Upelelezi kesi ya kusafirisha vinyonga mbioni kukamilika

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kusafirisha vinyonga 164, mijusi 20 na nyoka sita, inayomkabili mshtakiwa Eric Ayo na wenzake wawili, upo hatua za mwisho kukamilika.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo wakati kesi hiyi ilipoitwa kwa kutajwa.

Ayo na wenzake wawili wanakabaliwa na kesi ya Uhujumu Uchumi namba 23/2021 yenye mashtaka matatu yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kusafirisha nyara za Serikali pamoja na kutakatisha fedha, linalimkabili Ayo pekee yake.

Kasala ametoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.

“Kesi imeitwa kwa kutajwa na upelelezi wake upo katika hatua za mwisho kukamilika, kwa sababu hiyo tunaiomba mahakama yako ipange tarehe nyingine kwa kutajwa na kuangalia kama umekamilika,” amedai Kasala.

Hakimu Magutu alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 13, 2026 kwa kutajwa.

Mbali na Ayo, washtakiwa wengine ni Ally Ringo na Aziz Ndago, ambao kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha nyara hizo zenye thamani ya Sh20milioni bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kati ya Desemba mosi 2020 na Januari Mosi, 2021 katika mkoa wa Morogoro, Tanga na Dar es Salaam, washtakiwa wanadaiwa kupanga na kuongoza genge la uhalifu kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza nyara za Serikali bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.

Shtaka la pili ni kukutwa na nyara za Serikali tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Desemba mosi, 2020 na Januari Mosi, 2021 katika maeneo ya Tanga, Morogoro na Dar es Salaam.

Inadaiwa katika kipindi hicho, washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakikusanya, kusafirisha na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vinyonga 164, Mijusi 20 na nyoka 6, wote wakiwa na thamani ya Sh20milioni, mali ya Serikali,

Pia washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa na dola za kimarekani 9000 ambazo ni sawa na fedha ya kitanzania Sh19.8milioni, kwa wakati huo walipokamatwa.

Shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha linalomkabili Ayo, peke yake, ambapo Januari 26, 2021 katika benki ya CRBD iliyopo Msamvu mkoani Morogoro, kwa makusudi alibadilisha fedha dola za kimarekani 400 kwenda fedha ya Kitanzania na kupata Sh923,600, wakati akijua, fedha hizo zilikuwa zimetokana na uuzaji wa nyara za Serikali.

Hata hivyo, mshtakiwa Ayo, amerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 16, 2021 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.