Nairobi. Watu wengi hugundua kuwa wana kiwango cha juu cha lehemu (cholesterol) wakiwa wameshachelewa sana. Awali hawakubaini tatizo lolote.
Unajua kwa nini? Ni kwa sababu hakuna maumivu, hakuna ishara za kutisha, wala dalili za ghafla zinazokuonya kuwa kuna jambo hatari linaendelea kujengwa ndani ya mwili wako.
Unajisikia sawa. Unaonekana mzima. Unaendelea na shughuli zako za kila siku kama kawaida.
Lakini ndani ya mishipa yako ya damu, kuna simulizi inayoandikwa polepole na kwa ukimya.
Ni simulizi inayoeleza iwapo moyo wako na ubongo wako vitafanya kazi vizuri kwa miongo mingi ijayo, au iwapo siku moja vitaacha kufanya kazi ghafla bila onyo kwako.
Lehemu iko katikati ya simulizi hiyo, lakini kwa bahati mbaya imeeleweka vibaya na watu wengi. Wengine huamini kuwa cholesterol ya juu huwapata tu watu wanaokula vibaya au kupenda vyakula vya mafuta kupita kiasi.
Wengine hudhani kuwa ukiwa mwembamba, kijana, au mwenye mazoezi ya mara kwa mara, hali hizo ni kinga kamili dhidi ya tatizo hili.
Hata hivyo, madaktari huona hali tofauti kabisa kila siku: watu wenye uzito wa kawaida, wataalamu vijana, wanariadha, na hata wale wanaojitahidi kula kwa afya hubainka kuwa viwango vya lehemu vilivyo juu kuliko inavyotarajiwa.
Sababu moja kubwa ni vinasaba. Urithi wa kifamilia una nafasi kubwa sana. Magonjwa kama familial hyperlipidemia, ambayo hapo awali yalionekana kuwa nadra, sasa yanaonekana mara nyingi zaidi.
Katika hali hii, mtu anaweza kuonekana mwenye afya kamili kwa nje, lakini ndani, mishipa yake ya damu inazidi kuwa myembamba polepole bila yeye kujua.
Ndani ya damu, lehemu husafiri katika chembe zinazoitwa lipoproteini. Kuna aina mbili kuu zinazozingatiwa sana kitabibu. Low-Density Lipoprotein (LDL), maarufu kama lehemu mbaya”, hubeba lehemu hadi kwenye tishu za mwili, lakini inapozidi, hujikusanya kwenye kuta za mishipa ya damu.
Aina ya pili ni High-Density Lipoprotein (HDL), au “lehemu nzuri”, ambayo husaidia kuondoa lehemu iliyozidi na kuirudisha kwenye ini ili itolewe nje ya mwili.
Pia kuna ‘triglycerides’, ambazo ni aina ya mafuta yanayotumika kama chanzo cha nishati. Kiwango chake kinapokuwa juu kupita kiasi, huchangia kwa kiasi kikubwa kutengeneza tabaka la mafuta (plaque) ndani ya mishipa. Kadiri muda unavyopita, tabaka hili hukomaa na kuwa gumu, likifanya mishipa iwe myembamba, migumu, na dhaifu zaidi.
Mtiririko wa damu huanza kuwa mgumu, na siku moja, damu inaweza kuganda ghafla katika eneo lisilotarajiwa.
Ikiwa mgando huo utaziba mshipa wa moyo, husababisha mshtuko wa moyo. Ukiziba mshipa wa ubongo, kinachotokea hapo ni kiharusi.
Ukikatiza mtiririko wa damu kwenye miguu, husababisha ‘acute limb ischemia’ yaanio hali ya dharura kali inayoweza kusababisha ulemavu au hata kupoteza kiungo.
Madaktari wengi hutamani watu wengi zaidi wangeelewa kuwa sehemu kubwa ya matatizo haya yanaweza kuzuiwa. Mabadiliko ya mtindo wa maisha na lishe bado ni silaha zenye nguvu zaidi katika kudhibiti lehemu na kuboresha mzunguko wa damu.
Cha kufurahisha ni kwamba tatizo si wanga pekee, licha ya umaarufu wa lishe kali za kupunguza au kuondoa wanga kabisa.
Kwa baadhi ya watu, kuondoa wanga kabisa kunaweza hata kufanya cholesterol iwe mbaya zaidi. Jambo la msingi ni ubora wa chakula kama vile aina ya wanga na mafuta tunayochagua kula.
Nafaka zisizokobolewa, kunde, mboga za majani, karanga, na vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi husaidia kupunguza LDL. Mafuta tunayopika nayo pia yana umuhimu mkubwa. Mafuta yenye manufaa kwa moyo kama mafuta ya zeituni au canola yana faida iwapo yatatumika ipasavyo.
Hata hivyo, mafuta yanapopashwa moto mara kwa mara au yanapokuwa duni kwa ubora, hupoteza virutubisho na huchochea uchochezi (inflammation) na uundaji wa plaque kwenye mishipa.
Sayansi ya chakula imepiga hatua kubwa, lakini bado lishe haijachukuliwa kwa uzito unaostahili katika kaya nyingi.
Mazoezi ya mwili ni nyenzo nyingine muhimu lakini mara nyingi hupunguzwa thamani. Shughuli rahisi kama kutembea kwa kasi, kuendesha baiskeli, kufanya mazoezi ya viungo, sarakasi, au kuogelea huimarisha mishipa ya damu, huboresha mzunguko wa damu, na kusaidia kurekebisha uwiano wa lehemu.
Watu wengi hawahusishi dalili kama miguu kuwa baridi, ganzi kwenye vidole, maumivu yasiyoeleweka ya miguu, au uvimbe na matatizo ya mzunguko wa damu.
Hata hivyo, dalili hizi za awali hazipaswi kupuuzwa. Zinaweza kuashiria Peripheral Artery Disease (PAD), hali inayotokea mishipa ya miguu inapozidi kuwa myembamba. PAD si tatizo la miguu pekee; ni onyo kali kwamba mfumo mzima wa moyo na mishipa uko hatarini.
Uvutaji wa tumbaku, kwa aina yoyote ile unaendelea kuharibu mzunguko wa damu. Nikotini husababisha mishipa ya damu kukaza, huharibu tabaka la ndani la mishipa, hupunguza kiwango cha oksijeni kwenye damu, na huongeza hatari ya damu kuganda.
Kwa mtu mwenye cholesterol ya juu, mchanganyiko huu ni hatari zaidi, ukigeuza mishipa iliyobana kidogo kuwa bomu linalosubiri kulipuka.
Upimaji wa mara kwa mara wa lehemu unatoa fursa ya kuingilia kati mapema. Wagonjwa hupewa ushauri wa mabadiliko ya mtindo wa maisha na, inapohitajika, kuanzishiwa dawa za kupunguza hatari ya mshtuko wa moyo na kiharusi.
Wakati mwingine, mabadiliko ya lishe na mazoezi pekee hayatoshi, hasa kwa watu wenye matatizo ya kurithi kama familial hyperlipidemia. Katika hali hizi, dawa huwa muhimu.
Dawa hizi husaidia kuimarisha plaque, kupunguza uchochezi, na kwa kiasi kikubwa kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo na mishipa.
Habari njema ni kwamba viwango vya lehemu vinaweza kuboreka kwa haraka zaidi kuliko watu wengi wanavyodhani. Ndani ya wiki chache baada ya kubadilisha lishe na kuongeza mazoezi, maendeleo yanaweza kuonekana. Ndani ya miezi michache, mabadiliko yanaweza kuwa makubwa.
Virutubisho (supplements) vinaweza kuonekana kuvutia, lakini vingi havidhibitiwi vizuri, vina ufanisi usiotabirika, au vinaweza kuingiliana na dawa. Tahadhari ni muhimu na kumbka kile kinachoitwa “asili” si lazima kiwe salama kila wakati.
Lehemu ya juu na mzunguko duni wa damu mara nyingi huitwa matatizo “ya kimya”, na yasiyoonekana. Yanaonekana katika maamuzi yetu ya kila siku kupitia mafuta tunayopikia, vyakula tunavyoandaa kwa haraka, matembezi tusiyotaka kuyafanya, sigara tunazotumia siku zenye msongo wa mawazo, vipimo vya afya tunavyochelewesha, na historia ya familia tunayopuuzia kwa sababu tunajisikia vijana na wenye nguvu.
Lakini maamuzi hayo hayo pia yana nguvu ya kuandika upya simulizi zetu za maisha.
Katika dunia ambako magonjwa ya moyo bado ni tishio kubwa, kudhibiti cholesterol si suala la kuishi maisha yenye vikwazo. Ni kuhusu kulinda mitambo ya kimya inayofanya kila kitu kiendelee kama vile moyo unaopiga kwa uthabiti, ubongo unaofanya kazi kwa uwazi, na damu inayotiririka kwa uhuru kila sehemu ya mwili.
Mabadiliko madogo lakini ya kudumu leo yanaweza kumaanisha miaka mingi ya maisha yenye nguvu, afya na uhai kesho.
Dk Mzee Ngunga ni daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya moyo na mishipa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan. Makala iliyoboreshwa kwa hisani ya tovuti ya nationmedia.