Kibaha. Baadhi ya wakazi wa Kata ya Visiga, Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, wamelalamikia upatikanaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri.
Wamesema kuwa kila wanapofuatilia maombi yao, huambiwa fedha tayari zimeshatolewa, jambo linalosababisha kutoridhika na kutokuwepo kwa uwazi kwa walionufaika.
Hali hiyo ilisababisha mjadala mkali wakati wa mkutano wa hadhara ulioongozwa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk Nicas Mawazo, ambapo wakazi wameeleza hofu yao kuhusu hatma ya mikopo hiyo na kutopewa majibu ya wazi licha ya kufuata taratibu zote.
Malalamiko hayo yametolewa leo Ijumaa, Januari 2, 2026, katika mkutano uliofanyika kata hiyo, ambapo wakazi Amina Mwakafwila na Anna Mwinyikondo walisema licha ya kuandaa vikundi na kukidhi masharti yote, wamekuwa wakikosa majibu ya wazi kuhusu hatma ya maombi yao ya mikopo.
“Tunaomba mikopo kwa kufuata taratibu zote, lakini kila tukifuatilia tunaambiwa fedha zimeshatolewa. Hatuoni uwazi kuhusu ni vikundi gani vimepata na lini,” alisema Mwakafwila mbele ya hadhara.
Akijibu hoja hizo, Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Visiga, George Nipadon, amesema mikopo hiyo inaendelea kutolewa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, akibainisha kuwa tangu Serikali ilipofanya maboresho na kuurejesha mfuko huo kwa awamu ya pili, zaidi ya Sh100 milioni zimetolewa kwa vikundi nane katika kata hiyo.
Matukio mbalimbali ziara ya Meya wa Manispaa ya Kibaha. Picha na Sanjito Msafiri
“Mikopo ipo na imetolewa. Hakuna fedha iliyopotea. Changamoto iliyopo ni uelewa mdogo kwa baadhi ya waombaji pamoja na idadi kubwa ya wanaohitaji mikopo ikilinganishwa na fedha zilizopo,” amesema Nipadon.
Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk Nicas Mawazo, amesema changamoto kubwa inayoikabili Halmashauri ni urejeshaji hafifu wa mikopo hiyo, akieleza kuwa baadhi ya wanufaika wamekuwa hawarejeshi kwa wakati, huku wengine wakijificha nyuma ya majina ya vyama au makundi ya kijamii, jambo alilosema ni kinyume cha sheria.
Amewataka wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 kuhakikisha wanarejesha fedha hizo kwa wakati ili kutoa fursa kwa vikundi vingine kunufaika, akisisitiza kuwa Halmashauri itaendelea kusimamia kwa karibu mfuko huo ili utimize lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
