Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeonya uwepo wa mvua na radi kwa kipindi cha Januari 1 hadi 10, 2026, huku vipindi vya mvua vikitarajiwa katika baadhi ya maeneo ya Tanzania.
Utabiri huu unalenga kuwaonya wananchi na kuwahimiza kuchukua tahadhari stahiki, hasa pale mvua zinapochanganyika na ngurumo za radi.
Maeneo yanayotajwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi ni mikoa ya ukanda wa ziwa Viktoria abayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara.
Kwa upande wa nyanda za juu Kaskazini-Mashariki
mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro itapata vipindi vya mvua machache, hasa katika siku tano za mwanzo za Januari.
Pwani ya Kaskazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani ya Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba vinatarajiwa kupata mvua
“Magharibi mwa Nchi, mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora inatarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo,”taarifa hiyo imeeleza
Kanda ya Kati yaani mikoa ya Dodoma na Singida itapata mvua zinazoambatana na radi, hususan katika siku tano za mwanzo za Januari.
Pia, Nyanda za juu Kusini-Magharibi mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa inatarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo.
Nako mikoa ya Pwani ya Kusini inayojumuisha Mtwara na Lindi kulingana na taarifa ya TMA itapata vipindi vya mvua machache. Wakulima wanashauriwa kuzingatia ratiba za mvua ili kuepuka hasara ya mazao.
Kanda ya Kusini mikoa wa Ruvuma na maeneo ya kusini mwa Morogoro yanatarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo.
