Othman ataka Taifa lijengwe juu ya haki, Katiba 2026

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, ametumia salamu za Mwaka Mpya 2026 kuwataka Watanzania kuutumia kama fursa ya kuliponya Taifa, kurejesha misingi ya Katiba na kujenga umoja wa kitaifa unaotokana na haki, uwajibikaji na ridhaa ya wananchi.

Katika salamu alizozitoa Januari mosi, 2026, amesema licha ya majaribu, mitihani na maafa makubwa yaliyotokea mwaka 2025, bado nchi ilisimama na kupata nafasi ya kutafakari mustakbali wake.

Amewapongeza Watanzania waliochangia kurejesha utulivu nchini, akisisitiza utulivu uliopo haupaswi kuchukuliwa kama ishara ya furaha au amani ya kudumu.

“Pamoja na kwamba sote tunafahamu kuwa utulivu uliopo si kielelezo cha furaha wala amani endelevu katika nchi, lakini si sawa na vurugu na inatupa fursa nyingine ya kujenga mustakbali mwema wa Taifa endapo kila mmoja wetu kwa nafasi yake atakuwa na dhamira ya dhati na kutimiza wajibu wake kwa ukweli na nia safi kwa masilahi ya Taifa,” amesema.

Vilevile, amewapongeza waliothubutu kupaza sauti kupinga ufisadi, ukiukwaji wa Katiba, sheria, maadili na taratibu, akisema matendo hayo yamesababisha madhara makubwa kwa Taifa, ikiwemo kupoteza uhai wa watu, mali za raia na kuchafua taswira ya Tanzania kimataifa.

Akirejea matukio ya mwaka 2025 na miaka ya nyuma, Othman amewataka viongozi wenye mamlaka kutambua kuwa Taifa linahitaji kujengwa upya juu ya nia njema na dhamira ya dhati, akisisitiza hakuna Taifa linaloweza kuendelea endapo wananchi hawana haki ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa, wala kuwawajibisha viongozi wao.

“Niwasihi, kwa kupitia salamu hizi, tuutumie mwaka mpya wa 2026 kuchukua hatua za kuliponya Taifa na kulirejesha kwenye mstari sahihi.  Ni wakati kwa wenye mamlaka kutanabahi kuwa yaliyotokea yametufunza jambo moja muhimu, nalo ni kuwa tunahitaji kuchukua hatua za kujenga misingi ya Taifa kwa nia njema na kwa dhamira ya dhati,” amesema.

Amesema kunahitajika hatua za kuliunganisha Taifa: “Tuachane na dhana ya kuwa Taifa hili, wenye haki na hadhi ya kuliongoza ni kikundi, jumuiya au chama fulani pekee. Tukubali kuwa wenye haki ya kikatiba, wenye mamlaka ya kuamua nani waendeshe nchi na mamlaka zake mbalimbali ni wananchi wa Tanzania kama ilivyoelezwa waziwazi katika Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Ibara ya 9 ya Katiba ya Zanzibar.”

Amesema wajibu wa kikatiba na hata wa kimaadili wa viongozi ni kuhakikisha wananchi wanapewa fursa ya kutimiza haki yao hiyo. 

“Sheria, amri na hatua yoyote ya kiutawala inayoweka kikwazo katika hilo, ndiyo chanzo cha kuchafua amani katika Taifa.  Adui yetu namba moja ni yeyote anayetumia nafasi au wadhifa wake kukwaza haki hiyo ya msingi ya raia,” amesema.

Othman amesema hakuna maendeleo ambayo unaweza kujinasibu nayo katika mazingira ambayo wananchi hawana haki ya kuamua nani awaongoze, kuchagua wala kuchaguliwa na kuwawajibisha viongozi wenye kushikilia ofisi za umma. 

“Wananchi kuwa katika hali hiyo ni sawa na kuwa katika utumwa na hakuna maendeleo ya Taifa la watumwa,” amesema.

Amewataka raia kuhakikisha wanajenga mfumo wa kikatiba, wa kisheria, wa kimaadili na kiuendeshaji ulio madhubuti na ambao hautalirejesha Taifa katika utawala wa utashi wa mtu mmoja au kikundi kilichojitwalia mamlaka ya nchi, kwa mgongo wa Katiba au sheria ambayo kwa ukweli haikufuatwa wala kuzingatiwa. 

Kuhusu Zanzibar, amesema kutokuwapo maafa makubwa ya vifo baada ya uchaguzi mkuu kulitokana na uamuzi wa busara wa Wazanzibari wa kujizuia, licha ya madai wizi na ukiukwaji mkubwa wa sheria katika siku za uchaguzi wa Oktoba 28 na 29, 2025.

Amesema hatua za kisheria na kisiasa zinazochukuliwa na ACT-Wazalendo zinalenga kutafuta suluhisho la kudumu kwa njia ya amani, hata kama ni kwa gharama ya subira kubwa.

“Serikali ya Umoja wa Kitaifa ililetwa ili kutoa fursa, kutoa jukwaa rasmi kwa Wazanzibari kujenga amani ya kweli, umoja, mshikamano na maridhiano ya kitaifa.

“Serikali ya Umoja wa Kitaifa haikuanzishwa kwa madhumuni ya kutumiwa kuiba uchaguzi ili baadaye aliyeiba uchaguzi amkaribishe mshindi halali aliyeporwa ushindi wake katika Serikali ambayo haikutokana na ridhaa ya umma ili kujipa uhalali,” amesema.

Kwa upande wa chama chake, amewapongeza viongozi na wanachama kwa kazi kubwa waliyoifanya mwaka 2025, akisema licha ya mazingira magumu ya uchaguzi, kimeendelea kuwa imara na mshikamano umeongezeka.

“Dhamira yetu ni kuendelea kushiriki katika harakati za mageuzi ya kuliponya Taifa na kulirudisha kwenye mstari, ikiwemo kuhakikisha uwajibikaji kwa yaliyotokea, kwa kushirikiana na wadau wote makini,” amesema.