwananchi imemtafuta Kamanda Njera ili kupata maelezo kuhusu maendeleo ya uchunguzi huo, lakini simu zake zilizopigiwa Desemba 20, 2025 na mara mbili Januari 2, 2026 hazikupokelewa.
Hata alitumiwa ujumbe mfupi wa maandishi na ule wa WhatsApp pia haukujibiwa.
Hata hivyo, jitihada zingine za Mwananchi ziliendelea kwa kumtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime kuzungumzia hilo ambaye naye simu yake iliita bila kupokelewa.
Alipoulizwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Nchini (DCI), Ramadhan Kingai, kuhusu upelelezi wa tukio la mwanajeshi huyo, amesema atafutwe RPC Tarime/Rorya kuzungumzia hilo.
Alipoambiwa kuwa RPC simu haipokelewi, alisema aendelee kutafutwa.
Taarifa za awali za polisi ziliashiria kuwa Ongeta, ambaye ni Sajenti wa Jeshi la Marekani, alikuwa akisafiri kwa gari aina ya Toyota Land Cruiser lenye namba za usajili KDP 502Y, akiwa na familia yake. Katika mahojiano ya awali alidai familia yake ilikuwa inaelekea Shirati, wilayani Rorya, kumtembelea shangazi yake.
Mchambuzi wa masuala ya kijamii na usalama, Fazel Janja amesema ni muhimu vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kutoa hitimisho lolote.
“Tusikimbilie kuhukumu. Tunapaswa kujua mtu huyu alikuwa na nia gani, alikuja kufanya nini akiwa na silaha, na kama alikuwa na washirika ndani au nje ya nchi,” alisema.
Janja alisisitiza kuwa kwa mujibu wa taratibu za kidiplomasia, askari haruhusiwi kuingia katika nchi nyingine akiwa na silaha bila kibali cha mamlaka husika, na kitendo cha Ongeta kinaweza kutafsiriwa kama uvamizi.
Pia, alisisitiza kwamba kabla ya kumkabidhi Marekani, Tanzania inapaswa kuhakikisha uchunguzi umekamilika kikamilifu.
Mchambuzi mwingine wa masuala ya usalama, Chrisant Nyakitita alipongeza hatua ya polisi kumkamata mtuhumiwa na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana kulinda amani ya nchi.
“Kila Mtanzania ana wajibu kulinda amani na usalama wa taifa. Tusiruhusu kutumika kwa namna yoyote itakayoweza kuisukuma nchi kwenye machafuko,” amesema.
Mkazi wa Manispaa ya Musoma, Samuel Bwana, amesema tukio hilo ni ishara ya haja ya kuongeza ulinzi na uangalizi katika mipaka.
“Tusidhani kila mtu anatupenda. Matukio kama haya yanapaswa kutumika kama funzo la kuongeza umakini ili kuzuia maadui kutumia mianya iliyopo,” amesema.