Mpwapwa. Serikali imetangaza usafiri wa treni ya mwendo kasi (SGR) utaanza kesho jioni.
Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Januari 2, 2025 na Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbalawa wakati akizungumza na wananchi wa Gulwe wilayani Mpwapwa.
Waziri Profesa Mbalawala ametaja sababu za kusimamishwa usafiri huo ni kufanya uhakiki wa miundombinu ya reli yote kwa baadhi ya maeneo waliyokuwa na mashaka.
Ametaja eneo la Kidete Wilaya ya Kilosa kwamba lilikuwa na changamoto kidogo kwenye tuta la reli ambako mafundi wanaendelea kukamilisha.
“Niwahakikishie Watanzania kuwa kesho jioni usafiri wa SGR utarejea kama kawaida bila shida na watu wetu watambue ni lazima tujiridhishe kazi ambayo tumefanya na kuona tuko salama,” amesema. Profesa Mbalawala. Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amewataka Watanzania kuacha kusikiliza alichokiita propaganda za watu kuhusu usafiri wa treni ya mwendo kasi kwa kuwa unahusu maisha ya watu wengi.
Waziri Mkuu amesema hata katika mataifa makubwa treni na ndege kwenye usafiri nyakati za mvua na theruji huwa ni shida.
“Hata katika baadhi ya Mataifa makubwa kuna baadhi tangu Krismasi hawajawa na usafiri wa treni kutokana na changamoto za mvua, huwezi kusafirisha chombo kinachobeba maisha ya watu bila kuwa na uhakika,” amesema Dk Nchemba.
Waziri Mkuu ametaja chanzo cha uharibifu mkubwa wa Miundombinu ni uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti akitaka jambo hilo liwekewe mkakati wa haraka kuanzia serikali za vijiji.
Pia, Waziri Mkuu amewaagiza Wakala wa Barabara nchini (Tanrods) kuweka kambi eneo la Godegode ili kufanya tathmini ya ujenzi wa daraja ambalo linatenganisha majimbo ya Kibakwe na Mpwapwa.
Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi ambaye ni Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene amesema mkakati wa Serikali wa kujenga mabwawa unaweza usiwe suluhisho kama hautakuwepo mpango wa kupunguza kasi ya maji kutoka milimani.
Simbachawene amemuomba Waziri Mkuu kuruhusu wataalamu wafanye tathmini siyo kutegemea mabwawa ya zamani ambayo yanapokea wingi wa maji yakiwa tayari yamepita kwenye reli.
Kwa mujibu wa Simbachawene ikolojia imebadilika kati ya zamani na sasa, hivyo kauli za kuwa wakijenga mabwawa yatasaidia kumaliza tatizo haitakuwa sawa kama hawataanzia milimani.
