URA wana jambo lao, kocha asimulia mateso waliyopitia

URA FC ya Uganda imeanza vizuri michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mlandege, lakini kuna kitu kocha wa kikosi hicho amekisimulia.

Aliyetoa simulizi hiyo ni kocha mkuu, Mbalangu Hussein aliyesema haikuwa rahisi kufika Unguja na kupata ushindi huo kutokana na changamoto kubwa waliyokutana nayo wakati wa safari.

Kocha huyo amesema, kutoka Kampala nchini Uganda hadi Dar es Salaam, walitumia takribani siku mbili kwani wamesafiri kwa gari kwa umbali wa kilometa 1,498.

“Sio rahisi kusafiri kwa gari kutoka Kampala hadi Dar es Salaam ambapo ni takribani kilometa 1,498, tulitoka kwa kuchelewa na tumefika Jumatatu, kisha Jumanne tukafanya mazoezi ya mwisho na Jumatano tukaingia uwanjani kucheza.

“Tunachoshukuru tumeshinda lakini hatukucheza kwa kiwango kizuri. Ukiangalia wachezaji wangu walikuwa wamechoka sana, hawakuwa fiti kupambana dakika zote tisini, ilikuwa ngumu sana kutokana na tulichopitia,” amesema kocha huyo.

Pia amebainisha kwamba baada ya sasa kupata muda mwingi wa kupumzika, wana kila sababu ya kufanya vizuri zaidi na kubeba ubingwa.

“Mechi inayofuatia naamini itakuwa nzuri zaidi, tutakuwa tumejiandaa vizuri. Tumekuja hapa kwa ajili ya kushindana na kuwa mabingwa,” amesema kocha huyo.

URA inajaribu kupambania ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya pili baada ya kufanya hivyo mwaka 2016 ikiifunga Mtibwa Sugar mabao 3-1 katika mechi ya fainali.

Timu hiyo kutokana na kuchelewa kufika kituo cha mashindano, mechi ya kwanza kundi A dhidi ya Azam ambayo ilipangwa kuchezwa Desemba 28, 2025, imesogezwa mbele hadi Januari 5, 2026. Kabla ya kukutana na Azam, Januari 3, 2026 itacheza dhidi ya Singida Black Stars.